Change Language: English

Taamuli katika Ziara ya Arubaini ya Imam Hussein AS (6)

Assalam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki maalumu cha Majlisi za siku ya Arubaini ambacho hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walitoa mhanga roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.

Katika mfululizo wa makala zetu hizi leo tutaangazia Ziara ambayo husomwa katika siku hii ya Arubaini ya Imam Hussein AS

@@@

Tarehe 20 Safar inasadifiana na Arubaini ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake 72 katika jangwa la Karbala, Iraq ya leo. Hii huwa ni siku maalumu ya kusoma Ziara ya Imam Hussein AS. Hii ni ziara ambayo husomwa kumuadhimisha Hussein bin Ali AS. Huyu ni Hussein ambaye Imam Sadiq AS alisema kuwa, kwa kuuawa kwake shahidi, Waislamu waliweza kunusurika na ujahili ambao ulikuwepo kutokana na propaganda chafu za Bani Umayya ambaye alikuwa amewaweka mbali na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Sunnah ya Mtume Muhammad SAW.

Harakati ya kishujaa ya Imam Hussein AS ilifichua itikadi potovu za watawala wa Bani Umayya ambao walikuwa wakijiarifisha kama Warithi wa Mtume SAW. Kwa harakati yake, Imam Hussein AS aliweza kuarifisha Uislamu sahihi na kupelekea kusambaratika itikadi potovu za Yazid na wenzake.

Imam Hassan Askari AS anasema: "Ishara za Muumini ni tano, kusali rakaa 51, (17 za wajibu na 34 nawafil), kusoma ziara ya Siku ya Arbaeen, pete katika mkono wa kulia, kuweka kichwa katika udongo wakati wa kusujudu na kutamka kwa sauti Bismillahi Rahmani Rahim katika Sala."

Katika kuadhimisha Siku ya Arubaini kuna ziara kadhaa ambazo ni mashuhuri. Moja ya ziara hizo ni ile iliyo mashuhuri kama 'Ziara ya Arubaini' ambayo ni matini inayonasibishwa na Imam Sadiq AS. Hii ni matini iliyojaa maana na maarifa ya juu ya Kiislamu.

Katika maandishi ya Ziara hiyo tunapata mafunzo kuhusu irfani, ibada, kujitolea, kuuawa shahidi, ridhaa, jitihada na jihadi. Matini ya Ziara ya 'Arubaini' ni johari ya thamani za juu ambapo mwenye kuisoma hutangaza mfungamano na mashahidi wa Karbala ili katika hali yoyote ile awe mwendelezaji wa njia ya Imam Hussein AS.

Ziara ya Arubaini sawa na ziara nyiginezo katika Uislamu huanza na salamu, unyenyekevu na kumtakia mema Imam Hussein AS kwa kusoma ifuatavyo: "اَلسَّلامُ عَلى وَلِىِّ اللَّهِ وَ حَبیبِهِ، اَلسَّلامُ عَلى خَلیلِ اللَّهِ وَ نَجیبِهِ ، اَلسَّلامُ عَلى صَفِىِّ اللَّهِ وَ ابْنِ صَفِیهِ"....Katika salamu hiyo, mwenye kusoma Ziara hutaja sifa za mitume yaani Mtume Muhammad Al Mustafa SAW kama Habibullah na Ibrahim AS kama Khalilullah na Nabii Adam kama Safiullah na kuwanasibisha na Imam Hussein AS.

Kwa hivyo kwa kutumia maneneo hayo yaliyoandikwa na Imam Sadiq AS, mwenye kusoma Ziara hubainisha kuwa Imam Hussein AS ametokana na MItume. Katika sehemu nyingine ya Ziara hii tunasoma hivi: "Salamu kwa wale ambao wametii turathi za Mitume" ( السَّلَامُ عَلَی... اَعْطَیْتَهُ مَوَارِیثَ الْاَنْبِیَاءِ). Kwa msingi huo kuadhimisha Arubaini ni sawa na kuadhimisha na kuidhinisha harakati na mwamko wa Mitume wote kuanzia Adam hadi Mtume wa Mwisho, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu Yao.

Kila ambaye anasikia jina la Hussein AS na tukio la Karbala, huanza kutokwa na machozi. Haya ni machozi yanayotafautiana sana na yale ya mtu ambaye amekumbwa na msiba wa jamaa au rafiki.

