Mafundisho ya Imam Hussein AS (2)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Mpenzi msikilizaji tunaendelea kukuleteeni mfululizo wa makala hizi za Mafundisho ya Imam Husain AS ambao ni maalumu kwa ajili ya mwezi huu mtukufu wa Muharram kwa ajili ya kuzungumzia mapambano ya Imam Husain AS katika jangwa la Karbala lililoko Iraq ya leo.
Naam, tunaendelea kuzungumzia mapambano ya Imam Husain AS kwa kusema kwamba, kuna baadhi ya watu wanasema kuwa: Imam Husain AS aliamua kutoka Madina na kuelekea katika mji wa Kufa huko Iraq kuitikia maombi ya wakazi wa eneo hilo kutokana na kupokea barua nyingi sana za watu wa eneo hilo la Iraq waliokuwa wako chini ya ukandamizaji mkubwa na ambao walimuomba aende kwenye mji huo ili akasimamishe utawala wa Kiislamu. Hivyo kwa mujibu wa watu hao, matukio ya Karbala na Ashura ni matunda ya kuitikia Labeika Imam Husain AS maombi ya wakazi hao wa Kufa! Hata hivyo na hata kama sababu iliyomfanya Imam Husain AS aelekee Kufa ni kuitikia mwito wa wakazi wa mji huo, lakini qiyam na mapambano ya Imam Husain AS dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayyah yanatoa maana pana zaidi ya hiyo.
Katika Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu anazungumzia suala la ushujaa na kutomuogopa yeyote ila Mwenyezi Mungu tu na kuwasifu watu watukufu walioshikamana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa kusema: ...wanamwogopa Yeye (Mwenyezi Mungu tu), na wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Ndiye atoshaye kuhisabu. Suratul Ahzab, aya ya 39.
Tunapozingatia aya kama hizo za Qur'ani Tukufu, tutauona kwa uwazi kabisa ushujaa wa Imam Husain AS kwenye mapambano yake ya Karbala. Katika mapambano hayo, Imam alithibitisha kwa damu yake, kwamba alikuwa mja mwema ambaye hakumuogopa yeyote ila Mwenyezi Mungu Mtukufu tu.
Imam Husain AS alikuwa ni maarufu kwa ushujaa wake tangu udogoni mwake. Hilo linathibitishwa na marafiki na maadui zake. Historia imethibitisha kwamba katika kipindi cha ubarobaro, Imam Husain AS alisimama kidete kupambana na watu wanaoleta upotofu katika dini na hakusita kusema ukweli kila alipoona dini ya Mwenyezi Mungu inapotoshwa. Alikuwa na msimamo imara kiasi kwamba, watu waliokuwa wakijifanya wanayajua vizuri mafundisho ya Uislamu wakati hawakuwa na elimu nayo, walikuwa wakikumbwa na woga mkubwa kila alipojitokeza Imam Husain AS. Hamasa kubwa iliyojengwa na mtukufu huyo katika kipindi chake cha ujanani ilionekana kwa uwazi kabisa katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawan, na watu wote, mkubwa kwa mdogo, waliusifia ushujaa mkubwa wa mtukufu huyo. Aidha kila sehemu alipoongoza jeshi la Kiislamu, jeshi hilo lilipata mafanikio makubwa. Na kila sehemu makamanda wa Kiislamu walipokwama, ushujaa wake ndio uliokuwa ukikwamua na kuyafungulia njia majeshi ya Waislamu.
