Imam Hussein AS alihuisha Uislamu
Katika historia ya jamii ya mwanaadamu maisha yamekuwa yakiendelea na kuandamana na matukio mbali mbali. Ni wazi kuwa baadhi ya matukio ya zama tofauti si tu kuwa hayawezi kufutika bali pia hubakia na kung'ara katika kursa za historia na kuteka fikra na mitazamo ya wengi.
Mnamo mwaka 61 Hijria Qamaria, historia ilishuhudia tukio muhimu ambalo licha ya kupita karne nyingi lakini bado ni ilhamu kwa matukio mengi ya kijamii na kisiasa.
Hapa tunakusudia Hamasa ya Imam Hussein AS katika ardhi ya Karbala. Hii ni hamasa ambayo imebakia katika zama na maeneo yote. Ni hamasa ambayo imevuka mipaka ya kijiografia na kihistoria na kuwa ilhamu na mfano wa kuigwa katika zama zote za jamii ya mwanadamu.
Tuko katika siku za awali za mwezi wa Muharram, kumbukumbu ya hamasa adhimu ya Karbala. Tunatoa salamu zetu kwa Hussein bin Ali AS. Salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Imamu huyo mkubwa ambaye alinawiri katika kilele cha karama na heshima ili aweze kumpa mwanadamau somo la maisha ambalo litabakia na kudumu milele. Salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Imam Hussein AS na wafuasi wake watiifu, ambao walitoa maisha yao muhanga kwa ajili ya kuinua Uislamu.
Imam Hussein AS alianzisha harakati yake takatifu wakati ambao utamaduni na mafundisho asili ya Kiislamu yalikuwa katika hatari ya kupotoshwa.
Imam Hussein AS alikuwa akishuhudia namna malengo na mafundisho ya Mtume Muhammad SAW yalivyokuwa yakisahauliwa hatua kwa hatua huku Bani Ummaya wakiwatawala watu kwa mabavu na hadaa.
Kutokana na kuwa moja ya majukumu muhimu ya uongozi katika Uislamu ni kuuongoza umma katika njia ya haki, Imam Hussein AS aliamua kuwa ni jukumu lake kusimama na kupambana dhidi ya upotofu uliokuwepo katika zama zake. Ni kwa sababu hii ndio mtukufu huyo alisema: "Mfahamu kuwa hawa (Bani Ummaya) wako pamoja na shetani, wameacha kutii amri za Allah na wanaeneza ufisadi wazi wazi. Wamekiuka mipaka ya Allah na kupora mali ya umma na kuifanya kuwa yao. Wameyafanya yaliyoharamishwa na Allah kuwa halali na kuhalalisha yaliyoharamishwa na Allah."
Kwa kuzingatia hotuba hii tunaweza kufahamu kuwa msingi mkuu wa harakati ya Imam Hussein AS ulikuwa ni kuhuisha na kuimarisha thamani za kidini katika jamii. Mtukufu huyo alisema hivi kuhusu sababu ya mapambano yake dhidi ya hali mbaya iliyokuwepo:
"Ewe Allah! Wewe unajua kuwa kile ambacho tunakisema si kwa ajili ya kuwania utawala na wala si kwa ajili ya kuipenda dunia bali ni kwa ajili ya kuiona dini yako ikiwa imesimama na kuleta marekebisho katika ardhi zako na kuwasaidia waja wako waliodhulumiwa ili majukumu na hukumu za kidini ziweze kutekelezwa."
Maneno haya ya Imam Hussein AS yanaashiria kuporomoka umaanawi katika jamii ya Kiislamu ya zama hizo. Katika upande mwingine, kitendo cha watawala kupora mali na kueneza bidaa na khurafat sambamba na kusahauliwa Masahaba wa Mtume SAW na kutengwa Ahlul Bait wa mtukufu huyo, yote hayo yalikuwa yameandaa mazingira ya kurejea jamii katika zama za ujahiliya. Katika wakati wa utawala wa Bani Ummaya, ukabila na kujifakharisha kwa msingi wa rangi au kaumu, mambo ambayo yalipingwa vikali na Mtume, yalianza kuibuka tena katika jamii.
Tafsiri potofu kuhusu dini, kuibuliwa hadithi bandia na kuenezwa habari za uongo ni mambo ambayo yalipelekea watu kuwa na shaka kuhusu thamani halisi za kidini na hivyo kuwachanganya kuhusu muongozo sahihi.
Bani Ummaya kwa kueneza hadithi bandia kutoka kwa Mtume SAW na Masahaba zake walijiarifisha kuwa warithi wa Mtume.
Katika upande mwingine, tabia ya Bani Umayya ya kuhodhi kila kitu na kujitakia makuu ni mambo ambayo yalipelekea kuwepo ukosefu mkubwa wa usawa katika muundo wa kiuchumi katika jamii. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba pote la wachache waliokuwa wakitawala na wapambe wao walitumia fedha za umma au baitul mal kujitajirisha na kuishi maisha ya raha mstarehe huku wananchi waliowengi wakiishi katika mbano mkubwa wa kiuchumi. Hali hii mbya pamoja na upotofu wa kiitikadi na kijamii ulifika kileleni wakati wa utawala wa Yazid bin Muawiyya.
Mashinikizo na hitilafu za kisiasa katika zama za ukhalifa wa Bani Ummaya zilipelekea kuibuka hofu na wasiwasi katika umma kiasi kwamba watu hawakuthubutu kutetea haki zao.
Aghalabu ya watu mashuhuri katika jamii na wasomi wakubwa wa kidini walinyamaza kimya kwa kuhofia ukandamizaji na udhalimu wa Bani Umayya na hata walitoa wito kwa Imam Hussein AS asalimu amri kwa hali hiyo. Kidhahiri watu wote walikuwa wakiswali, kufunga na kuenda hija lakini swali linaloiibuka ni hili kuwa je, amali na ibada zao zilikuwa na athari na natija iliyokusudiwa maishani?
