Kufunga Saumu Siku Ya Ashura
Baadhi ya Ahadith zinapatikana katika vitabu vya Ahl as-Sunnah kwamba Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipofanya Hijrah kwenda Madina aliwaona Mayahudi wakifunga saumu siku ya Ashura, tarehe 10 ya mwezi mtukufu Muharram. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliwauliza sababu ya kufanya hivyo, alijibiwa :
“Ni Siku njema, ni Siku ambayo Mungu alipowaokoa watoto wa Israil kutokea maadui wao ( yaani Firaun ); na, hivyo, Mtume Musa a.s. alifunga saumu siku hiyo.”
Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Akasema :
“Mimi namtukuza na kumsatahiki Mtume Musa a.s. kuliko nyinyi”
Hivyo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alifunga saumu siku hiyo na kuwaamrisha Waislamu wawe wakifunga siku hiyo.2
Imeandikwa na Mfasiri wa Mishkatul-Masabih kuwa :
“Ilikuwa katika mwaka wa pili, kwa sababu mwaka wa kwanza ulikuwa ni mwaka ambapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa ameingia Madina baada ya ‘Ashura, katika Rabiul-Awwal.”
Umuhimu huo unaweza kupimwa na kuamuliwa kutokana na Hadith nyingineyo iliyoelezwa katika al-Sahihya al-Bukhari :
“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwamrisha mtu mmoja kutokea kabila la Aslam: Watangazie watu wote kuwa yeyote yule aliyekwisha kula chochote basi afunge saumu kwa sehemu ya siku hiyo iliyobakia na yeyote yule ambaye hajala chochote kile, basi afunge saumu siku hiyo nzima, kwani leo ni Siku ya ‘Ashura ( tarehe 10 ya Mwezi wa Muharram)”
Ni katka mwaka huo huo ambapo saumu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zilipofaradhishwa na kuondolewa na kubatilishwa kwa kufunga saumu katika siku ya ‘Ashura, kama vile ilivyodaiwa katika Hadith zinginezo ambazo zimenakiliwa katika kitabu hicho hicho. Lakini jambo la kustaajabisha ni kwamba pamoja na kuelwea ukweli kuwa saumu hiyo imeondolewa, bado saumu hiyo ya siku ya ‘Ashura inapewa umuhimu kuwa ni saumu Sunnah.
Sasa tujaribu kuzichunguza Ahadith hizi kwa undani zaidi :
1. Kwanza:
Wayahudi walikuwa na kalenda yao na miezi yao. Hakuna mantiki yoyote kuwa wao walikuwa wakifunga saumu siku ya ‘Ashura yaani tarehe 10 ya Mwezi wa Muharram – hadi hapo itakapokuja kuthibitika kuwa siku hii ya ‘Ashura itakuwa ikipatana au kuingiliana na siku ya kufunga katika Mayahudi.
Imezungumzwa katika makala yangu ya Martyrdom of Imam Husayn and the Muslim and the Jewish Calendars" (Alserat, Vol.VI, No's 3 & 4; Muharram 1401 Nov.1980) kuwa mwezi wa kwanza wa Kiyahudi
(Abib, uliokuja kuitwa Nisan hapo mbeleni) ulikuwa ukiingiliana na Mwezi wa Kiislamu unaoitwa Rajab. W.O.E. Oesterley na Theodore H.Robinson wameandika kuwa katika Arabia Siku Kuu kuliko siku kuu za kusherehekea zote za mwezi mpya ilikuwa imeangukia katika mwezi wa Rajab, iliyokuwa sawa na mwezi wa Kiyahudi wa ‘Abib, huu ndio uliokuwa kipindi ambacho Waarabu wa kale walikuwa wakisherehekea sherehe za Chimbuko.”
(Hebrew Religion; S.P.C.K., London; 1955; Uk.128)
Inawezekana, katika zama za kale za matawi mawili ya nyumba ya Mtume Ibrahim a.s. walikuwa wakifuata taratibu za kupenyeza ziada ya mwezi mara 7 katika mzunguko wa miaka 19. Na hivyo mwezi wa 7 wa Kiyahudi, Tishri I, iliingiliana na Mwezi wa Muharram. Hivyo ‘Ashura ikatokezea mnamo tarehe 10 ya mwezi Kiyahudi Tishri I, Siku ya upatanisho wa Yesu Kristo kwa kufa kwake – siku ya kufunga saumu.