Machozi ambayo yanatokana na msiba wa Imam Hussein AS, iwapo yatatokana na maarifa na uono wa mbali basi yanaweza kumuinua mwanadamu kutoka dunia hii na kumpaza kuelekea katika ulimwengu wa malakuti. Kama ambavyo tunasema katika aya ya 83 ya Surat Al Maida: Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa Mtume utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyoitambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia.

Ni kwa msingi huo ndio mwenye kusoma Ziara ya Arubaini sambamba na kutuma salamu zake kwa Imam Hussein AS anasema: " اَلسَّلامُ عَلىَ الْحُسَینِ الْمَظْلُومِ الشَّهیدِ ، اَلسَّلامُ على اَسیرِ الْکرُباتِ ، وَ قَتیلِ الْعَبَراتِ

"Salamu zimefikie Hussein Madhlumu na Shahidi, Salamu kwa aliyekuwa mateka wa masaibu na mhanga wa machozi"

Sehemu nyingine ya Ziara ya Siku ya Arbaeen inahusu saada na utakasifu wa Imam Hussein AS pale tunaposoma: "Ewe Mola, Nashuhudia kuwa, Hussein AS ni walii wako ni mwana wa Walii wako. Yeye ni mteule wako na ni mwana wa mteule wako, chaguo lako na mwana wa chaguo lako. Ewe Mola! Nashuhudia kuwa umemtukuza kupitia kufa kwake shahidi na umempata saada na ametokana na nasaba iliyotakasika na uzawa uliotakasika, na ukamfanya awe mkuu na mmoja wa viongozi, mmoja wa watetezezi wa dini yako na mritihi wa mitume wote na umemfanya awe hujja kwa viumbe wako na mmoja wa waritihi wa Mitume"

Hussein AS alilelewa na Mtume SAW ambaye Mwenyezi Mungu SWT amemtaja kuwa 'Rehema kwa Walimwengu na hilo lipo katika Aya ya 107 ya Suratul Anbiya katika Qur'ani Tukufu ifuatavyo: "Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote. "

Ni kwa sababu hii ndio Imam Hussein AS akaonyesha ukarimu kwa wanajeshi wa Yazid na akawa ni mwenye kuwapa mawaidha pamoja na kuwa walikuwa wamefika hapo kumuua. Hata katika lahadha alimokuwa ameanguka chini alikuwa akijitahidi kuwaongoza. Hatimaye alitoa damu yake kwa ajili ya kuwaokoa watu kutoka katika ujahili na upotofu. Kwa msingi huo katika sehemu nyingine ya Ziara ya Arubaini tunasoma: "Ewe, Mola! Hussein alitimiza Hujja katika kuwaongoza watu na hakuacha kisingizio kwa yeyote. Alijitahidi kikamilifu katika utendaji mema na kujitoa muhanga katika njia yako.!

Imam Hussein AS kabla hajaondoka Makka alimuandikia wasia ndugu yake, Muhammad ibn al-Hanafiyyah ambapo alimfahamisha kuhusu malengo ya mwamko na harakati yake na kusema: "Mwamko wangu ni kwa ajili ya kuleta marekebisho katika dini ya Babu Yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, pamoja na kuamrisha mema na kukataza maovu." Kauli hiyo ilitokana na kuwa, katika zama za Imam Hussein AS kulijiri mabadiliko makubwa katika dini pamoja na bidaa nyingi kutoka kwa watawala waovu wa zama hizo.

Ili kuilinda hakika katika dini ya Babu yake, na kuikabidhi kwa vizazi vijavyo ikiwa salama, Imam Hussane AS hakuwa na njia nyingine ila kuanzisha harakati na kwa njia hiyo kuwatangazia wote kuwa kile kilichokuwa kikihubiriwa na watawala wa wakati huo haukuwa Uislamu sahihi bali kilikuwa tafauti na mafundisho ya Mtume Muhammad SAW. Kwa msingi huo, mwenye kusoma Ziara ya Siku ya Arubaini anaashiria malengo ya mwamko wa Imam Hussein AS ifuatavyo: "Ewe Mola! Hussein AS alianzisha harakati na kuitoa muhanga roho yake kwa ajili yako na kuacha yote katika maisha yake ili kuwaokoa waja wako ambao walikuwa wametumbukia katika ujahili."

