Change Language: English

Maadhimisho ya Maulidi ya Mtume Muhammad SAAW - Wiki ya Umoja

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja ambacho ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia. Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.
Sheikh Muhammad Arafa mmoja wa maulama mahiri na watajika wa Chuo cha al Az'har nchini Misri anasema: "Ujazi na neema kubwa kabisa ya Mwenyezi Mungu kwa Waislamu ni mshikamano, mahaba na kuziunganisha nyoyo zao. Hii inatokana na kuwa katika kipindi cha kabla ya Uislamu, ujahilia na uadui ndio uliokuwa ukitawala baina ya watu. Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya Aali Imran aya ya 103:
"Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu."
Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 63 ya Sura ya al Anfaal:
"Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima."
Sheikh Muhammad Arafa amebainisha umuhimnu wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu akinukuu aya za kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Mwanazuoni huyo anaamini kwamba, maulama na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu wana nafasi muhimu katika kuwaunganisha au kuwatenganisha Waislamu.
Ukweli wa mambo ni kuwa, katika kipindi cha miaka mia moja iliyopita, warekebishaji wa nchi za Kiislamu, wamefganya hima na idili kubwa katika uga wa umoja wa Kiislamu. Katika muongo wa 50 kuna maulama na wanafikra wengi wa Kisuni na Kishia ambao walifanya juhudi kubwa za kutundika juu bendera ya kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu katika nchi mbalimbali za Kiislamu. Miongoni mwa maulama hao ni Sheikh Mustafa Abdur Razaaq, Sheikh Abdul Majid Salim na Sheikh Mahmoud Shaltut ambao wopte hao ni maulama wa Kisuni. Kwa upande wa maulama wa Kishia waliokuwa mstari wa mbele katika harakati ya kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu na kupiga hatua muhimu katika uga huu ni Ayatullah Sheikh Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa, Sayyid Sharafudeen Musawi, Ayatullah Burujerdi na Sayyid Hibatudeen Shaharistani.
Katika kipindi chote hiki wanafikra wengi wa Kiislamu walifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuleta kizuizi kikubwa kwa jina la Umma mmoja wa Kiislamu ili umma huu uwe ni mkono mmoja mkabala na ulimwengu wa kikoloni. Miongoni mwa shakhsia waliokuwa na nafasi muhimu katika uga huu ni Sayyid Jamaludeen Asad Abadi.
Katika muongo wa 60 Miladia, kulisikika sauti kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ya wito wa umoja na mshikamano kutoka kwa Imam Ruhullah Khomeini mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kuliendelea hilo Imam Khomeini alitoa wito katika minasaba na hatua mbalimbali wakati wa kuchanua Mapinduzi ya Kiislamu na kuonyesha umuhimu wa umoja wa kalioma na kushikamana Waislamu. Kutangazwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds na siku ya Waislamu kuonyesha kufungamana kwao na wananchi wa Palestina kwa ajili ya kuikomboa Quds Tukufu, kutangazwa Wiki ya Umoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa hatua muhimu za Imam Khomeini za kuleta umoja nma mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Aidha Ayatulllahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa pendekezo la kuasisiwa Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu katika fremu ya umoja na kuhuisha adhama ya Waislamu.
Nukta muhimu na ya kuzingatia ni hii kwamba, Umma wa Kiislamu una uwezo mkubwa na suhula nyingi ukiwemo utajiri mkubwa wa nishati ya mafuta na gesi bila kusahau nguvu kazi kubwa iliyoko katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa kuzingatia uhakika na ukweli huu, ubeberu umekuwa ukitumia nguvu zake zote kwa ajili ya kuendesha njama za kishetani dhidi ya nguvu hii muhimu yaani umoja na mshikamano wa Waislamu na mabeberu wakiwa na nia ya kufikia malengo yao machafu wamekuwa wakitumia kila wenzo. Hata hivyo, licha ya njama zote hizo za maadui, jamii za Kiislamu zimekuwa zikipiga hatua na kusonga mbele katika njia ya umoja na mshikamano.