Imam Husain AS alisimama imara kupambana na maadui wa Uislamu na watumiaji mabavu na waistikbari wa zama hizo kwa nguvu zake zote, na kila alipohisi ni wajibu wake kuchukua hatua, alilinda haki kwa nguvu zake zote, na kwake yeye wafuasi wa batili walionekana wadogo sana. Wakati Waislamu walipokuwa katika mazingira magumu sana na ukata mkubwa kutokana na ukosefu wa uadilifu uliofanywa na utawala wa Muawiya, misafara mikubwa ya fedha zenye thamani kubwa ilikuwa ikitumwa kwenye kasri ya Muawiya kutoka Yemen ili kwenda kutumika katika maisha yake ya anasa na familia yake, Imam Husain AS alisimama imara kukabiliana na dhulma hiyo. Imam AS ambaye alichukizwa mno na vitendo vya kitaghuti vya Bani Ummayah vilivyokuwa vinakwenda kinyume kabisa na mafundisho ya dini ya babu yake Bwana Mtume Muhammad SAW na baada ya kuona nasaha zote alizokuwa akimpa Muawiya hazikuzaa matunda, alichukua uamuzi wa kuzuia msafara wa fedha na mali za Waislamu wa Yemen usimfikie Muawiya na badala yake akatumia mali hiyo ya Waislamu kuwapa wahitaji kwa ushujaa mkubwa.
Imam Husain AS alikuwa na ushujaa mkubwa katika kutangaza na kubainisha ukweli na kufichua uovu na upotoshaji wa baadhi ya watu. Alipokuwa mwishoni mwa umri wake, Muawiya alifanya njama za kumtia nguvu mwanawe Yazid na kumpachika sifa kubwa kubwa. Siku moja alimsifia mwanawe Yazid mbele ya Imam Husain AS na watu maarufu na mashuhuri wakati huo. Imam Husain AS alisimama na kutoa hotuba muhimu na kali sana ya kubainisha ufisadi wa Yazid na kumlaumu vikali Muawiya kwa kujaribu kumsafisha mwanawe fisadi na muovu. Hotuba hiyo kali ilivuruga njama za Muawiya.
Kilele cha uongofu na ushujaa wa Imam Husain AS kilidhihirika katika Siku ya Ashura. Siku hiyo alipambana na jeshi kubwa la adui akiwa amebakia peke yake huku akiwa na kiu kali mbele ya jeshi la watu 30 elfu la adui. Wakati huo alipoangalia katika kila upande aliona viwiliwili vya wapendwa wake na wafuasi wake wakiwa wameuawa kikatili na katika upande mwingine aliwaona akinamama na watoto wadogo kutoka kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW wakiwa hawana pa kukimbilia. Lakini pamoja na hayo, hakutetereka hata kidogo na kamwe woga haukuigusa nafsi yake, bali alipambana kwa ushujaaa mkubwa sana, kiasi kwamba haijawahi kushuhudiwa katika historia ushujaa mkubwa wa namna hiyo. Mwenyezi Mungu anasema katika Suratul Maida aya ya 54 kwamba: Enyi mlioamini! Atakayeiacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakujaleta watu anaowapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anayelaumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na Mwenye kujua.
Kama tulivyotangulia kusema kwenye makala hii, kuna baadhi ya watu wanasema kuwa, barua za watu wa Kufa ndizo zilizomfanya Imam Husain AS afunge safari kutoka Madina kwenda Kufa huko Iraq. Kwa maneno mengine ni kuwa, watu hao wanaamini kwamba, kama watu wa Kufa wasingelimwandikia barua Imam, basi tukio la Karbala lisingelitokea. Hata hivyo mapambano ya Imam Husain AS dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayyah yanaonesha kuwa, hata kama Imam alielekea Iraq baada ya kuandikiwa barua ya watu wa Kufa, lakini mapambano yake yana upeo mpana zaidi. Imam Husain AS ni mwana wa Simba wa Mwenyezi Mungu, Imam Ali bin Abi Talib AS, kamwe asingeliweza kukaa kimya na kuangalia kwa macho tu namna dini ya babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW ikivurugwa na kupotoshwa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wakati Marwan bin al Hakam, liwali wa Madina alipomwita Imam Husain AS kumtaka ampe bay'a ya utii Yazid, Imam alimkaripia na kusema: Innalillahi Wainna Ilayhi Rajiun! Wakati umma wa Kiislamu utakapoingia mikononi mwa mtu muovu kama Yazid, itabidi kuuambia kwaheri Uislamu. Na ni kwa sababu hiyo ndio maana Imam Husain AS aliamua kuingia katika hatua na awamu ya kuufufua Uislamu wa asili aliokuja nao babu yake, Bwana Mtume Muhammad SAW.