Ni kwa nini Waislamu wa zama hizo walionyesha kutojali kuhusu matukio ya kijamii na kisiasa katika mazingira hayo?
Kwa sentensi moja tunaweza kusema kuwa kulikuwa na ufa baina yao na uhakika wa dini. Ujahili na kutofahamu masuala ya kisiasa na kijamii kulizusha matatizo katika upambanuzi baina ya haki na batili, na wala hawakujua waelekee wapi.
Kufuata dunia na kusahau umaanawi ni jambo ambalo liliwashughulisha zaidi watu kuliko suala jingine lolote. Kuhusu hili, Imam Hussein AS alisema: "Mnaona namna ahadi ya Mwenyezi Mungu inavyovunjwa, lakini hamsemi chochote na wala haiwaingii hofu. Katika hali ambayo mnapiga mayowe pale baadhi ya ahadi za baba zenu zinapovunjwa, lakini hamlipi umuhimu suala la kupuuzwa ahadi za Rasulullah SAW." Tuhaf Al Uqul Uk. 237
Katika hali hii ya kusikitisha ni kipi kingeweza kufanyika ili kuinusuru dini kutoka kwenye makucha ya madhalimu?
Imam Hussein AS aliposhuhudia hali hii, alichukua hatua za kuzuia kuporomoka umma kifikra na aliamini kuwa si tu katika masuala ya kiitikadi na kimaanawi, bali pia katika masuala ya kijamii na kisiasa kulihitajika marekebisho na mabadiliko ya kina na kimsingi katika jamii. Labda kama Imam angechukua hatua ya harakati ya kiakhlaqi na kiutamaduni tu, hangefanikiwa kuufahamisha umma kile kilichokuwa kikiusibu.
Kwa hivyo ili kuiondoa dini katika tatizo hili kubwa, hatua ya awali ilikuwa ni kutoutambua rasmi utawala wa Yazid na pili kujitoa muhanga kwa ajili ya mapambano haya yenye kuainisha hatima.
Imam Hussein AS aliwasilisha mpango sahihi wa mfumo wa Mwenyezi Mungu uliojengeka juu ya msingi wa kumtii imamu muadilifu na kulaani tabia za mtawala dhalimu. Imam alibainisha nadharia ya kimantiki ya dini ya Kiislamu kwa kutegemea kauli ya Rasulullah SAW kwa kusema: "Kila ambaye anamuona mtawala dhalimu anaharamisha aliyohalalisha Allah na kunyamaza kimya na kutoonyesha radiamali yoyote, basi Mwenyezi Mungu atamhukumu." Tuhaf Al Uqul Uk. 505
Maneno haya ya Imam ni nembo ya hati ya kiitikadi na kifikra ya umma. Lakini ubabe wa kisiasa na kiutamaduni wa Bani Ummaya ni jambo ambalo lilipelekea ujumbe huu usienee miongoni mwa Waislamu na kizuizi hiki kilikuwa chanzo cha ujahili na kutotambua mambo watu na hivyo kuandalia Bani Umayya mazingira ya kuukandamiza zaidi Umma wa Kiislamu.
Imam Hussein AS alifahamu ukweli kuwa madhalimu waliweza kuwatawala Waislamu kwa kudai kuwa wanafuata dini. Madhalimu hao walijitahidi kutumia mbinu mpya kuhuisha Ujahiliya uliokuwepo kabla ya Uislamu. Walihalalisha yaliyokuwa yameharamishwa na Allah na kuharamisha aliyoyahalalisha. Ni kwa sababu hii ndio wakati Imam Hussein AS alipobainisha lengo la mwamko wake wa kukabiliana na Yazid alisema hivi:
'Mimi nimejitokeza kwa ajili ya kuurekebisha umma wa babu yangu. Ninataka kuamurisha mema na kukataza mabaya na kuenda kwa mujibu wa Seerah na Sunna ya babu yangu, Rasulullah SAW.'
Imam katika falsafa ya harakati yake alibainisha suala la kurekebisha umma na kuhuisha Seerah ya Rasullah SAW. Kimsingi aliwataka watu watambue kuwa mushkili katika Umma wa Kiislamu ulitokana na wao kujiweka mbali na Sunna ya Mtume SAW. Imam Hussein AS alifahamu kuwa upotofu uliokuwepo ulikuwa unahatarisha fikra za Kiislamu na iwapo hali hiyo ingeruhusiwa kuendelea basi sehemu kubwa ya mafundisho halisi ya kidini yangetengwa na kile ambacho kingebakia katika Uislamu ni dhahiri tu pasina kuwepo na chochote cha maana. Baada ya kubainika ufisadi na upinzani wa wazi wa Yazid dhidi ya mafundisho ya kidini, haikujuzu tena kunyamaza kimya. Hii ni kwa sababu yamkini kimya kingepelekea kupotoea yale yote yaliyoletwa na Mtume SAW. Kimsingi harakati ya Imam Hussein AS ilikuwa onyo kwa umma wa Kiislamu. Onyo kwa zama zote za historia na kwa hivyo tokea wakati huo, harakati ya mtukufu huyo imekuwa ni ilhamu kwa wanaharakati wote wa Kiislamu. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa chanzo kikuu cha harakati ya Imam Hussein AS ilikuwa ni kujaribu kuonyesha Uislamu wa kweli katika jamii iliyokuwa imepotea wakati huo. Ni kwa sababu hii ndio katika kutathmini mapambano ya Imam Hussein AS, tukasema kuwa mtukufu huyo alihuisha tena Uislamu