Tatizo la Majadiliano Katika Jamii ya Kiislamu:
Sisi tunaona katika zama hizi kwamba jamii zilizoendelea zimekata masafa ya ukomavu katika muamala wake wa ndani pamoja na matatizo yake ya kifikira, kisiasa na katika maslahi mablimbali, wao wanahitalafiana lakini wanajadiliana na wanazungumza na hatimaye wanafikia kwenye ufumbuzi na wanaishi pamoja na ikhitilafu zao mbalimbali katika nyanja na medani mabalimbali. Ama katika jamii yetu ya Kiislamu, jamii hii ambayo ilikuwa ni wajibu iwe ndio mfano katika uhusiano wake wa ndani kwa mafunzo ya Aya ya Qur'an Tukufu:
"Mmekuwa ni umma bora mliotolewa kwa watu, mnaamrisha mema na kukataza maovu na mnamwamini Mwenyezi Mungu." (Surat Aali Imran: 110).
Tunaikuta hali yetu haiakisi hali hiyo yenye kuangaza ambayo Qur'an inaitaka kwetu, na kwa hiyo unakuta jamii zetu zinaishi katika matatizo mbalimbali katika nyanja hii, na matatizo haya yako aina mbili:
Matatizo yenye kulipuka na mengine ni kama vile moto chini ya majivu unaweza kulipuka wakati wowote, kwa nini?
Kwa sababu sisi hatufuati njia ya mazungumzo, na hii inaweza kuwa ni katika athari za kasumba za kijahilia, kinyume na mwongozo wa Uislamu, ambao miongoni mwa mafunzo yake ni: Usamehevu na kuheshimiana kwa pande zote. Lakini athari za kasumba za kijahilia bado hazijamalizika. Na wakati mwingine inatokea fitina na matatizo na mizozo bila ya kisingizo wala sababu.
Imenukuliwa kuhusu moja ya vita vikubwa katika historia ya Waarabu kwamba mtu alinyoosha mguu wake katikati ya njia na akapiga kelele: “Yeyote ambaye ni mwanaume basi asogeze mguu wangu kutoka kwenye njia hii.” Mmoja wa wapita njia hakuweza kuvumila maneno haya akachukua upanga wake na akakata mguu wake. Na kwa sababu ya tukio hili dogo ikatokea vita ya kipumbavu baina ya makabila mawili kutokana na kitendo cha kipumbavu.
Na katika hali yetu ya kijamii wakati mwingine tunaona baadhi ya matatizo na tunapoingilia ili kuyatatua tunakuta kwamba sababu yake ni ya kipuuzi haistahiki kutokea tatizo kwa sababu yake. Na unakuta hali hii imeenea katika jamii yetu ya Kiislam na ya Kiarabu katika nyanja na viwango tafauti, sawa iwe ni katika ngazi ya familia au katika siasa au katika mambo ya kijamii au katika nembo ya kimadhehebu, na kwa hiyo utaona katika nchi za Waislamu kama vile Afghanistani, Palestina, Lebanoni, Iraki, Somalia na Sudani kuna matatizo mengi na mizozo mingi.
Swali: Kwa nini matatizo haya yamerundikana katika jamii ya Kiislam na ya Kiarabu? Wakati ambapo tunakuta upungufu wa kiwango cha matatizo katika jamii zingine, je wao si wana mgongano katika maslahi vilevile?
Ndiyo, na maslahi huko ni makubwa sana kuliko yalivyo katika jamii zetu za Kiislamu na za Kiarabu. Na tunawakuta wanatofautiana na maslahi yao yanagongana, kinachowatofautisha na sisi ni kumiliki kwao mfumo wa kuamiliana pamoja na matatizo yao. Na sisi kwa masikitiko makubwa hatuna mfumo huu. Na hata nchi yetu haiepukani na aina hii ya matatizo ya kijamii ambayo hayana kisingizio, tarehe 18/12/1412 Hijiria, nilisoma (katika jarida)habari mbili kuhusu mambo mawili tofauti:
Habari ya Kwanza: Inazungumzia kuhusu mzozo uliotokea katika mji mmoja wa Saudia, kuna watu ambao ilitokea baina yao ikhitilafu kuhusu makaburi, habari inasema: Kwamba waombolezaji wawili walizozana wakati wa kusindikiza jeneza, kwa sababu ya mvutano tu baina ya wachache miongoni mwao yalitokea mapigano baina yao na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa kwa majeraha mbalimbali.
Na sababu ya lililotokea inarejea katika mabishano yaliyotokea baina ya watu wawili kati ya waombolezaji, mabishano yaliyotokana na ikhitilafu ya zamani iliyokuwepo baina yao, hivyo ikageuka kuwa mapigano ya mikono; kisha baadhi ya waliokuwepo wakaingilia kati na mzozo ukawa mkubwa hadi zikatumika fimbo na makaburi yakageuka uwanja wa mapigano, mpaka chombo cha usalama kikaingilia kutuliza ghasia, na mapigano yakasababisha kujeruhiwa watu wanne huku mmoja akijeruhiwa vibaya sana.
Pamoja na kujua kwamba mwanadamu anapokuwa makaburini inampasa akumbuke mauti na hisabu na auweke moyo wake katika unyenyekevu, lakini hili halikutokea, na kama alivyosema mshairi wa zamani: "Hakika vita mwanzo wake ni maneno."
Habari ya Pili: Ilichapishwa na jarida siku ileile kuhusu mji wa Habari, inazungumzia ikhitilafu iliyogeuza hafla ya harusi kuwa maombolezo kwa sababu ya ikhitilafu baina yawatu wa bibi harusi na watu wa bwana harusi, na damu zikamwagika na furaha ikageuka huzuni na ikamalizikia katika kituo cha polisi.