Katika awamu hiyo ya pili Imam Husain AS aliamua kutoka nje ya mji mtakatifu wa Madina kwa ajili ya kupambana na ufisadi na kufufua dini ya Uislamu. Na hilo alilisema wazi wakati alipomuaga mdogo wake Muhammad bin Hanafiya kwa kumwambia: Mimi siondoki Madina nikiwa sijui ninachofanya, au kwa ajili ya kufanya jeuri au kufanya uovu au dhulma; bali ninatoka Madina kwa ajili ya kwenda kupigania marekebisho katika umma wa babu yangu. Ninatoka kwa ajili ya kuamrisha mema na kukataza maovu na kutekeleza sira ya babu yangu na baba yangu Ali bin Abi Talib AS.
Tab'an wakati wa utawala wa Muawiya, Imam Husain AS alitekeleza jukumu lake la kuamrisha mema na kukataza mabaya kila alipopata fursa ya kufanya hivyo. Katika moja ya safari zake za kuelekea Makkah, mtukufu huyo alizungumza na kundi la maulamaa na wanachuoni wa maeneo mengine na kutoa hotuba kali sana. Katika hotuba yake hiyo, sambamba na kuwakumbusha maulamaa hao majukumu mazito na ya hatari waliyo nayo katika suala zima la kulinda na kuipigania haki, aliwaonya kuhusu madhara ya kunyamazia kimya jinai zinazofanywa na watawala wa Bani Umayyah, na kuwalaumu wale wote waliokaa kimya mbele ya ukandamizaji huo. Alisema, kushirikiana na kupatana kwa namna yoyote ile na watawala hao ni madhambi yasiyosameheka. Miongoni mwa matamshi muhimu sana ya Imam Husain ni pale aliposema, nimetoka kwa ajili ya kupigania marekebisho katika umma wa babu yangu. Aidha aliposema, kama dini ya Muhammad haiwezi kusimama ila kwa kuuawa mimi, basi enyi panga, ichukueni roho yangu.
Maneno yote ya Imam Husain AS aliyoyasema kwenye kipindi chote cha kuelekea Karbala, yamehifadhiwa katika historia. Maneno hayo yanaonesha nia ya ndani ya moyo wake ya kufunga safari kutoka Madina kuelekea Iraq, na namna alivyokuwa akibainisha upotofu wa utawala wa Yazid bin Muawiya na wajibu wa kupambana nao. Ni vivyo hivyo alivyosema wakati alipoona na Hur, kamanda wa jeshi la Yazid, ambapo alibainisha kwa uwazi lengo lake na kwa kutegemea hadithi ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kusema: Enyi watu! Watu hawa wameomkubatia shetani na kuacha kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Wameonesha wazi ufisadi wao, na kudharau mipaka ya Mwenyezi Mungu. Mayazid wameifanya Baytul Maal ya Waislamu kuwa ni mali yao binafsi na wamehalalisha haramu ya Mwenyezi Mungu na kuharamisha halali Yake na mimi ndiye mtu bora kabisa wa kuweza kuleta marekebisho katika masuala ya Waislamu.
Msafara wa Imam Husain AS ulianza safari ya kutoka Madina kuelekea Kufa Iraq. Mkuu wa msafara huo alikuwa ni yeye mwenyewe. Imam zilimfikia habari ya kuvunjwa mapambano ya Mashia wa Kufa na kuuawa shahidi kidhulma Muslim bin Aqil, mauaji ambayo yalifanywa na vibaraka wa Abdullah bin Ziyad. Lakini msafara ulikuwa tayari uko njiani kuelekea Kufa. Ilipofika Adhuhuri, mmoja wa watu wa msafara huo kwa mastaajabu alisema Allahu Akbar! Imam Husain AS alimuuliza sababu ya kusema Allahu Akbar. Alijibu kwa kusema, tumeanza kuiona mitende ya Kufa. Imam alimjibu kwa kumwambia, hiyo si mitende, bali ni jeshi kubwa lililojizatiti kwa silaha, linakuja upande wetu. Msafara wa Imam ukasimama, muda haukupita, jeshi la watu elfu moja lililoongozwa na Hur bin Yazid ar Riyahi lilifika hapo. Imam aliona namna wanajeshi hao walivyokuwa wamechoka. Hivyo alitoa amri wapewe maji wao na wanyama wao.
