Mauaji Ya Kikatili Ya Watu Wa Nyumba Ya Mtume
Ilikuwa Jumatano, siku ya kumi, (Ashura) ya mwezi wa kwanza wa Muharram kwa kalenda ya kiislamu katika mwaka wa 61 B.H. (13th October 680 A.D) Husayn alipomwambia mwanawe wa pili Ali Akbar, kuadhin minajili ya sala ya Alfajri ili kuwakumbusha na kuwazindua wale waliomuona na kumsikia Mtume juu ya utakatifu wake Husayn, kwa vile Ali Akber alifanana na Mtume kwa sauti yake na umbo lake pia.
Hili lilikuwa ni lengo la kuwazindua wale waliopotea, ili kuzuia umwagikaji wa damu. Kabla ya kuamkia usiku wa tukio la Ashura (Siku ya tisa maghribi), Abbas ibni Ali ambae ndie aliyekuwa muangalizi mkubwa wa usalama katika kambi ya Husayn, alitokwa na machozi akiona kila mwanamke akiungana na mumewe na watoto wao wakiwahimiza kujitolea kufa kwa kumsaidia Husayn. Huu ndiyo ulikuwa uthabiti wa imani yao kwa Imam. Husayn alipanga vikosi vya usalama, chini ya uongozi wa nduguye Abbas ibni Ali kujitetea mbele ya majeshi dhalimu ya Yazid.
Kama ilivyo, Husayn hakutarajia kupata sifa na ushindi akijitetea na akali ya watu aliyokuwa nao bali alikuwa na lengo la kuwakilisha na kudumisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mtume wake aliyemchagua. Alipochoka kuwasairi maadui wake, Husayn aliangua kilio na kuita:
“Iwapo dini ya Muhammad, haiwezi kunusurika bila ya ushahidi wangu (kukutuliwa), basi enyi mapanga, njooni mpate kunimaliza”. Kufikia wakati wa adhuhuri nusu ya watu wa Husayn walikwisha kukutuliwa (kuwa mashahidi) na baada ya kumalizika mashujaa wao ikaja zamu ya watu wa ukoo wa Hashimiya ingawa wafuasi hao walipigana na maadui mpaka dakika yao ya mwisho wa pumzi yao, hawakukubali vijana wa Hashimiya waingie vitani. Husayn juu ya fahari ya watu wake alitangaza akisema: “Hakuwa babu yangu wala baba yangu wala ndugu yangu aliyekuwa na watu waaminifu kama hawa wangu.”
Mmoja baada ya mmoja watu wa Husayn na marafiki zake walimalizwa, akiwamo Habib ibni Mazahir mwenye umri wa miaka thamanini na sita aliyekuwa rafiki yake mpendwa tangu siku zao za utotoni, Muslim ibni Ausajah, Hurr ibni Riyahi, John na Wahab na baadhi ya wengine. Wafuasi hawa hawakutokana na asili moja, kabila, wala nchi. Miongoni mwao mulikuwa na waafrika kumi na watatu waliojitolea kupigania upande wa Husayn wakawa mashahidi minajili ya dini ya Kiislamu na Mwenyezi Mungu. Ilipofika zamu ya vijana wa Hashimiya, waliokuwa baina ya umri wa miaka sita hadi thelathini na nne, hapo Husayn alimtoa kijana wake wa pili Ali Akbar aingie katika uwanja wa vita. Husayn alisema iwapo Mtume angekuwa pamoja nao katika vita hivi, basi yeye Husayn angechukua nafasi badala ya Ali Akbar kuunusurisha Uislamu.
Ali Akbar alifanana na Mtume katika kila njia na fani ya maisha yake hata kwa usemi wake na mwenendo wake wa tabia na umbile na alikuwa mzuri mno katika vijana wa Hashimiya na yeye alishahidiwa katika uwanja wa vita.
Habari za kifo cha kijana huyu, zikamfanya Husayn kuomboleza na kujiuliza: "Ni kitu gani kilichobaki ulimwengu huu baada ya kuondokewa na wewe?"
Qassim mtoto wa Hasan ibni Ali, ambae ombi lake lilikubaliwa baada ya kunyenyekea sana, alijitolea na kwenda vitani, alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu tu, kisha alikuwa ni yeye pekee ukumbusho wa Hasan kaka yake. Qassim alikanyagwa kanyagwa na kuthinyangwa na mafarasi wa maadui akiwa hai hata akafa.
