Hali Gani hii ya Kutokuendelea?
Hujitokeza hali ya ikhitilafu ya wazi upande wa kimadhehebu, na kati ya matukio ya mwisho ni mkutano wa Doha wa kuleta ukuruba baina ya madhehebu za Kiislamu, pamoja kwamba mkutano ni wa kuleta ukuruba, lakini tumekuta hali ya kutoelewana iliyo wazi katika baadhi ya khutuba ambazo zilitolewa katika mkutano huo. Hakika kuwepomkutano huu ni bora zaidi kuliko kutokuwepo, na uwazi ni njia ya kujuana na kuweka wazi picha ya wote, na hii ni bora kuliko kubakia katika ikhitilafu zilizofichikana ndani ya nafsi na wote kuishi katika hali ya kujizuia na kutokukaribiana.
Na kama nilivyoeleza, hakika watu na makundi katika jamii zilizopevuka wanapokhitalifiana wanakutana na kujadiliana ili wafikie kwenye ufumbuzi, na wanaafikiana juu ya nukta za ushirikiano, wakati ambapo katika jamii ambazo hazimiliki upevu huu hakika ikhitilafu baina ya watu wake inapelekea kutengana na kuwa mbali. Na hapa tunataja tukio lilitokea katika historia ya Waarabu kwa Nabii wetu Muhammad (saww) kabla ya utume, na umri wake mtukufu ulikuwa ni miaka 35, Waarabu walipotaka kujenga upya Kaaba na ikatokea baina ya makabila ikhitilafu kuhusu ni kabila lipi litapata utukufu wa kuweka jiwe jeusi katika sehemu yake. Ikhitilafu hii ilikaribia kuleta vita yenye kuhilikisha kama si mmoja wa wahenga kuwashauri wamfanye hakimu mtu wa kwanza atakayeingia katika msikiti mtukufu, na wakaafikianajuu ya hilo, na wa kawanzakuingia kwao alikuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), walipomuona wakasema: Amekuja mkweli na mwaminifu, tumemkubali kuwa ni hakimu wetu, hapo wakamweleza tatizo. Akasema nileteeni shuka kubwa na jiwe likawekwa humo, kisha akasema: Kila kabila lishike ncha ya shuka, wakanyanyua hadi walipokaribia sehemu ya jiwe, akalichukua Mtume wa Mwenyezi Mungu na akaliweka katika sehemu yake.
Matatizo hayashindikani kutatuliwa akili inapopewa fursa ya kuingilia katika jambo. Na leo umma wetu wa Kiislamu unaishi katika matatizo ya kimadhehebu ya kiubaguzi ambayo yanatakiwa kulipuliwa katika wakati huu mgumu. Na kama suala lingekuwa katika mikono ya wenye akili jambo lingekuwa jepesi sana, isipokuwa uwanja umeachwa kwa wachupa mipaka na wenye kasumba, Zaidi ya haponi uwepo wa matakwa ya kimaslahi, na kisiasa yanayotaka kulipua hali ya umma na kuushughulisha na tatizo hili. Vinginevyo hakika madhehebu sio mapya na ikhitilafu za kimadhehebu ni jambo la kihistoria tangu karne kumi na nne, na nilikuwa nawaambia baadhi ya Maulamaa wa Kisuni: Kila tatizo ambalo mnalo dhidi ya madhehebu ya Shia ni la zamani, na majibu ambayo tunayo ni ya zamani walishayasema Maulamaa wetu, sasa hadi lini tutabaki katika hali hii ya upofu?
Hapa unajitokeza umuhimu wa majadiliano na ukuruba. Kwa nini tuwe mbali? Na kwa nini tutuhumiane?Na kwa nini tuache fursa kwa maadui ili wanufaike kutokana na ikhitialfu hizi kwa hisabu ya maslahi yetu, utukufu wetu na mustakabali wetu?
Hapa Maulamaa katika zama hizi wamezungumza kwa sauti ya akili na mantiki, miongoni mwao ni Sheikh Ali Abu al-Hasan al-Khaniziy (r.a) (aliyezaliwa mwaka 1291 Hijiria na kufariki mwaka 1363 Hijiria) ambaye alitunga kitabu Daawatul-Islamiyah Ilaa Wahdat Ahali Sunnat Wal-Imamiyah ambacho kina ukubwa wa zaidi ya kurasa elfu moja.
