Change Language: English

IMAM HUSEIN (AS) NA HARAKATI ZAKE ZA AMANI

"Enyi mlioamini! Ingieni katika usalama nyote, wala msifuate nyayo za Shetani. Kwa hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi." (Surat al-Baqarah: 208).

Utamaduni wa Amani na Utamaduni wa Mabavu:

Mwanadamu kwa kuzingatia kuwa ni mwanajamii, huishi ndani ya mazingira ya jamii ambayo humlea na katika utamaduni unaomzunguka, na hivyo mambo mawili hayo hutoa mwelekeo wa nafsi yake na huathiri katika mwenendo wake. Kama atakulia katika jamii inayotawaliwa na huruma, upendo na mshikamano, hakika hali hiyo humwandaa kisaikolojia ili afuate njia ya amani, upendo na muamala sahihi katika maisha. Ama akikulia katika mazingira ya ubabe na ukatili, au ikiwa utamaduni uliotawala katika jamii yake ni utamaduni unaoshajiisha mabavu na ukatili, bila shaka jamii hii itatengeneza watu waasi, makatili na wababe. Na kwa sababu hiyo ndio maana Uislamu unahimiza kuandaa mazingira ya kijamii yanayozungukwa na huruma na upendo. Wazazi wawahamasishe watoto kuwa na tabia ya upole na upendo, imepokewa katika hadithi kwamba busu la baba kwa mtoto wake lina malipo, katika hadithi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) amesema: "Mwenye kumbusu mtoto wake Mwenyezi Mungu anamwandikia jema. Na pia imepokewa kutoka kwake (saww) kuwa: "Zidisheni kuwabusu watoto wenu, hakika mnayo katika kila busu daraja katika pepo. " Na katika riwaya nyingine ni kwamba mtu mmoja alimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu(saww) amemkalisha Hasan na Husein katika mapaja yake,na alikuwa anambusu huyu na kisha anambusu mwingine, yule mtu akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nina watoto kumi na sijambusu hata mmoja kati yao.” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) akasema: “Mimi sina chochote kwako, kama Mwenyezi Mungu ameondoa huruma moyoni mwako. " Na katika kitabu Wasailus-Shia kuna hadithi kwamba Mtume alisema: "Asiyehurumia hatahurumiwa."

Hivyo inapasa mtoto aishi katika mazingira ya upendo na upole tangu utotoni mwake. Na Uislamu unaamuru wanajamii wote wawahurumie watoto, na hii ni katika adabu ya Kiislamu na ni katika maelekezo yake matukufu kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww): "Waheshimuni wakubwa wenu na wahurumieni wadogo wenu. "Hakika Uislamu unamtaka mwanadamu aishi katika jamii inayotawaliwa na huruma, na sio tu ndani ya familia bali katika jamii nzima,na kwa hiyo malezi haya yataakisi katika silka yake, na utamuona anamheshimu huyu na anamhurumia yule, anaunga udugu wa jamaa zake na wala hawaudhi jirani zake.

Na katika Uislamu kuna mafunzo maalum kwa ajili ya kumtendea yatima, kwa sababu amemkosa mmoja kati ya wazazi wake au wote wawili, kwa kuzingatia kuwa wazazi ni upande ambao unampa yeye upole na huruma, na kwa sababu hiyo Uislamu unaamuru yatima atendewe muamala maalumu ili yatima huyu aleleke katika mazingira ya huruma ya Kiislamu, anasema (swt):

"Ama yatima usimwonee!" (Surat Dhuhaa: 9).

Kama mwanadamu ataleleka katika mazingira ya mabavu ya kibabe na kikatili, hakuna yeyote anayemjali au kumhurumia, mwanadamu huyu hawezi kutarajia isipokuwa njia ileile aliyoishi utotoni mwake. Anaweza kuwa na hisia ya kulipiza kisasi kwa jamii na mazingira yanayomzunguka, na ataamiliana kwa moyo mgumu na wa ubabe. Na kwa sababu hii utaukuta Uislamu unatahadharisha uwepo wa hali ya ufakiri, kuhitajia na dhulma katika jamii, hiyo ni kutokana na yale yanayozalishwa na mazingira hayaikiwa ni pamoja navisasi vibaya dhidi ya jamii, na kwa ajili hiyo imepokewa katika hadithi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) kuwa amesema: “Ufakiri unakaribia kuwa ni ukafiri. " Kama ambavyo Abu Dhar al-Ghiffari ana neno zuri katika hilo, anasema: "Pindi ufakiri unapokwenda katika mji ukafiri huuambia nichukue na mimi pamoja nawe."