Change Language: English

TUKIO LA ASHURA NA SABABU ZAKE

Katika mwaka wa 41 H., Muawiya alichukua madaraka kwa kutumia njia za rushwa, umwagaji damu, vitisho na udanganyifu. Imam Hasan (a) baada ya kuwa khalifa kwa miezi sita tu baada ya baba yake, alilazimika kumuachia Muawiya madaraka kwa masharti. Sababu ya kuachia madaraka ni jeshi lake ambalo halikuwa tayari kupigania haki bali lilikuwa limejaa wanafiki ambao wanashirikiana na Muawiya na walikuwa tayari kumsaliti Imam Hasan (a). Utawala wa Muawiya na mwanae Yazid (l.a.) ulitegemea nguvu za upanga. Walitumia nguvu za ukatili, kuhakikisha wanatawala Ummah wa Kiislamu kwa njia zozote zile za haramu.

Kabla hajafariki, Muawiya alimchagua mwanae Yazid (l.a.), ambae sifa zake zimetajwa, kuwa khalifa wa Mtume na Amiri wa waumini! Katika mwaka wa 60 H., anapofariki Muawiya, Yazid (l.a.) akachukuwa madaraka na akajitangaza kuwa ni kiongozi wa Ummah wa Kiislam. Popote watu walipokataa utawala wake alitumia rushwa, vitisho na ukatili ili kusimika utawala wake. Kama vile baba yake Muawiya, Yazid (l.a.) alitumia kila njia za hila na ujanja. Baada tu ya kuingia madarakani, Yazid (l.a.) alituma barua akimuamrisha Walid gavana wa Madina, kuchukua kiapo cha utii (bay‘a) bila masharti, kwa wote walio na mamlaka na hususan Imamu Husayn (a). Alipeleka barua hiyo ikiwa na amri kwamba ikiwa Imamu Husayn (a) atakataa kula kiapo cha utii (bay‘a) kwa Yazid (l.a.) auawe, na kichwa chake kikatwe na kipelekwe Dameshki, Syria kwa Yazid (l.a.).

Ilikuwa ni muhali, haiwezekani kabisa, kwa mtu kama Imamu Husayn (a) kumkubali mtu kama Yazid (l.a.) kuwa kiongozi wa Waislamu na kuwa na mamlaka juu ya Uislam. Imamu Husayn (a) alipoitwa na Walid (gavana wa Madina) na kutakiwa atoe kiapo cha utii kwa Yazid (l.a.), alikataa katakata na kuweka wazi msimamo wake:

“Ewe gavana! Sisi ni watu wa Nyumba ya Utume, na machimbo ya Utume, na mahali wanaposhuka Malaika; kwa sisi ndiyo Allah amefungua na ni kwa sisi ndiyo atahitimisha. Ama Yazid (l.a) ni mtu mnywaji pombe, muuaji, anamwaga damu za watu wasio na hatia, fasiki kwa wazi, mfano wangu hawezi kula kiapo cha utii kwa mfano wake, Yazid ...”

Kwa nini Sayyidna Husayn (a) alisimama dhidi ya Maluuni Yazid (l.a.) na kukataa kula kiapo cha utii?

Imamu Husayn (a) alielewa kwamba kula kiapo cha utii kwa Yazid (l.a.) kusingeleta faida yeyote kwa Ummah wa Kiislamu bali kungehatarisha uhai wa Uislamu. Imam alikuwa hana uchaguzi bali kuulinda na kuuchunga Uislam na kukabiliana naYazid (l.a.) na madai yake ya kuwatawala Waislamu hata ikibidi kujitolea muhanga maisha yake na ya wafuasi wake wapendwa.

Kumkubali Yazid (l.a.) kama khalifa wa Mtume (s), kiongozi na mwakilishi wa Waislam itakuwa na maana ya kuharibu kazi ngumu aliyoifanya Mtume Mtukufu (s) na Maimamu (a) ya kuusimamisha Uislamu. Itakuwa ni kubomoa dini tukufu ya Allah na kuondosha ubinadamu juu ya ardhi. Hivyo ilibidi Imamu kukataa kutoa kiapo cha utii kwa Yazid (l.a.). Uislamu ulikuwa hauwezi kudumu mpaka Imamu Husayn (a) ajitolee muhanga, yeye ambaye ndiye Imamu wa zama hizo, mlinzi wa dini, amani na utu ambaye alikuwa badala ya Mtume na mwakilishi wa Mwenyezi Mungu ulimwenguni.

Mtume Muhammad (a) alikuwa tayari amemfahamisha Imam tukio hili alipokuwa mdogo ambalo litatokea baada ya kifo chake na Imam alijua upinzani mkubwa unaomsubiri siku za baadaye. Imam Husayn (a) alipambanua kwamba njia pekee ya kuamsha Ummah wa Kiislam kutoka katika usingizi ni yeye kujitoa muhanga na kila kilicho kitakatifu, na kuufahamisha Ummah kwamba bora mtu kufa kuliko kupigia magoti batili. Shirk siyo tu kuabudu masanamu, lakini mbaya zaidi kuliko hiyo ni kumkubali kiongozi mpotofu, muovu, taghuti kama kiongozi. Ni kukana uongozi wa Mwenyezi Mungu na kupigia magoti uongozi wa Shetani.

Hali ya kutishia maisha yake ilimlazimisha Sayyidna Husayn (a) kuacha mji wa Babu yake na kuelekea Makkah. Lakini hata Makkah hakuwa na usalama kwa sababu maluuni Yazid alikuwa amewapeleka watu wa kumuua Imam Husayn (a) hata kama atakuwa anatufu Nyumba ya Allah! Hali hii ilimlazimisha Imam kuondoka Makkah bila kuhijji –ilhali hijjah imewadia - na kuelekea mji wa Kufa ambako Waislamu walikuwa wanamuita aje awaongoze na kwamba wako tayari kula kiapo cha utii kwake kama khalifa wa Mtume (s)na Amiri wa waumini.

Tabia za usaliti na uduni na kupenda madaraka na dunia ziliwafanya watu wa Kufa kumsaliti Imam Husayn (a) na kusalimu amri kwa maluuni Ubaydullah bin Ziyad, gavana wa Yazid (l.a.) katika mji wa Kufa. Hali hii ndiyo iliyopelekea Imam Husayn (a) kuuliwa kikatili hapo Karbala, tarehe 10 Muharram, 61 H.