Na vilevile Sheikh Muhammad Swalehe bin Sheikh Ali bin Sheikh Suleiman Aali Sheikh Mubaraka (aliyezaliwa mwaka 1318 na kafarika mwaka 1394 Hijiria) ambaye alikuwa Kadhi katika mji wetu kuanzia mwaka 1376 Hijiria hadi kufariki kwake, yaani muda wa miaka kumi na nane. Ana kitabu jina lake ni Daawat Fiy Kalmati Tawhid, humo alifuata njia ya kuleta ukuruba baina ya Waislamu na kuwalingania kwenye kufahamiana wao kwa wao kabla ya yeyote kuelekeza tuhuma ovu kwa ndugu zake, kwa kutilia mkazo umuhimuwa umoja katika kila hali, kila wakati na kila sehemu.
Ni haja ilioje ya sauti ambazo zinazungumza kwa sauti ya akili na mantiki ili tutatue mambo kwa majadiliano na sio kwa mashambulizi na malumbano. Ni wajibu wetu tufahamu mambo vizuri, malumbano haya ya ukinzani yatatufikisha wapi? Sisi ni watu wa nchi moja na sote tuko katika lengo moja, kwanini tunatoa fursa kwa maadui? Na tatizo kubwa ni kwamba athari za uchochezizinadhihiri katika maisha ya wananchi na katika uhusiano wao na wengine pindi wanapokutana katika sehemu mbalimbali kama vile idara za serikali, vyuo vikuu, shuleni na sehemu nyingine za umma, na hii ni hatari kubwa, ni wajibu wetu kuiepusha nchi yetu isije kutumbukia humo.
Dondoo Kutoka Katika Riwaya ya Imam Husein (as) na Sira Yake:
Watu wengi wanamjua Husein (as) kwamba ni mwenye kudhulumiwa na wanajua mateso na machungu ambayo aliyabeba, nayo ni makubwa na ni muhimu. Lakini sisi ni wajibu tujue vilevile kuhusu mafunzo ya Imam Husein (as) na mfumo wake katika upande wa kulingania na majadiliano. Miongoni mwa maneno yake (as) ni kwamba alisema: “Usizungumze yasiyokuhusu, hakika mimi naogopa kwako dhambi, wala usizungumze kuhusu yanayokuhusu hadi uone mahala pa kuyazungumzia, huwenda mzungumzaji amezungumza kwa haki lakini ikawa ni aibu kwake. Wala usijifaharishe kwa mpole wala kwa mpumbavu, hakika mpole atakudharau na mpumbavu atakuudhi."
Na katika ibara zifuatazo kuna baadhi ya dondoo kutoka katika sira ya Imam Husein (as) kuhusu maudhui tunayozungumzia.
Werevu wa Kukosoa:
Unapomuona mwanadamu mwenye kukosea katika rai yake au katika vitendo vyake inapasa kujaribu kumuongoza lakini kwa werevu, baadhi ya watu hawana mbinu nzuri utawaona wanatumia onyo na kemeo haraka, na hili ni kosa.
Hebu tutafakari msimamo huu kutoka katika sira ya Imam Husein: Walipita maimamu wawili Hasan na Husein (as) wakati wangali wadogo, kwa mzee aliyekuwa anatawadha, na hakuwa akitawadha vizuri. Jukumu hapa linahitajia kumwelekeza na kumuongoza, na kwa kuzingatia kuwa ni mtu mzima mkubwa kwa umri na wao ni wadogo walifikiria njia ya werevu kwa namna ambayo hawatausononesha utu wake na hisia zake, kwani lengo ni kuelekeza, alikwenda mmoja wao kwake na kusema:“Ewe mzee kuwa hakimu baina yetu kila mmoja wetu atatawadha.” Wakatawadha kisha wakasema: “Nani kati yetu anatawadha vizuri.” Akasema: “Nyote mnatawadha vizuri isipokuwa huyu mzee mjinga ndio ambaye hakuwa anatawadha vizuri, na sasa amejifunza kutoka kwenu na ametubia mbele yenu kwa baraka zenu na huruma yenu kwa umma wa babu yenu."
Kuepukana na Mijadala Isiyo na Tija:
Imepokewa kwamba mtu alimwambia Imam Husein (as): “Kaa ili tujadiliane katika dini.” Akasema: “Ewe mtu, mimi najua dini yangu na najua uongofu wangu, kama wewe hujui dini yako basi nenda ukaitafute, ni wapi mimi na majadiliano!! Hakika shetani anamshawishi mtu na anamnong'oneza na kumwambia: Jadiliana na watu katika dini ili watu wasihisi mapungufu yako na ujahili wako."