Katika makala hayo imeweza kuwa bayana kuwa kalenda zote mbili zimepoteza maingiliano yao pale Islam, katika maka wa 9 wa Hijriyyah, ilipopiga marufuku kuingiliana. Lakini kunapochunguzwa kiundani inaonekana kuwa umuhimu wake ulikuwa umeshapotea hata kabla ya kuja kwa Islam, kwa sababu Waarabu walikuwa hawakufuata mahisabu katika kuingiliana huko.
Na ndiyo kwa hivyo Mwezi Muharram wa mwaka wa 2 wa Hijriyyah ulianza mnamo tarehe 5 ya Mwezi wa Julai, mwaka 623 C.E. ( Al-Munjid, chapa ya 21 ), miezi mingi kabla ya mwezi wa Kiyahudi wa Tishri I ( mwezi ambao daima umekuwa ukiingiliana na miezi ya Septemba na Oktoba ).
Ni wazi kuwa ‘Ashura ya Muharram katika mwaka huo ( au, kwa jambo hilo, katika zama za uhai wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. huko Madina ) haikuwa na umuhimu wowote kwa Mayahudi.
Swali:
Sasa, je ni kwa nini walifunga saumu siku hiyo ?
2. Pili :
Maandishi ya Kiyahudi ya Midrash tarehe 10 ya mwezi wa 7 ( Yom Hakippurim – Siku ya Siku ya upatanisho wa Yesu Kristo kwa kufa kwake) kwa tukio la kuletwa kwa amri za Mungu kutokea Mlima Sinai, kama vile Dr. Mishael Maswari-Caspi alivyoandika katika barua yake, kama ilivyonukuliwa katika makala yangu yaliyotangulia, kutajwa hapo juu.
Swali :
Iwapo Mayahudi walikuwa wakitaka kudumisha maingiliano yaliyopotea zamani kabisa ya Tishri I na Muharram, kwa kuweka maanani ilikuwaje wao wakasahau kuleta Ahadith hii mbele ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ?
3. Tatu :
Mwezi ambao Mungu alipowaokoa Waisraili kutokana na Firaun, ulikuwa ni mwezi wa ‘Abib ( yaani Mwezi wa Rajab katika kalenda ya Kiislamu ), kama vile Biblia inavyosema :
“Utunze mwezi wa ‘Abib, ukamfanyie pasaka Bwana, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abib, alipokutoa Misri usiku.
(Kumbukumbu la Torati (Kum.), 16:1)
Swali :
Je itawezekanaje kwa Mayahudi kulihamisha tukio la ‘Abib
( ambalo kiasili linaingiliana na Mwezi wa Rajab ) kuingia katika mwezi wa Muharram, kwani ni kuipinga Tawrati yao kiwaziwazi ?
Mwishoni kuna jambo kwa Waislamu walizingatie na kulifikia :
Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alitumwa kuja humu duniani pamoja na Dini na Shariah ambayo ilikuwa ikibatilisha dini na shariah zote zilizokuwa zimemtangulia.
Je ilikuwaje yeye akaja kuiga utamaduni wa Kiyahudi ?
Hivyo inatuwia waziwazi kuwa Mayahudi hawakuwa na sababu yoyote ya kufunga saumu katika siku ya ‘Ashura ya mwezi wa Muharram katika nyakati hizo, kwani hayo ni uzushi mtupu uliobobekwa. Ni dhahiri kuwa, ilizuliwa na mwandishi na mwenyekuripoti kuwa mwezi Muharram ulitokea kuingiliana na mwezi wa Kiyahudi Tishri I; lakini hawakuwa wakijua kabisa kuhusu dini na utamaduni wa Kiyahudi.
Mtu anakuwa amebanwa kwa kuelezea hapa kuwa hadith kama hizi zilikuwa zimezuliwa na kambi ya wafuasi wa Bani Umayyah, baada ya kuuawa Shahidi kwa Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , ikiwa kama ndiyo kampeni zao za kuigeuza tarehe 10 ya Muharram iwe ndiyo siku ya kusherehekea.
Hadith hizi ndizo za aina ya zile zisemazo kuwa mnamo tarehe 10 ya Muharram
• Safina ya Mtume Nuh a.s. ilitua juu ya Mlima Arafat,
• Moto ulipooza kwa ajili ya usalama wa Mtume Ibrahim a.s.
• Mtume Isa a.s. alipaa kwenda mbinguni
Katika kikundi hiki hiki zikaja Hadith zikiwataka Waislamu kuichukulia ‘Ashura kama sherehe za kufurarisha, na kuhifadhi nafaka zao siku hiyo kwani itamwongezea mtu huyo riziki na baraka za Allah swt kwake yeye na wananyumba wake.