Bibi Zainab, aliyeandamana na watoto wake wawili, Aun na Muhamad, wenye umri wa miaka sita na saba hivi walijitolea vitani na mara walikutuliwa pia, na Zainab akawachwa pekee. Mmoja baada ya mmoja vijana wote wa Hashimiya waliingia uwanja wa vita na kushahidiwa. Hatimaye kabla ya zamu ya Husayn mwenyewe kufika kwenda kupigania Uislamu, ndugu yake Abbas ibni Ali aliyekuwa shujaa mno mwenye nguvu na ujuzi mwingi wa kijeshi, alinyenyekea sana akitaka ruhusa ya kwenda yeye vitani ingawa alikatazwa mara nyingi. Badili yake, Abbas akaagizwa akateke maji kwa ajili ya watu wa nyumba kutoka mto wa El-Furat.
Ilikuwa ni siku tatu tangu jamii ya Mtume kuishiwa na maji ya kunywa toka watu wazima hadi mtoto mchanga wa miezi sita hawakuwa na tone la maji. Abbas ibni Ali alijitahidi, akafanikiwa kuteka na kujaza kiriba wa maji kutoka mtoni na alipokuwa akirejea huku amebeba kiriba chake, maadui walimshambulia kutoka nyuma wakihakikisha kwamba maji hayakufikia watoto wa kambi ya Husayn bali na kumuua nduguye Husayn aliyekuwa mpiganaji hodari, kiongozi mtukufu wa majeshi yote, akabakia Husayn peke yake. “Kwa hakika kifo (shahada) cha Husayn kitaamsha mori katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele.” Mtume Muhammad (s.a.w.w)
Mwisho Wa “Watu Wa Nyumba (Utaji)Akijikuta peke yake pasi kuwa na mtu aliyeko ndani wala nje ya kambi yake, Husayn aliita kwa sauti:
“Je... yuko yeyote wa kutusaidia?, yuko yeyote wa kutuitikia na kututimizia haja yetu?” Mwito huu haukuitikiwa na yeyote ila mtoto mchanga Ali Asghar ibni Husayn aliyekuwa wa mwisho katika watoto wake, ambae alikuwa na umri wa miezi sita tu, aliangua kilio kana kwamba kuitikia mwito wa babaake. Husayn alimbeba mtoto huyu mchanga akipapatika mikononi mwake kwa kiu ya maji, mtoto huyo hakuweza kustahimili dhiki, Husayn alitoka nae nje lakini ah... maadui walimjibu kwa kumfuma mtoto huyo kwa mshale wa vyembe vitatu na mtoto akafa mikononi mwa babaake. Husayn alirudi katika hema lake na mwili wa mtoto mikononi mwake. Mamaake alipomuona aliliya na kuomboleza akisema: “Je watoto wa umri wenu pia huuliwa namna hii?”
Husayn hatimae alimchimbia kaburi ndogo kwa upanga wake na kumzika mtoto huyo. Baada ya mazishi ya mtoto Ali Asghar yasiyo kuwa na sherehe yoyote, Husayn aliingia tena kambini, akamwita kila mwanamke mmoja mmoja aliyekuwako na watoto, akawaaga kwaheri ya mwisho, akamuaga dadake Zainab pamoja na binti yake Sakina aliyekuwa kipenzi cha moyo wake, ambae alikuwa na umri wa miaka minne tu. Alimnasihi kuvumilia na kuwa na subira juu ya dhuluma yote yatakayo kuja, kwa sababu ya matakwa ya Mwenyezi Mungu, kupitia kwa Mtume wake mtukufu, ni muhimu kuliko kumhusu yeye mwenyewe. Katika dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake mtukufu, hayana budi khususan kumuhusu yeye mwenyewe.