Na hili ni somo kubwa, na ni wajibu tulitafakari, hakika mwanadamu inapasa asivutike kwenye mjadala usio na tija. Na napenda kutoa angalizo kwamba maneno haya ya kiubaguzi ya kimadhehebu ambayo yamejaa anga yanataka kushughulisha watu na mijadala tasa.Nasaha yangu kwa nafsi yangu na kwa ndugu zangu wananchi wote ni kwamba wajiepushe kuingia katika mjadala huu. Wakati mwingine unaona katika madrasa au chuo kikuu au katika sehemu yoyote mjadala unaotokana na yale wanayoyasikia katika runinga, na baadhi wanadhani kwamba ni wajibu wake kujitetea, na kama hajajadili atakuwadhaifu, na kutokana na mantiki hii baadhi wanatumbukia na kuvutika katika mjadala huu tasa, ambao haujulikani utaishia wapi. Asidhani yeyote kwamba kwa kujibu kwake anatumikia madhehebu na itikadi, dhana hii ni makosa.
Na mara nyingi lengo la upande mwingine la mjadala ni uchochezi na kutengeneza tatizo, tumeshuhudia na tumesikia mengi katika nyanja hii, na kwa sababu hii Qur'an inawasifu waumini kwa kauli yake (swt):
“Na wale ambao hawawi kwenye uzushi, na wanapopita kwenye upuzi hupita kwa heshima zao.” (Surat Furqan: 72).
Na kauli yake (swt):
"Na waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea ardhini kwa unyenyekevu. Na wajinga wakiwasemesha, husema: 'Salama.'" (Surat Furqan: 63).
Kama tungesoma vitabu vya Hadithi kama vile al-Kafiy na Biharul-An’war tungekuta riwaya nyingi kutoka kwa Maimamu wetu (as) kuhusu majadiliano, mazungumzo na kujionyesha katika dini, nazo ni hadithi zinazokataza hali hiyo, Imam as-Sadiq(as) anasema: "Jihadharini na ugomvi katika dinihakika unazizuia nyoyo kujishughulisha na utajo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu." Na nasema: “Msigombane na watu kwa ajili ya dini yenu hakika ugomvi unaleta ugonjwa katika nyoyo, waacheni watu hakika watu wamechukua kutoka kwa watu."
Na ni wazi kwamba wewe huwezi kubadilisha ukinaikaji wa wengine; kwa sababu wao wamechukua maarifa yao kutoka kwa masheikhe wao wanaowazingatikia kuwa ni watukufu na wanawaheshimu. Na kuna riwaya kutoka kwa Imamu al-Baqir (as) ambayo inatia mkazo juu ya dharura ya kuwa mbali na mjadala na majadiliano tasa, inawaeleza Mashia kwa sifa ya ajabu, Imam anasema: "Hakika Mashia wetu hawazungumzi." Ikimaanisha kujiepusha kwao na hali hii isiyo na faida.
Hadi mmoja wa wanafunzi wa Imam as-Sadiq (as) alimwambia Imam:“Imenifikia kwamba wewe umechukia kujadiliana na watu.” Akasema: "Ama maneno ya aliye mfano wako hayachukiwi, ambaye akiruka anajua kutua vizuri bila kuanguka, na akitua anajua kuruka vizuri, ambaye yuko hivi hatumchukii." Na amesema Abdul-Ulaa: Nilimwambia Abu Ja'far: “Hakika watu wanamtia dosari Ali kwa maneno, na mimi najadiliana nao.” Akasema: Ama mfano wako, ambaye anatua kisha anaruka, huyu ni bora, ama anayetua lakini hawezi kuruka, huyu hapana."
Hapa tunatia mkazo kwamba mtu yeyote ambaye ana uwezo wa kutatua mambo kwa njia sahihi inasihi kwake kujadili, ama ikiwa hawezi hayo kama ikiwa maarifa yake ni madogo au hawezi kudhibiti hasira zakebasi mjadala sio katika maslahi yake na madhehebu hayanusiriwi kwa mjadala bali yananusurika kwa amali njema.
Kuamsha Utu, Dhamira na Maadili Yenye Uongofu:
Njiani Imam Husein alipokuwa anakwenda Iraki alipitia katika sehemu inayoitwa Zarud, na huko alikuta hema la Zuhair bin al-Yaqiin, na alikuwa ni katika watu wa Uthman yaani kati ya wanaounga mkono kutaka kulipiza kisasi kwa damu ya Uthman, hivyo msimamo wake ulikuwa umeathirika kwa msimamo wa Ban Ummayya, riwaya zinaashiria kwamba Zuhair alikuwa ameazimia kumkwepa Imam Husein (as) njiani ili asipate taabu ya kukutana naye, hivyohaikutokea kusimama msafara wa Imam Husein na msafara wa Zuhair bin al-Yaqin katika sehemu moja muda wote katika njia ya Husein (as) hadi Iraki, isipokuwa katika sehemu hii (Zarud) ambapo Zuhair hakuwa na hiyari nyingine.
