Change Language: English

Waislamu wapya na wasiokuwa Waislamu katika matembezi ya Arubaini (3)

Matembezi ya Siku ya Arbaini ambayo hufanyika kwa nia ya kumzuru Imam Hussein (as) na ambayo hutimia katika siku ya arubaini tokea auawe shahidi mtukufu huyo, ndiyo matembezi makubwa zaidi ya binadamu duniani, jambo ambalo wanalikiri marafiki na maadui wote ulimwenguni.

Iraq ni nchi isiyokuwa na suhula nyingi za starerehe wala usalama wa kutosha lakini pamoja na hayo mamilioni ya watu walio na hamu kubwa ya kumzuru Imam Hussein (as) humiminika nchini humo kwa ajili ya kuzuru kaburi la mtukufu huyo katika mji mtakatifu wa Karbalaa bila ya kulazimishwa wala kushawishiwa na matangazo ya vyombo vya habari vya kimataifa. Ni karibu karne 14 sasa tokea sahaba wa Mtume Jabir bn Abdillah al-Ansari, mfanya ziara wa kwanza wa Arubaini ya Imam Hussein (as), alipotembea kwa miguu kutoka mjini Madina kwenda kumzuru Imam Hussein, siku Arubaini tokea auawe shahidi kidhulma katika jangwa la Karbala. Tokea wakati huo hadi leo na licha ya kuwa ziara ya Imam Hussein (as) imekuwa ikitekelezwa katika mazingira magumu yanayohatarisha maisha ya wafanyaziara katika vipindi tofauti vya historia lakini pamoja na hayo wafanya ziara hufumbia macho hatari hiyo na hata wengine kufanya zira hiyo kwa siri kwa ajili ya kwenda kutoa heshima zao na kumzuru mtukufu huyo (as). Hivi sasa baada ya kung'olewa madarakani utawala dhalimu wa dikteta Saddam Hussein na licha ya kuwepo vizuizi na hatari ya mashambulio ya magaidi lakini matembezi ya Arubaini yanafanyika kwa wingi na mafanikio makubwa kuliko wakati mwingine wowote, ambapo mamilioni ya watu hutokea katika kila pembe kwa ajili ya kwenda kumzuru mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as).

Mahudhurio ya mamilioni ya wafanyaziara katika Arubaini ya Imam Hussein (as) Karbala

Tunapokuwa miongoni mwa watembezi wa siku ya Arubaini katika barabara na njia zinazoelekea Karbala, tunawaona waumini na Mashia walio na hamu kubwa ya kwenda kumzuru Imam Hussein. Miongoni mwao kuna Waislamu wapya waliosilimu hivi karibuni kutoka katika nchi zilizozama kwenye utajiri na starehe lakini pamoja na hayo hawako tayari kubadilisha barabara zilizojaa vumbi zinazoelekea kwenye kaburi la Imam Hussein (as) na majumba marefu ya kifahari yanayopatikana kwenye nchi hizo. Katika matembezi haya ya kuvutia kuna mwanamke mmoja aliyesilimu hivi karibuni raia wa Uholanzi ambaye amejiunga na safina ya uongofu ya Imam Hussein (as), mwanamke ambaye alisilimu na kufikia ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu miaka michache iliyopita baada ya kufanya utafiti wa kina wa Qur'ani Tukufu. Huku akisema kuwa ziara ya Karbala yalikuwa matumaini yake makubwa na ya muda mrefu, bibi huyo wa Kiholanzi anasema: 'Mara hii Imam Hussein (as) ndiye aliyenichagua na safari hii ni wito kutoka kwake.'

Mwislamu mpya wa kike kutoka Uholanzi ambaye ameshiriki matembezi ya Arubaini

Mwanamke huyu yuko kwenye matembezi haya akiandamana na mumewe pamoja na mtoto wao mdogo. Mchanga na vumbi ulioko kwenye njia ya kuelekea Karbala unaonekana kote kwenye uso wa mtoto huyo lakini pamoja na hayo anatembea harakaharaka ili kumsaidia mama yake aweze kufikia ndoto na matarajio yake hayo makubwa. Mwislamu huyu mpya anasema: 'Huwezi kuyaona haya mambo nchini Uholanzi. Huko serikali ina pesa nyingi ambazo huzigawa na kuwasaidia raia wake.... lakini mimi ninapendelea zaidi maisha ya hapa. Sijali kuwa hapa kuna suhula chache mno za burudani (maisha bora). Hakika maisha (na mahusiano ya kibinadamu) nchini Uholanzi ni baridi sana na mimi nina hamu ya kuwa na maisha yaliyo na uchangamfu na ya kirafiki yaliyoko hapa.'