Hatimaye akiandamana na Zainab, Husayn akamwendea mtoto wake mkubwa, aliyekuwa akiugua siku nyingi, Ali Zainul Abideen, ambae ni mtoto mkubwa katika watoto wake na khalifa wakuelekea. Ali ibni Husayn, alivyokuwa katika hali ya maradhi kwa muda wa siku nyingi, hakuwa na khabari yoyote juu ya matukio ya siku na vifo vya watu wote wa babaake, alishtushwa na majeraha yaliyompamba babaake Husayn. Husayn alimtuliza na kumuaga kwaheri. Alipanda farasi wake mara ya mwisho akisaidiwa na dadake Zainab. Sasa Zainab ndiye mwangalizi mkuu wa usalama na jeshi katika kikundi chake kilichokuwa hakina yeyote, ila Zainul Abideen, Ali ibni Husayn na wanawake waliopotelewa na waume zao, watoto na ndugu zao kwa kushahidiwa vitani na baadhi ya watoto wachache. Husayn alisimama kati kati ya maadui na kuwaita akiwaambia wamuachilie na kusalimisha maisha yake ili apate kwenda zake baada ya kumuulia watu wake wote, marafiki zake, ndugu zake na wajomba zake na watoto wake ndani ya siku moja.
Jawabu lake alijibiwa kwa umoja wa maadui, kwamba hawatamuachilia hadi atakapomtambua Yazid licha ya alivyodokezewa na Mtume. Husayn hapo alisema na kujitambulisha nafsi yake mbele ya majeshi ya Yazid kwamba yeye ni mjukuu wa Mtume, mtoto wa Ali na Fatimah binti ya Mtume na ndugu yake Hasan na kuimwaga damu yake hakutawafalia chochote katika ulimwengu wao sasa na wa baadaye pia. Alijaribu pia kuamsha fikira zao akiwambia: “iwapo hamuamini katika dini yoyote basi fikirini kama watu walio huru” (kwamba yatendwayo si haki). Husayn mwenye umri wa miaka 57, bado alikuwa mkakamavu na mvumilivu juu ya kupoteza watu wake 72, katika kambi yake ambamo walikuwako miongoni mwao watu 18 wa jamii yake, ukoo wa Abu Talib. Naam, Husayn sasa alipigana kishujaa na maadui zake hata kufikia wakati wa sala ya Al-asiri, Umar bin Sa’ad aliamuru vikosi vyote vya majeshi yake wamzingire kwa umoja na kupigana naye.
Katika kipindi hicho ardhi yote ilitingishika, na jua lilipatwa na kutanda kiza cheusi kwa kutangazwa, “Husayn ameuawa katika Karbala, Husayn amekutuliwa katika Karbala” miongoni mwa sauti za maadui ilisikika na kuleta takbira ya “Allahu Akbar”, Mungu ni mkubwa, kwamba jamaa wa mwisho, mtakatifu wa nyumba ya Mtume (utaji) ameangushwa na kukatwa kichwa akiwa na njaa na kiu na Shimer ibni Joshan kwa tamaa ya kidunia aliyoahidiwa na Yazid. Dhuluma yao haikukomelea hapo kwa kumkutuli Imam Husayn, bali mwili wake pamoja na miili ya wenzie wote ilikanyagwa kanyagwa na kuvurugwa na kwato za farasi wa maadui kiasi cha kuangamizwa kabisa. Historiya inajidhihirisha yenyewe.
Baadaye majeshi ya Yazid, yaliwavamia watu wa nyumba ya Mtume na kuzitia moto hema zao, waliwapokonya wanawake mavazi yao ya mitandio na hijab za vichwani, wakawapokonya kila kitu chao kichache walichokuwa nacho, waliwapokonya hata na bembeya ya mtoto Ali Asghar; jamii ya Mtume ilitendewa kinyama ikidhalilishwa na kuchukuliwa mateka. Zainab binti Ali, “Fatimah” wa pili na mshirika wa Husayn alijitolea kishujaa nakusimama imara, akijipa nguvu na kupiga moyo konde, alivuta subira, baada ya kupotelewa na waume wote, alishika jukumu la kuwakinga na kuwasaidia wanawake wote na watoto pamoja na Zainul Abideen aliyekuwa mgonjwa akiugua ndani ya hema lililoshika moto na kuziponya nafsi zao. Alikuwa ndiye mwangalizi wao, mkuu wa usalama, alisamehe usingizi na kujitolea kukesha usiku kucha akitekeleza jukumu lake kuihudumia jamii yake iliyo athiriwa.
“Iwapo hamuamini katika dini yoyote basi tafakurini japo kama watu walio huru.” Imam Husayn bin Ali (a.s)