Change Language: English

Dhihirisho la mapenzi na ibada ya Mwenyezi Mungu

Katika suala zima la mapambano ya Husain bin Ali AS dhidi ya dhulma na ukandamizaji, Ashura ni mithili ya jabali kubwa ambalo limeenea na kufunika nyika zote. Mapambano ya Imam Husain AS ni utamaduni ambao chimbuko lake ni Uislamu asili. Mapambano hayo yalitoa mchango mkubwa mno wa kuibakisha hai dini tukufu ya Kiislamu. Hamasa ya mwezi 10 Muharram mwaka 61 Hijria iliyotokea kwenye jangwa la Karbala katika Iraq ya hivi sasa, ni mwenge wa kuwaongoza kuwaongoza kwenye njia sahihi, wapigania haki.
Imam Husain AS ni mjukuu mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye ndani ya shakhsia yake, zimekusanyika khulka zote bora zilizojaa baraka. Mtukufu huyo hakuwa mtu mmoja, bali alikuwa ni mtu mwenye upana na ukubwa wa historia. Akipata ilhamu kutoka katika aya za Qur'ani Tukufu na sira ya babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, Imam Husain AS alileta tabasuri na hamasa ya hali ya juu katika uma wa Kiislamu na harakati yake ikawa ni kigezo na rasilimali ya mwamko na mapinduzi makubwa duniani. Husain AS amefundisha kwamba woga na kupenda sifa, kujipendekeza na kujidhalilisha mbele ya wageni yote hayo yanatokana na mtu kujiweka mbali na maumbile yake ya dhati na ya asili.
Kwenye mapambano yasiyo na nguvu sawa ya siku ya Ashura, Imam Husain na wafuasi wake watiifu walipambana na jeshi kubwa la Yazid bin Muawiya lililokuwa limejizatiti vibaya sana kwa silaha na Imam akaligeuza jangwa la Karbla kuwa medani ya ukombozi wa kudhihiri mapenzi ya kweli. Watu watukufu waliojenga historia huko Karbala walikuwa ni wanawake na wanaume ambao walistahabu kufa kwenye dimbwi la damu na kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu kulikoni kuishi kwa madhila. Walifanya hivyo ili kuutakasa msamiati wa maneno ya ukombizi na uhuru katika historia na kuupa msamiati huo, heshima na uhai unayostahiki katika kipindi chote cha taarikh.
Ashura imechora muongozo na dira ya mapenzi ya kweli na kujitolea muhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Imam Khomeini (quddisa sirruh), kadiri Imam Husain AS alivyokuwa akikaribia kwenye kuuawa shahidi na kumwaga damu yake tukufu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu katika siku ya Ashura, ndivyo sura yake ya kweli iliyojaa mvuto wa kipekee, ilivyozidi kudhihirika. Vijana waliokuwa pamoja na Imam Husain AS wakati huo, walikuwa wakishindana ili kila mmoja awe wa kwanza kufa shahidi kabla ya Imam wao mtukufu. Sekunde hizo zilichora sura ya kipekee ya kimaanawi iliyotoa dhihirisho bora kabisa la utiifu na kujitolea katika njia ya haki. Lililokuwa muhimu kwa vijana hao watukufu lilikuwa ni kutekeleza wajibu na majukumu yao na kuunawirisha mmea mtukufu wa Uislamu kwa damu zao.
