Change Language: English

MAPAMBANO DHIDI YA ASKARI WA IBN ZIYAD

Baada ya Imam Husein kuamua kutua hapo Kar-bala miongoni mwa wafuasi wake waliokuwa bora na wanaombatana naye mara kwa mara ni Bwana Nafii bin Hilal Al-Jamali.

Bwana huyu alikuwa hodari sana wa kupanga mbinu za mapambano ya vita hasa kwa kutokana na ujuzi mkubwa aliokuwa nao kuhusu mambo ya kisiasa.

Basi siku moja Imam (a.s.) akatoka nje ya mahema mpaka akawa mbali, Nafii akamuona Imam naye mara akachukua upanga wake na haraka akamfuata Imam (a.s.).

Nafii akamuona Imam akiwa katika harakati za kufanya uchunguzi kwenye mipaka ya maeneo ya mahema ya watu wake, mara Imam (a.s.) akageuka na akamuona Nafii akasema, "Nani wewe Nafii?"

Nafii naye akasema, "Ndiyo ewe mwana wa mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni fidia kwako".

Imam (a.s.) akasema kumwambia Nafii, "Ewe Nafii ni jambo gani Iililokutoa katika usiku huu?"

Nafii akasema "Ewe Bwana wangu kumeniogopesha kutoka kwako usiku kuelekea upande wa hawa maadui".

Imam (a.s.) akasema, "Ewe Nafii nimetoka ili kufanya uchunguzi wa maeneo yetu kwani nachelea hali ya usalama wetu siku tutapopambana na maadui hawa".

Nafii anasema, "Kisha Imam hali ya kuwa amenishika mkono wangu kushoto huko akisema "Wallahi hii ni ahadi isiyovunjwa".

Baadaye Imam Husein akasema kumwambia Bwana Nafii, "Ewe Nafii pita baina ya milima hii miwili (Ukimbie) uokoe nafsi yako?"

Nafii bil Hilal aliporomoka chini akaibusu miguu ya Imam (a.s.) akalia na huko anasema, "Ewe Bwana wangu, bila shaka upanga wangu thamani yake ni Dir-ham alfu moja kadhalika farasi wangu naye hivyo hivyo, namuapa Mwenyezi Mungu ambaye amenineemesha kwa kuwa pamoja nawe mahali hapa ya kwamba, sitakuacha mimi ni mtumwa wa Mungu naye atanilinda kwa hali yeyote itakayotokea". Nafii anasema: "Kisha Imam aliniacha na akaingia kwenye hema la dada yake Zainab bint Ali (a.s.), nami nikasimama namsubiri.

Bibi Zainab akamkaribisha Imam (a.s.) na akampa kiti akakaa na akawa anazungumza naye mazungumzo ambayo sikuwa nasikia kinachozungumzwa.

Basi mara ghafla bibi Zainab alilia na akawa anasema "Bila shaka nitashuhudia kifo chako, na huu ni mtihani mkubwa hasa utakapokuwa umeniacha kuwaangalia wanawake hawa waliojaa hofu na woga".

"Ewe ndugu yangu, kama unvyofahamu uadui walionao watu hawa toka hapo zamani, kwa hivyo jambo hili ni zito sana kwangu mimi, vifo vya vijana wa Kibanihashim ni msiba mkubwa sana kwangu".

Kisha Bibi Zainab akasema, "Ewe mtoto wa Mama yangu, hivi wazifahamu niya na dhamira zawafuasi wako? Bila shaka mimi nachelea kwamba watakutelekeza wakati wa mapambano". Imam Husein (a.s.) akalia kisha akasema, "Wallahi nimewajaribu ili nipate kuwafahamu Imani na niya zao, sikuona miongoni mwao isipokuwa ni watu mashujaa tena hodari wanafurahia kifo kwa ajili yangu na kuliwazika kama anavyoliwazika mtoto mdogo anyonyapo maziwa ya mama yake".

Nafii akasema, Nikalia kwa kumuonea huruma bibi Zainab, kisha nikamuendea Habib bin Mudhahir na nikamuona amekaa ndani ya hema lake, mkononi mwake ameushika upanga ulionolewa barabara huku anasema kama mtu anayesemesha upanga wake. "Ewe dhoruba ya upanga, jiandae kujibu mashambulizi pindi mapambano yatakapoanza".

Nafii anaendelea kueleza anasema, "Nikamsalimia Habib na akaniitikia kisha akasema, ewe ndugu yangu ni jambo gani lililokutoa nje usiku huu?"

Basi nikamsimulia mwanzo wa kisa cha mimi kutoka nje mpaka mahali ilipofikia Imam Husein (a.s.) kusema kwamba wafuasi wangu wanfurahia kifo kwa ajili yangu na wanaliwazika kama ambavyo mtoto anavyoliwazika pindi anyonyapo ziwa la mama yake".

Baada ya kuambiwa maneno haya Habib alisimama kisha akasema "Aa!!! Wallahi kama isingekuwa kusubiri amri ya Imam (a.s.) katika kuwashambulia adui zetu mimi ningewaanza kuwashambulia usiku huu kwa upanga wangu huu na wala asingemudu yeyote mapambano dhidi yangu"

Kisha Nafii akamwambia Habib "Ewe ndugu yangu nimemuacha Husein (a.s.) akiwa na dada yake Zainabu wakiwa na hali ya khofu, nadhani wanawake wengine nao watakuwa tayari wameungana na Bibi Zainab katika hali ya huzuni na majonzi, je waweza kuwakusanya wenzio ili muende mukawatulize nyoyo zao kuwaondolea woga walio nao, kwani nimeshuhudia hali ambayo siamini kama (Husein a.s) atabakia duniani hapa."

Habib akasema, "Mimi ninatii nakukubali utakavyo".

Pale pale Habib akaanza kuwaita jamaa zake akasema, "Wako wapi watu wakumnusuru Mwenyezi Mungu, wako wapi watakaomsaidia Mtume wa Mwenyezi Mdngu (s.a.w), wako wapi wasaidizi wa Amiril-Muuminina Ali (a.s.), wako wapi watakaomsaidia Fatma (a.s.) wako wapi watetezi wa Husein (a.s.), wako wapi watakaounusuru Uislam?

Wakachomoza kutoka katika mahema yao mfano wa simba wakali wenye kushambulia hali wakiongozwa na Abul-Fadhili Abbas (a.s.) (mdogo wake Imam Husein). Walipokwishakusanyika Habib akawaambia bani Hashim, "Rudini mahala penu (katika mahema yenu) hakuna haja ya kukesha".