Mfano wa Jamii iliyokufa
Wale ambao wameishi vijijini au kukaa kwa muda kidogo vijijini, watakuwa wameona wanyama waliokufa. Wakati mnyama fulani kama ng’ombe akifa kijijini watu huchukua mzoga ule wa ng’ombe na kuutupa nje ya kijiji. Baada ya siku kidogo mzoga wa mnyama yule huoza, hunuka na pamoja na harufu hii maelfu ya minyoo (funza) hujitokeza kutoka kwenye mzoga ule. Minyoo hii imetokana na mzoga huu huu na inakula na kuishi katika mzoga huu huu. Minyoo hii haiingii kutoka nje ya mzoga badala yake inazaliwa ndani ya mzoga huo, hula minofu iliyooza ya mzoga huo, hunywa damu na usaha wa mzoga wa mnyama huyu, na pia huzaliana humo na kuongezeka idadi yao humo. Huongezeka kwa idadi kubwa katika mzoga huo wa ng’ombe kiasi kwamba kama hawa wangekuwa wanadamu wengi kiasi hicho tungehitaji kujenga jiji kubwa kwa ajili yao. Utakuwa umeona mandhari hii iliyotajwa ambako kuna mzoga wa ng’ombe ambao umelala kwa siku kadhaa, minyoo ikitoka kwenye mzoga huo, ikila minofu iliyooza na pia kuongezeka idadi yao. Sasa, kama ungeuonesha mzoga huu wa ng’ombe kwa mtu na kisha akasema kwamba mnyama huyu hakufa kwa sababu anaona mamilioni ya viumbe (minyoo) wakiwa katika harakati ndani ya mzoga wa ng’ombe huyu ambao wanakula, wanakunywa na kuzaliana, mara moja utabishana na kusema kwamba harakati hii ya minyoo ndani ya mzoga huu yenyewe ni ushahidi kwamba ng’ombe huyu amekufa. Kama minyoo hii isingekuwepo basi kungekuwa na uwezekano wa hoja, iwapo mnyama huyu yu hai au mfu. Hivyo sasa tunaweza kuhitimisha kwamba kama mamilioni ya minyoo inaonekana ikiwa katika harakati ndani ya mzoga wa kiumbe, basi kiumbe huyo hachukuliwi kuwa yu hai, ni mfu.
Tunaweza kuchukua mfano huu huu kuulekeza kwenye jamii. Wakati jamii ikifa kifo cha Umma basi watu wanaoishi ndani ya jamii hii iliyokufa hawawezi kuchukuliwa kama wako hai; kwa kweli mfano wao ni kama ule wa minyoo ndani ya mzoga. Kama mtu atasema katika mji wetu watu wana maduka makubwa, majumba, wanakula vyakula vya anasa, wana watoto, na wanawajibika kila mahali na wana familia kubwa, lakini jamii hii haina maisha ya “Umma”, basi harakati zote hizi na kula, kunywa kutaonesha kifo cha jamii hii. Kuishi maisha kama hayo ya minyoo ndani ya mwili uliokufa hakuchukuliwi kama maisha. Maisha yanayoendeshwa katika jamii iliyokufa ni maisha ya uvundo, wakati ambapo kama mtu atapita kwenye maisha haya atashika pua yake kujizuia na harufu mbaya ya jamii hii iliyokufa. Nimechukua tu jina la mwili uliokufa, na kwa kusoma tu utajisikia vibaya kidogo. Minyoo hii inazaliwa wakati jamii inapokufa. Jukumu na kazi ya minyoo hii ni kunyonya tu damu ya jamii iliyokufa, kukwangua minofu kutoka kwenye jamii na kuitafuna. Hufikiria kazi yao ni kula tu rushwa, kuishi kwa riba, kutengeneza dunia yao na kufikiria tu masilahi yao binafsi. Hawajali kuhusu afya na ustawi wa jamii, wanafurahia kunyonya damu ya jamii na kubeba marundo ya minofu ya jamii na kupeleka majumbani kwao. Tunajisikia vibaya hata kuzungumzia kuhusu viumbe hawa, hii ni kwa sababu siku zote kiumbe aliye hai anajisikia vibaya kuhusu mwili uliokufa.
Wakati tunapochukua jina la jamii zilizokufa tunajisikia vibaya na kusikitika, hivyo wakati majina ya jamii yanapochukuliwa mbele ya chanzo cha maisha, mtu ambaye atawapa wokovu wanadamu yaani Imamu wa zama, yeye (a.t.f.s) hawi na furaha, anafurahia tu majina ya jamii zile tu ambazo ndani yake dalili za maisha huonekana. Minyoo hii ndani ya mfu siku zote huomba maisha zaidi kwenye mwili huu mfu ili kwamba iweze kula minofu kwa siku nyingine zaidi, inaweza kunyonya damu na usaha kwa siku chache nyingine zaidi, na inaweza kuongeza kizazi chao zaidi kwa siku chache; haya ni maombi ya minyoo. Wanaomba kwa ajili ya mnyama mwingine zaidi kufa ili kizazi chao kimoja zaidi kipate kuishi. Kama Allah akianza kukubali maombi yao basi kutakuwa na minyoo tu ulimwenguni pote. Lakini Allah ameweka kanuni kwa ajili ya minyoo hii kwamba minyoo hii itaishi katika jamii kwa muda mfupi tu kwa kunyonya damu ya jamii. Lakini baada ya muda wakati damu hii itakapokauka, wakati maiti hii itakapooza kabisa basi minyoo hii vilevile itakufa. Hivyo sio kwamba watu wanaoishi katika jamii iliyokufa wataishi milele, wataishi tu muda jamii hii iliyokufa bado ipo. Siku moja myama huyu aliyekufa atatoweka kwa sababu ameliwa na kwisha. Hii ndio kanuni ambayo kwamba Allah ameiweka kwa ajili ya jamii zilizokufa kama ilivyotajwa katika Qur’ani Tukufu:
Tunapotaka kuangamiza mji, huwaamrisha wapenda anasa wake, lakini hufanya maovu humo; basi hapo kauli huhakikika katika mji huo na tukauangamiza maangamizo makubwa kabisa. (Surat Bani Israil 17 : 16)
Mji, maanana yake jamii, jumuiya au taifa. Ni kama Allah anasema: “Tunapotaka kuiangamiza jamii tunatengeneza minyoo ndani yake.”
Wapenda anasa, maana yake wale viumbe ambao wanataka tu kufurahia maisha yao. Maisha ya anasa na starehe hayahusiani na kuwa na mamilioni, huanza hata kwa kuwa na shilingi moja. Maisha ya anasa ni pamoja na pesa nyingi na kidogo halikadhalika. Watu hawa mafisadi huja na kufanya maovu na uchafu katika jamii kwa kiasi kwamba jamii hii iliyokufa hufikia hatua ya kuangamizwa. Wakati ikifikia hatua hii tunaiangamiza jamii hii pamoja na minyoo hii na kuifuta kabisa kuwepo kwao.
Na tukauangamiza maangamizo makubwa kabisa, tunaisaga kuwa unga, huipuliza katika majivu na hata majina ya jamii kama hizo hayakumbukwi. Maisha kama hayo, kama yale ya minyoo sio maisha.