Imam Husain alikuwa na wafuasi wachache tu katika jangwa la Karbala. Lakini wafuasi wake hao walikuwa mashujaa, wenye imani thabiti, kama ambavyo walikuwa ni wanafikra na urafaa wakubwa. Imani ya watu hao watukufu ilikuwa thabiti kiasi kwamba haikuacha nafasi yoyote ya woga wala cheche za hofu katika nyoyo zao. Mapenzi ndiyo yaliyofunika kila kitu katika nyoyo hizo. Miongoni mwa watu hao watukufu alikuwa ni Hajjaj Ibn Masruq al-Ju'fi. Hajjaj alikuwa ni mwadhini wa Imam Husain AS katika safari yote ya kuelekea Karbla ambapo mwangwi wa takbiri yake, uliziliwaza na kuzipa utulivu maalumu nyoyo za wafuasi wa Imam Husain AS. Siku ya Ashura alikwenda kwa heshima zote mbele ya Imam Husain AS na kuomba ruhusa ya kwenda kwenye medani ya mapambano. Aliporuhusiwa alielekea kwenye medani hiyo na kuonyesha ushujaa wa ajabu katika mapambano. Baadaye alirejea kwa Imam huku mwili wake wote ukiwa umejaa damu. Akasimama mbele ya Imam Husain AS na kusema: Imam wangu mpenzi, roho yangu iwe fidia kwako. Leo nitaonana na babu yako Mtume wa Mwenyezi Mungu. Leo nitaonana na baba yako Ali. Seyyidi yangu! Je nimeweza kukuridhisha? Imam akamwangalia Hajjaj kwa yale mapenzi yake na huruma zake nyingi tukufu na kumwambia, Naam, ndivyo ilivyo. Mimi nami nitaonana nao baada yako. Hajjaj akarejea tena kwenye medani ya mapambano, akapambana tena kwa ushujaa mkubwa hadi alipouawa shahidi.
Mirengo miwili ya haki na batili imekuwa ikipambana katika kipindi chote cha historia. Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu, ndio walinganiaji wa haki na tawhidi ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Watukufu hao walikuwa wanalihesabu suala la kumtambua na kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja kuwa ndiyo siri ya uongofu na ukamilifu. Roho ya tawhidi na kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja ilijidhihirisha kwa uwazi kabisa katika mapambano ya Ashura. Katika hotuba yake muhimu, Imam Husain AS aliashiria kupotoka na kutoka jamii ya Kiislamu katika njia ya haki na kusema: "Je, hamuoni kwamba mumeacha kumtii Mwenyezi Mungu, mumekengeuka haki na hamuachani na batili?"
Mapambano ya Imam Husain AS yalikuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kamwe hayakufanyika kwa malengo ya kidunia. Imam Husain AS aliwahutubia watu akisema: "Nyinyi mnajua vyema kwamba kundi hili (Yazid na jeshi lake) limekuwa tiifu kwa shetani na limeasi amri ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema. Kundi la watu hao limejitumbukiza katika shimo la ufisadi na limevuuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Watu wa kundi hilo wamehodhi Baytul Maal kwa manufaa yao binafsi na wanayafanya halali yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu. Mimi ndiye mwenye haki zaidi ya kupambana na watu hawa kuliko mtu mwingine yeyote."
Imam Husain alichukua hatua mbalimbali za kuleta marekebisho katika umma wa Kiislamu. Alifanya hivyo hatua kwa hatua na wakati alipoona kwamba mazungumzo hayasaidii tena aliona hakubakiwa na njia nyingine isipokuwa mbili tu, ima kuulinda Uislamu au kulinda nafsi na roho yake. Njia iliyochaguliwa na mtukufu huyo ilikuwa ni kuulinda Uislamu kwa gharama yoyote ile. Mtukufu huyo alinukuu miongozo mitukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kuwaambia watu kwamba: "Yeyote kati yenu ambaye atamuona mtawala ni dikteta na katili... akamuona anapinga sunna za Mwenyezi Mungu, na anaamiliana na waja wa Mwenyezi Mungu kwa uhalifu na uadui, na asimpinge mtawala huyo wala kumzuia kwa maneno na vitendo vyake, basi haki ya mtu huyo ni Mwenyezi Mungu kumuingiza katika sehemu ile ile atakayoingia mtawala huyo dhalimu."
Ashura ni chuo cha uaminifu na kuheshimu kikamilifu ahadi na makubaliano. Katika usiku wa Ashura, Imam Husain AS Aliwataka wafuasi wake watukufu watumie kiza cha usiku ili waokoe nafsi zao kwani kundi la maadui lilikuwa linataka roho ya Imam si roho zao. Lakini ikhlasi ya kweli iliwafanya watu hao watukufu waseme kwa sauti moja kwamba hata kama watauawa mamia ya mara na kukatwa vipande vipande na baadaye kufufuka na kuuawa tena hivyo hivyo, hawako tayari kumwacha peke yake mwana huyo ya Mtume na Kiongozi wao huyo mtukufu. Hii ndiyo ikhalisi ya kweli. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.