Baada ya kusali, Imam Husain AS aliwaamrisha wafuasi wake waendelee na safari, lakini Hur aliwazuia. Imam alimuuliza sababu za kuwazuia wasiendelee na safari. Hur akajibu kwa kusema: Mimi sikupewa amri ya kupigana na wewe, lakini nimepewa amri ya kukuzuia usije ukakanyaga Kufa. Ni matumaini yangu kuwa hakuna baya lolote litakalotokea baina yangu na wewe. Ewe Husain! Iokoe roho yako kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na usiingie kwenye vita hivi, kwani ukiingia vitani, lazima utauawa!
Imam alimjibu kwa kumwambia: Unaniogopesha mimi kwa kifo? Je, kwa kuniua mimi mambo yako yatatengenea? Baada ya hapo Imam aliendelea na safari yake kuelekea upande wa Karbala. Hur akamtumia mjumbe Ibnu Ziyad kumueleza mazungumzo yaliyojiri baina yake na Imam Husain AS. Wakati habari hiyo ilipomfikia Ibnu Ziyad, msafara wa Imam Husain AS ulikuwa tayari umeshafika Karbala. Ibnu Ziyad akamwandikia barua Hur na kumwambia, mara barua hii itakapokufikia, uzuie msafara wa Husain katika jangwa kavu, lisilo na maji wala majani! Hur naye alitekeleza amri hiyo na kumwambia Imam Husain AS kwamba: Siwezi kukuruhusu uendelee mbele zaidi ya hapa. Kwani Ibnu Ziyad ameniwekea majasusi ili kuangalia nitatekeleza amri yake au la. Mtu mmoja alimshauri Imam apambane na Hur, lakini Imam hakukubaliana na ushauri huo na alisema: Sisi kamwe hatutakuwa waanzishaji wa vita. Muda ukapita, hadi ukamanda wa jeshi ukaingia mikononi mwa Omar bin Saad.
Asubuhi ya siku ya Ashura, majeshi ya pande mbili yakawa yamekabiliana. Hur alijiweka pembeni na kumwambia mmoja wa wafuasi wake: Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Hivi sasa najiona nipo baina ya moto na pepo. Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Siwezi kuchagua kitu chochote isipokuwa pepo, hata kama mwili wangu utakatwa vipande vipande na kuchomwa moto. Baada ya kusema hayo alielekea upande wa Imam Husain AS.
Alipofika kwa Imam, alisema huku akiona haya: Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi ndiye niliyokufungia njia. Sikuwa na nia kabisa ya kupigana na wewe. Hivi sasa nimekuja kwako nikiwa na haya nyingi usoni, je, toba yangu ni yenye kukubaliwa? Imam alimjibu kwa upole akimwambia: Naam! Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba za waja Wake.
Baada ya hapo Hur alipambana kwa ushujaa wa aina yake na maadui wa Imam Husain AS. Lakini hatimaye nguvu zilimuishia, akaanguka chini kwenye dimbwi la damu. Masahaba wa Imam Husain AS wakaupelekea kwa Imam, mwili wake uliokuwa katika sakaratul maut. Imam akawa anafuta damu kwenye kipaji cha shujaa huyo akisema: Umeshakuwa huru kama jina lako ulilolopewa na mama yako mzazi.
Wasikilizaji wapenzi, na kufikia hapa ndipo tumetamatisha sehemu hii ya pili ya makala hii maalumu ya Mafundisho ya Imam Husain AS. Ni matumaini yetu mumenufaika vya kutosha. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.