Walimwengu wamfanye Imam Hussein AS kuwa kigezo chao katika kupambana na ubeberu
Ayatullah Muhammad Ali Movahedi-Kermani amesema hayo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran ambapo mbali na kutoa mkono wa pole na tanzia kwa mnasaba wa kuwadia kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS amesema kuwa, ana matumaini Waislamu na watu wenye fikra huru duniani watamfanya Imam Hussein kuwa ruwaza njema na kigezo chao cha kufuata kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu na kuwafikisha katika saada na ufanisi.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran amesikitishwa na hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kufuata siasa za kuzusha machafuko za maadui wa Uislamu ikiwemo Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mashariki ya Kati na kusema kwamba, umewadia wakati sasa kwa nchi za Kiislamu kuzinduka na kuwa macho na kwa msingi huo kukwamisha mipango michafu ya maadui.
Aidha katika sehemu nyingine ya hotuba yake katika Sala ya Ijumaa hii leo hapa mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Ali Movahedi-Kermani amekumbushia hatua ya utawala wa kifalme wa Saudi Arabia ya kuwazuia Wairani kwenda kutekeleza faradhi ya ibada ya Hija mwaka huu na kusema kuwa, maafa ya mwaka jana ya Mina katu hayawezi kusahauliwa, kwani yalizijeruhi hisia za Waislamu wote ulimwenguni.