Katika kona nyingine ya mkusanyiko mkubwa wa Arubaini kuna kijana kutoka Ukraine kwa jina la Roman ambaye kwa hakika si Mwislamu lakini amefika hapa akiandamana na marafiki zake wa Kiislamu kwa ajili ya kushuhudia kwa karibu mandhari hii adhimu. Alifika hapa kwa ajili ya kutazama tu mkusanyiko huu mkubwa wa jamii ya wanadamu lakini hivi sasa amevutwa na mvuto mkubwa wa simaku ya Imam Hussein (as). Amepigwa butaa na kushangazwa na mjumuiko huu mkubwa wa mamilioni ya wafuasi wa Imam Hussein (as) ambao wamedhihirisha picha na taswira ya kuvutia ya umaanawi na maadili ya kiutu na kumfanya ajiulize swali hili muhimu kwamba je, ni nani huyu Hussein ambaye hata baada ya kupita karne 14 lakini bado ana uwezo wa kuvutia idadi hii kubwa ya watu? Kila anapozidi kupiga hatua kuelekea Karbala ndivyo anavyozidi kudiriki taratibu ukweli wa mambo na hatimaye kuketi chini na kusema: 'Mimi nitasilimu.!' Anaendelea kusema: 'Jambo lililonishangaza zaidi ni huruma na ukarimu walionao Waislamu wa Iraq na safari yangu ya kuelekea Karbala kwa hakika imebadilisha kabisa mtazamo wangu kuhusiana na Mashia. Kwa hakika Waislamu hawa ni tofauti kabisa na vile wanavyoakisiwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Hawa ni watu wenye huruma na wakarimu na walio mbali kabisa na vita na uadui.' Roman anaendelea kusema: 'Katika safari hii, nimepata yakini kwamba Uislamu halisi ulioletwa na Muhammad ni dini ya msamaha na kujitolea na nimeamua kukubali na kutangaza kusilimu kwangu katika Haram Tukufu ya Imam Hussein (as).'

Roman, kijana wa Ukraine aliyesilimu katika matembezi ya Arubaini

Igor Saladaniyuck ni Mwislamu mwingine mpya kutoka nchini Ukraine ambaye anashiriki katika matembezi haya ya Arubaini kwa mara ya kwanza. Anasema: 'Tulipokuja Najaf na kuingia kwenye Haram ya Imam Ali (as), tulishangazwa sana na mazingira ya utulivu na amani ya eneo hili na kuguswa na ukarimu pamoja na mapokezi mazuri ya watu wa huku pamoja na ya wasimamizi wa Haram Tukufu. Ni kinyume kabisa na vile tulivyokuwa tukiambiwa kuhusiana na hali ya Iraq.' Mfanyaziara huyu Mwislamu wa Ukraine anaendelea kusema: 'Tutawaambia jamaa na watu wa nchi yetu yale yote tuliyoyashuhudia huku na kuwafahamisha kwamba maana halisi ya Uislamu inapatikana katika mafundisho na maarifa ya Ahlul Beit (as) na katika Haram Takatifu.'

Hatupasi kuwatazama Roman na Igor kama watu binafsi bali ni wawakilishi wa harakati na wimbi kubwa la Waislamu wapya ulimwenguni ambao wana mapenzi makubwa kwa Imam Hussein (as). Matembezi ya Arubaini ni harakati kubwa ambayo inaweza kuvunja njama na propaganda za uongo za mataifa ya kibeberu duniani na kuangaza nuru ya hakika kwenye nyoyo zilizo na hamu ya kujua ukweli katika kila pembe ya dunia.