Imam (as) akatuma mjumbe kwake akimwita aende kwake, mpokezi amesema: Sisi tulipokuwa tumekaa tunakula, ndipo alipoingia mjumbe wa Husein akasalimia, na akasema: “Ewe Zuhair bin al-Yaqin hakika Abu Abdillahi Husein bin Ali amenituma kwako nikwambie uende kwake.” Mpokezi anasema: “Kila mtu alitupa kilichokuwa mkononi mwake kana kwamba imetuteremkia balaa.” Mke wake akamwambia: “Je, Mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu anatuma kwako mjumbe kisha huendi? Subhanallah, lau ungemwendea usikie maneno yake!!” Zuhair bin al-Yaqiin akamwendea, haukupita muda akaja hali ni mwenye furaha na uso wake umebadilika na kuwa wa njano, akaamuru apewe tandiko lake na vitu vyake akavibeba kuelekea kwa Husein, kisha akamwambia mke wake: “Wewe umeachwa! Nenda kwa Ahali yako, hakika mimi sipendi upate kwa sababu yangu isipokuwa kheri.” Kisha akawaambia wafuasi wake: Anayependa miongoni mwenu anifuate, hakika haya ni maagano ya mwisho.
Na katika riwaya nyingine: “Anayependa kufa shahidi miongoni mwenu basi asimame na anayechukia basi aondoke. Hakika mimi nitawasimulia hadithi; Tulipigana vita (Balanjar) na Mwenyezi Mungu akafungua kwetu na tukapata ngawira, Salman al- Farisiy akasema: “Mmefurahi kwa aliyofungua Mwenyezi Mungu kwenu na mliyoyapata miongoni mwa ngawira?” Tukasema: Ndio, akatuambia: Mtakapo mkuta kijana wa Aali Muhammad – na katika riwaya nyingine: Bwana wa vijana wa Aali Muhammad – basi kuweni ni wenye furaha zaidi kwa kupigana kwenu pamoja nao kushinda ile ya yale mliyoyapata miongoni mwa ngawira. Ama mimi nawaaga.” Mke wake akamwambia: Mwenyezi Mungu amekuchagulia, nakuomba unikumbuke siku ya kiyama mbele ya babu wa Husein (as).”
Na katika riwaya nyingine ni ule msimamo aliouonesha Husein (as) kwa adui mkubwa, ambaye aliongoza jeshi dhidi ya Husein, naye ni Umar bin Sa'd, pamoja na uadui huo utamkuta Imam Husein (as) katika siku ya tisa ya Muharram anataka kukutana naIbn Sa'd, lakini Ibn Sa’d anakataa, mwishoni anaafiki, riwaya inasema:
Husein alimwambia: “Ole wako, ewe Ibn Sa'd! Je humuogopi Mwenyezi Mungu, nakuona unanipiga vita na unataka kuniuwa, na mimi ni mtoto wa ambaye umeshamjua, waache hawa watu, waache wao na kuwa pamoja na mimi, hakika hilo liko karibu zaidi na wewe na ni lenye kukurubisha kwa Mwenyezi Mungu.” Akamwambia: “Ewe Husein, hakika mimi naogopa kuvunjiwa nyumba yangu huko Kufah na kuporwa mali zangu.” Husein alimwambia: “Mimi nitakujengea nyumba bora kuliko nyumba yako.” Akasema: “Naogopa kuchukuliwa mifugo yangu huko Sawadi.” Husein akamwambia: “Mimi nitakupa miongoni mwa mali zangu Baghibaghah, nayo ni chemchem kubwa iliyopo katika ardhi ya Hijazi, Muawiya alitaka kunipa thamani yake dinari milioni moja za dhahabu na sikumuuzia.” Umar bin Sa'd hakukubali chochote kati ya hayo.
Husein aliondoka kwake akiwa amekasirika na akisema: “Mwenyezi Mungu akuchinje haraka ewe Ibn Sa'd juu ya kitanda chako, na wala asikusamehe siku ya kufufuliwa kwako, wallahi hakika mimi nataraji hutakula katika ngano ya Iraki isipokuwa kidogo sana.” Umar bin Sa'd akamwambia kwa istihizai: “Ewe Husein, hakika kuna shairi badala ya ngano.”
Huu ndio mfumo wa Husein na sira yake, inafaa kwa umma uchukue katika mfumo huu wa kiutume ambao unaangazia njia ya maendeleo na mafanikio.