Change Language: English

Mafundisho ya Imam Hussein AS (3)

Miongoni mwa sifa bora na za kuvutia za mwanadamu ni sifa ya ukarimu na kutenda wema. Katika utamaduni wa Qur'ani Tukufu ukarimu na mtu kutoa alichonacho kwa wasiojiweza, hisani na kusaidia waliodhulumiwa na kukandamizwa ni kielelezo cha kuhudumia wanadamu. Imam Hussein (as) kama walivyokuwa baba na babu yake watukufu, alikuwa dhihirisho kamili la ukarimu na kutenda wema.

Kamwe hakumrejesha mwenye haja aliyekwenda kwake bila ya kumsaidia, na hakuacha kutoa alichokuwa nacho kwa ajili ya kutatua matatizo ya maskini na wasiojiweza. Alikuwa akifanya jitihada kubwa kulinda heshima ya waombaji na wenye haja waliokwenda kwake na kukidhi haja zao kwa njia bora zaidi.

Imepokewa kwamba, bwana mmoja alikwenda kwa Imam Hussein (as) akiwa na nia ya kumweleza haja haja yake. Imam alitambua suala hilo kwa njia moja au nyingine na akamwambia: Ewe ndugu yangu! Eleza haja yako kwa njia ya maandishi nami nitajitahidi kukukidhia haja yako na kukufurahisha, Inshaallah. Bwana yule aliandika haja yake na Imam alimpa mara mbili ya kiwango alichokuwa ameomba.

Imam Hussein bin Ali (as) alijitahidi sana kuhakikisha kuwa, analinda heshima ya maskini na watu wasiojiweza wakati wa kuwahudumia na kukidhi haja zao. Imepokewa katika vitabu vya historia kwamba, siku ya Ashura baada ya mauaji ya Karbala kulionekana makovu ya majeraha ambayo hayakusababishwa na silaha za kivita kwenye mgongo wa Imam Hussein (as). Watu waliokuwepo hapo walimuuliza mwanaye, Ali Zainul Abidin (as) kuhusu makovu hayo. Alisema: makovu haya yametokana na mizigo na vifurushi alivyokuwa anabeba mgongoni na kwenye mabega yake nyakati za usiku kupeleka kwenye nyumba za watu wasio na wasimamizi, mayatima na maskini.

Imam Hussein (as) alikuwa karimu sana kuliko watu wote wa zama zake na hakulinganishwa na yeyote katika uwanja huo isipokuwa maasumina katika kizazi cha Bwana Mtume (saw). Miongoni mwa sifa zake kuu ilikuwa ile ya kuona haya na huruma kubwa kwa wasiojiweza wakati wa kutoa auni na msaada kwa maskini na wenye haja. Aghlabu ya watu huona karaha pale wanapokumbana na maskini au fakiri anayewaomba chochote njiani au kwengineko na pale wanapotoa fedha au chochote kumpa maskini huyo basi hufanya hivyo si kwa sababu ya kutenda wema au kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu, bali kwa ajili ya kuondokana haraka na kujiweka mbali na maskini huyo. Kinyume chake, Imam Hussein (as) alikuwa akipatwa na huruma kubwa wakati alipokuwa akikutana na maskini na mtu asiyejiweza na alijitahidi kukidhi haja yake tena kwa haya na kuomba radhi, na ikiwezekana bila ya kujulikana kwa ajili ya kulinda heshima na hadhi ya mwenye kuomba.

Wapenzi wasikilizaji baada ya kufariki dunia Mtukufu Mtume Muhammad (saw) kulitokea upotofu wa aina mbili katika Umma wa Kiislamu. Kwanza ni upotofu wa Waislamu katika suala la uimamu na khalifa wa Mtume baada ya mtukufu huyo kufariki dunia, na upotofu wa pili ambao ulidhihiri kadiri muda ulivyopita ni ule wa kubadilishwa thamani, maadili na mafundisho halisi ya Uislamu. Katika zama za Imam Hussein bin Ali (as) upotofu huu wa kubadilishwa matukufu na mafundisho ya Uislamu ulifika kiwango cha juu sana kwa kadiri kwamba, mtu kama Yazid bin Muawiya ambaye alikuwa mashuhuri kwa ufuska, ulevi na kadhalika, alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu! Inatupasa kuelewa hapa kuwa, hata baba yake Yazid mlaaniwa, Muawiya bin Abi Sufiani pia alikuwa mtu fasiki na muovu kama mwqanaye Yazid lakini alifanya hila na ujanja wa kuficha maovu hayo mbele ya watu na kadamnasi ya kujidhihrisha kuwa mtu wa dini.