Igor Saladaniyuck akiwa katika Haram ya Imam Ali (as) mjini Najaf, Iraq

Bibi Clodia Burja ni mpiga picha raia wa Italia ambaye miaka kadhaa iliyopita aliandaa maonyesho ya picha za Ashura mjini Rome. Bi Burja ambaye ni Mkristo alifika nchini Iran na kupiga picha za kuvutia marasimu ya maombolezo ya Imam Hussein (as) yanayofanywa hapa nchini na Wairani walio na hamasa na mapenzi makubwa kwa Imam Hussein (as), ili kwa njia hiyo aweze kuwafikishia wananchi wa Italia ujumbe halisi wa tukio la Ashura. Anasema Imam Hussein (as) alimuathiri pakubwa kadiri kwamba naye pia aliamua kuomboleza na kumlilia Imam Hussein kama walivyokuwa wakifanya Wairani. Mwaka uliopita, alishiriki kwenye matembezi ya Arubaini na anaamini kwamba Imam Hussein (as) ndiye aliyemwita. Clodia ambaye ni Mkatoliki anaamini kwamba kushiriki kwenye mjumuiko mkubwa wa mamilioni ya waombolezaji ni fahari kubwa kwake na kwamba hivi sasa anatambua kwamba Imam Hussein sio mtu mmoja tu bali ni njia na mtindo wa maisha, ambayo ni maisha ya hakika. Anasema: 'Mimi ninayapenda maisha haya na ninataka kuyafuatilia maisha haya, yaani nifanye kazi bora zaidi kwa ajili ya kufikia haki na uadilifu.' Anaamini kwamba matembezi haya huweza kumsaidia mwanadamu kutambua mambo mapya kuhusiana na nafsi yake na Imam Hussein (as). Mpiga picha huyu Mtaliano na ambaye amevalia hijabu kamili ya Kiislamu na aliyefunga kichwani pake kitambaa kilicho na maandishi yanayosomeka, 'yaa Hussein madhlum!, na ambaye ameandamana na wapenzi wengine wa Imam Husein anasema: 'Hapa kuna kitu kizuri na bora zaidi ambacho nimewahi kukipata maishani mwangu.' Clodia pia si mtu mmoja bali ni mwakilishi wa mjumuiko mkubwa wa watu ambao licha ya kuwa hawajasilimu bado lakini wameathirika pakubwa na mvuto na adhama ya Imam Hussein na hivyo kulazimika kupiga magoti mbele ya malengo yake matukufu.

Katika kipindi hiki tumezungumzia Waislamu wapya ambao wamesikiliza kwa makini ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein (as) na kuamua kumfuata. Katika njia hii kuna kundi kubwa la Mashia wasiojulikana, ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha suala hilo ambao ndio watakaotukamilishai kipindi hiki. Mashia wa Nigeria, nchi ambayo miaka 40 iliyopita haikuwa ila na idadi ndogo tu ya Mashia, hivi sasa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, imefanikiwa kuwaingiza zaidi ya wafuasi wa madhehebu ya Suni na Wakristo milioni 10 katika madhehebu ya Ahlul Beit wa Mtume (saw). Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye kwa miezi kadhaa sasa anashikiliwa katika mojawapo ya jela za Nigeria ndiye kiongozi wa Mashia hao wenye ikhlasi. Bila shaka mwamko wa Mashia hao unatokana na juhudi kubwa na za kuvutia za Sheikh Zakzaky. Sehemu kubwa ya Mashia hao wa Nigeria hawana uwezo wa kushiriki katika matembezi ya Arubaini ya Karbala kutokana na umbali wa masafa na matatizo ya kifedha. Kwa msingi huo katika kukaribia siku ya Rubaini ya Imam Hussein (as), Mashia hao wanatembea kwa miguu kutoka katika miji yao ya mbali kuelekea mji wa Zaria ambayo ndiyo makao makuu ya shughuli za kidini za Sheikh Zakzaky, ili waweze kushiriki kwenye maombolezo ya Arubaini yanayofanyika katika Husseiniya ya mji huo. Karibu watu milioni 8 hushiriki kwenye matembezi hayo ambayo kwa kawaida huwa yanafanyika hata bila ya kuakisiwa na vyombo vya habari vya kimataifa. Matembezi hayo makubwa ya maombolezo huwa yanaandaliwa na kuendeshwa na Mashia hao wenye ikhlasi kwa kutegemea suhula chache mno walizonazo. Licha ya ukandamizaji unaofanywa na jeshi la Nigeria na vilevile hatari ya makundi ya kigaidi lakini kila mwaka matembezi hayo ya maombolezo hufanyika kwa mafanikio makubwa zaidi na watu wengi zaidi kujiunga nayo kutokana na mapenzi makubwa waliyonayo kwa Imam Hussein (as).