Change Language: English

Ni nini kinacholeta uhai kwa jamii zilizokufa?

Sasa hebu tuangalie kile kilichotokea Karbala na katika siku ya Ashura. Lakini kwanza weka kando mitazamo na uelewaji wako wa Karbala katika pembe moja ya akili yako. Sisemi uitupilie mbali, weka tu kando picha ambayo umekwishaichora juu ya Karbala, kwa sababu kama utaendelea kuwa pamoja na picha hiyo katika kichwa chako kile ambacho nataka kukisema sasa hivi hakitaingia akilini mwako kwa urahisi.

Ni Karbala na Ashura ileile ambayo sisi tumetakiwa kuikumbuka na kuomboleza kwa kaulimbiu: “Kila ardhi ni Karbala na kila siku ni Ashura.” Nini maana ya Falsafa ya kaulimbiu hii na kwa nini tunawaambia tuifanye kila ardhi ni Karbala na kuifanya kila siku yetu kuwa ni Ashura? Hili huwezekana tu wakati tutakapojua nini kilichokuwepo kule Karbala na nini kilichotokea siku ya Ashura.

Karbala ni jina la kukuza hisia katika jamii iliyokufa. Ni jina la uhai katika Umma uliokufa. Katika jamii hiyo iliyokufa miongoni mwa minyoo hiyo, mmoja ya minyoo ulio mchafu zaidi mno kwa jina la Yazid ukawa kiongozi wao, lakini Kiongozi wa Mashahidi (as) hakutafuta haki yoyote kutoka kwa mnyoo huu mkubwa, lakini badala yake yeye (as) alisema jukumu lake sio kuhifadhi minyoo hii au kudai haki kutoka kwa mnyoo huu mkubwa, bali kwa kweli jukumu langu ni kupuliza uhai kwenye jamii hii iliyokufa na kuweza kuihuisha.

Allah alimtunuku muujiza Mtume wake Isa (as) aliyekuwa akihuisha wafu (kwa idhini ya Allah). Wakati uhusiano kati ya mwili na roho ya mwandamu ulipovunjika, Nabii Isa (as) alikuwa akija na kufanya muungano huu tena (kwa idhini ya Allah). Alikuwa akija kwenye mwili uliokufa na kuuamuru uhuike kwa idhini ya Allah na mwili huu uliokufa ungehuika tena. Hivyo, kama mwili ukifa basi mkombozi (Masihi) wa mwili ni Ibn Mariam (as), lakini kama jamii ikifa basi mkombozi wa jamii hiyo ni Ibn Zahra – Husein (as). Isa (as) alikuwa akihuisha miili iliyokufa, lakini mwana wa Zahra (as) hupuliza uhai kwenye jamii na kuhuisha jamii zilizokufa.

Wakati Imamu Husein (as) alipoondoka Madina watu hawakuelewa alikuwa anaelekea wapi. Walidhani anakwenda kupigana vita, lakini kama hii ingekuwa ndio sababu basi angekwenda na wapiganaji pamoja naye, lakini tazama jeshi ambalo yeye (as) alilikusanya pamoja naye. Aliandaa jeshi ambalo lina wanadamu safi waliotakasika juu ardhi; hakuchagua wapiga mieleka wakubwa kwa sababu uwanja huu wa mapambano haukuwa kwa ajili ya wapiganaji wa mieleka, ulikuwa ni kwa ajili ya wanadamu waliotakasika. Yeyote yule aliyefikia kigezo cha utakaso alichaguliwa. Awe ni kijana, mtoto au mwanamke. Hii ni kwa sababu mtu yeyote anaweza kuihuisha jamii. Alikuwa akionesha mpango makini (formula) wa kuweza kuhuisha jamii zilizokufa. Watu walimuuliza ni kwa nini anachukua watoto na wanawake. Hili pia hutokea hata leo kwa wale watu wanaotoa ushauri. Walikuwa wakimshauri kwamba harakati hii ambayo Imamu (as) anaipanga sio sahihi, kwa sababu mtawala muovu kama Yazid yuko kwenye upinzani na hakuna wa kumsaidia (Imamu) na ataachwa akiwa ametengwa. Leo yuko mtu yeyote ambaye anaweza kusema kwamba ametengwa kiasi hicho kama Imamu Husein (as)? Kama mtu leo atawaasi angalau wenzake wachache na majirani mara moja watu wataungana naye. Lakini mtazame mwana wa Zahra (as)! Aliwalingania Mahujaji waungane naye lakini walikataa, aliwaita wageni waliokuja kuzuru kaburi la Mtukufu Mtume (saww) lakini wao pia walikataa, aliwaita wanaofanya ibada kwenye Msikiti wa Mtume, wanaozuru makaburi ya Baqii lakini pia hawakuungana naye; aliwaita watu wa Kufa na Basra lakini pia hawakuja; aliuita Umma wote lakini hakuna aliyekuja. Mwishowe alichukua familia yake mwenyewe na akaenda Karbala. Watu walikuwa hawaelewi ana maana gani, hivyo aliandika kwa mkono wake mwenyewe wosia na akampa ndugu yake Muhammad Hanafia ili watu wa zama ile na vizazi vijavyo wapate kuelewa kitu cha kufanya katika jamii wakati jamii hizo zikifariki.

Kunyonya damu na kukwangua minofu katika mwili uliokufa sio jukumu letu; jukumu letu ni kuchangia damu kwenye jamii zilizokufa. Jamii hazihuiki kwa kunyonya damu yao, kwa kweli hata jamii zinazoishi hufariki kama damu yao inanyonywa, ili kuhuisha kitu tunahitaji kukipa damu.