Yazid alisisitiza kwamba Hussein bin Ali anapaswa kuwa mtu wa kwanza kumpa mkono wa utiifu na kukubali utawala wake. Hii ni kutokana na kwamba alijua vyema nafasi ya Imam Hussein (as) katika Umma wa Kiislamu.

Baada ya liwali wa Yazidi mjini Madina kumtaka Imam ampe baia na mkono wa kutii na kukubali utawala wa Yazid, Imam Hussein (as) aliondoka katika mji mtakatifu wa babu yake wa Madinatul Munawwara nyakati za usiku. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Imam alitambua vyema kwamba, kama atabakia katika mji huo atalazimishwa kutoa mkono wa utiifu la sivyo atauawa bila ya damu na mauaji yake kuwa na taathira kubwa katika Umma. Kwa msingi huo aliondoka Madina na kuelekea Makka. Akiwa huko pia aligundua njama za kutaka kumuua, hivyo alikatisha amali na ibada ya Hija na badala yake akafanya ibada ya Umra na kisha akaanza safari ya kuelekea Kufa nchini Iraq. Imam alielewa kwamba, kubakia Makka kuna maana ya kuuliwa, jambo ambalo kwanza lingevunjia heshima Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, na pili kwa kutilia maanani kwamba kuuliwa kwa aina hiyo hakutakuwa na faida na athari yoyote katika mustakbali wa Uislamu. Imam alichukua hatua zake zote kwa kutumia mantiki na umakini mkubwa. Katika harakati zake zote za kuanzia Madina hadi Karbala alifanya juhudi kubwa za kukusanya watu ambao alihisi kwamba wanaweza kuwa na taathira kubwa katika kuimarisha fikra za Kiislamu. Wakati mwingine watu waliathirika na kuvutiwa na Imam Hussein baada ya kuingia katika hema lake na kuzungumza naye tu, na wakati mwingine wako waliojiunga na Imam baada ya kupokea wito na barua za mtukufu huyo akieleza falsafa na malengo ya harakati yake kama ilivyokuwa kwa mtu kama Zuhair ibn Qayn.

Harakati za kimantiki za Imam Hussein (as) ziliendelea hata katika ardhi ya Karbala. Imam alifanya mazungumzo na Umar bin Saad, kamanda wa jeshi la Yazid, na kulihutubia jeshi la mtawala huyo dhalimu na hakuacha kutumia njia zote za mantiki na busara hata baada ya kutambua kuwa, hakuwa na njia nyingine isipokuwa kupambana na kuuawa shahidi. Kusimama kidete kwa wapiganaji 72 mbele ya maelfu ya askari wa Yazid bin Muawiya tangu asubuhi ya siku ya Ashuraa mwezi Muharram mwaka 61 hadi wakati wa adhuhuri wa siku hiyo kunadhihirisha tabdiri kubwa ya Imam Hussein na taathira ya maneno na misimamo yake. Watu wote walielewa kwamba, idadi hiyo ndogo ya masahaba wa Imam Hussein haiwezi kubakia hai mbele ya maelfu ya wapiganaji wa jeshi la Yazid na kwa msingi huo wangeweza kuuawa shahidi mapema asubuhi ya siku hiyo. Hata hivyo jeshi hilo dogo kwa idadi lakini kubwa kwa imani na msimamo thabiti lilipangwa na kutayarishwa vyema na Imam kwa kadiri kwamba, muda mfupi tu baada ya mtukufu huyo kuuawa shahidi yeye na masahaba zake, misingi na nguzo za utawala wa Bani Umayyah zilianza kuporomoka ndani kwa ndani.