@@@@

Kundi moja la watu ambao walikuwa wanapambana dhidi ya Imam Hussein AS na ambao pia walimuua shahidi walikuwa watu waliohadaiwa na dunia. Tumbo zao zilikuwa zimejaa mali haramu. Waliuza Akhera yao kwa thamani ndogo. Kwa msingi huo katika Ziara ya Arubaini tunaendelea kusoma hivi: "Wale ambao walikuwa na hamaki na wakaangamia kwa ajili ya kufuata matamanio ya nafsi zao. Wakajiletea adhabu yako na ya Mtume Wako, waliwatii waasi na wanafiki na wakawa ni wenye kubeba madhambi ya wanaostahiki kuchomwa moto."

Imam Hussein AS alikuwa na subira wakati wa jihadi katika njia ya kutii amri ya Mwenyezi Mungu, damu yake ikamwagwa na akavunjiwa heshima.

Katika mapambano ya Karbala, watu wa nyumba ya Imam Hussein AS pamoja na masahaba zake walibainisha utiifu wao kwake kwa njia ya kipekee kwake hasa katika siku ya Ashura. Zaidi ya utiifu huo, ni utiifu wa Imam Hussein AS kuhusu kufungamana na ahadi yake kwa Mwenyezi Mungu. Hapa kwa mara nyingine mwenye kusoma Ziara anamtumia Salamu Imam na kusema: "Ewe Hussein AS! Nashuhudia kuwa, wewe umelinda amana ya Mwenyezi Mungu na wewe ni mwana wa Mlinda amana ya Mwenyezi Mungu, umeishi kwa saada hadi wakati wa kufa shahidi. Mwenyezi Mungu amuangimize kila aliyekukosoa na amuadhibu kila aliyekuua. Nashuhudia kuwa Wewe Ulikuwa mtiifu kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na ulipigana Jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu hadi wakati wa kifo na shahada yako"

Kile kilicho wazi ni kuwa, rafiki wa kweli na hakika ni yule ambaye anawaonyesha marafiki wako mahaba. Aidha maadui na wanaomtakia mabaya rafiki yako wewe pia utawachukia na kwa msingi huo katika sehemu ya Ziara ya Arubaini tunasoma hivi kuhusu marafiki na maadui wa Imam Husseina AS: "Ewe Mola! Naapa kuwa kila ambaye anampenda Hussein AS mimi pia nampenda na kila ambaye ana uadui naye mimi pia ni adui yake."

Mwenye kusoma Ziara ya Siku ya Arubaini, baada ya kuwa amebaini baadhi ya fadhila na maadili mema ya Imam Hussein AS, anabainisha pia itikadi za moyo wake na kusema: "Kila ninchokifanya kinategemea muongozo wako, matakwa ya moyo wangu yamesalimu amri mbele ya matakwa ya moyo wako na ninakufuata katika masuala yangu yote na niko tayari kuwa msaidizi wako na maadamu Allah ameidhinisha basi mimi niko nawe na wala siko na maadui wako."

Baada ya msoma Ziara kubainisha baiya na utiifu wake kwa Imam, anaendeleza Ziara kwa kutoa sala na salamu kwa Ahul Bayt watoharibu kwa kusema: "Sala na Salamu za Mwenyezi Mungi ziwe juu yenu enyi roho takatifu na viwiliwili vyenu vilivyotakasika". Kwa msingi huo mwenye kusoma Ziara anaonyesha mahaba , mapenzi na imani yake kwa Imam Hussein AS.

Jabir ibn 'Abdullah al-Ansari katika maandishi yake mwishoni mwa Ziara ya Siku ya Arubain anasema: "Naapa kwa Mungu ambaye alimteua na kumtuma kwa haki Muhammad SAW kuwa, sisi ni washirika wenu enyi Mashahidi katika kile kilichowasibu." Hapo akaulizwa "Ni vipi sisi ni washirika wao katika hali ambayo hatukuwa pamoja nao katika Njia ya Mwenyeji Mungu na wala hatukunyosha upanga?" Akasema "Mimi nilimsikia Mtume SAW akisema: "Kila ambaye atalipenda kundi fulani, basi atafufuliwa nalo, na kila ambaye atapenda kazi ya kundi fulani basi atakuwa mshirika wa vitendo vyake."

Mwishoni mwa makala hii tunawakaribisha kusikiliza Ziara ya Arubaini ya Imam Hussein AS. Tukumbukane katika Dua