Zuhair bin Qain alikuwa mtu sharifu na mwenye heshima na hadhi kubwa kati ya watu wa kabila na kaumu yake. Alikuwa mpiganaji shupavu na shujaa na aliishi baina ya kaumu yake katika mji wa Kufa nchini Iraq. Wakati Imam Hussein (as) alipokuwa mjini Makka, Zuhair pia alikuwa katika mji huo mtakatifu na watu wa kabila lake wakitekeleza ibada ya Hija. Aliposikia kuwa Imam amekatiza ibada ya Hija na kuelekea Kufa, alikuwa na wasiwasi mkubwa wa kukutana naye uso kwa uso. Hii ni kwa sababu, kutokana na propaganda chafu zilizokuwa zimeenezwa na Muawiya bin Abi Sufiani akidai kuwa Imam Ali bin Abi Twalib alishiriki katika kumwaga damu ya khalifa wa tatu, Uthman bin Affan, Zuhair aliathiriwa na uongo huo. Hivyo hakuonesha mapenzi kwa Ali bin Abi Twalib na watoto wake.

Akiwa safarini kurejea Kufa, Zuhair alijiepusha kusimama mahala popote msafara wa Imam Hussein uliposimama. Hata hivyo katika safari hiyo msafara wa Zuhair ulitua na kupumzika bila ya kujua katika sehemu iliyokuwa karibu na eneo msafara wa Imam Hussein ulipofikia. Zuhair na watu wa kaumu yake walikuwa wakipata chakula, ghafla mjumbe wa Imam aliwasili katika eneo hilo na kumwambia: "Ewe Zuhair bin Qain! Abu Abdillahil Hussein amenituma kwako na anakuita uende kwake."

Kimya cha ajabu kiligubika hadhirina wote. Kila mtu aliweka chini tonge lililokuwa mkononi mwake. Wakati huo mke wa Zuhair bin Qain, Dulham, alisimama na kusema: Subhanallah! Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu anakuita kisha unasita kuitikia wito wake?! Kwa nini huendi kwake na kusikia anasema nini?

Zuhair alitikiswa sana na maneno hayo ya mkewe. Alipiga ukelele kwa sauti kisha akainuka na kuelekea mbiyo upande wa hema la Imam Hussein (as). Muda mfupi baadaye, Zuhair alirejea haraka kwenye hema na kambi ya kaumu na jamaa zake akiwa mwenye bashasha. Haiba ya Hussein (as) ilimteka Zuhair bin Qain kwa kadiri kwamba, katika muda mfupi tu alikata uhusiano wake na dunia, milki na kila alichokuwa nacho. Aliamuru mahema yakusanywe na kuhamia katika kambi ya Imam Hussein (as). Zuhair bin Qain alimwambia mkwewe kwamba: Mke wangu Dulham! Nakuacha na kukupa talaka na sasa uko huru kwenda unakotaka, kwani sitaki kuona unapatwa na masaibu kwa sababu yangu mimi. Aliwageukia jamaa zake na kuwaambia: Kila mtu anayetaka kuandamana na mimi, aje.. Huu ndio wakati wa mwisho wa kuwa pamoja nanyi. Kisha Zuhair aliondoka na kujiunga na Imam Hussein (as).

Image Caption

Usiku wa siku ya Ashura yaani tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria wakati Imam Hussein alipowaambia masahaba zake kwamba, watumia giza la usiku kuondoka ili wasije kuuawa pamoja naye na kwamba adui anamtaka yeye, Zuhair bin Qain alisimama na kusema: Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba: Ninapendelea kuuawa shahidi na kufufuliwa kisha niuawe mara elfu moja na kufufuliwa kwa ajili ya kukulinda na balaa wewe na vijana katika Ahlubaiti wako.

Wakati wa mapigano ya siku ya Ashura, Zuhair aliingia katika medani ya mapambano kwa ushujaa usio na kifani. Alibariziana na maadui wa mjukuu wa Mtume (saw) akisema: Mimi ni Zuhairi, mwana wa Qaini. Kwa panga langu namlinda Husseini, na kumuweka mbali na nyinyi.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.