Change Language: English

Bustani ya Uongofu

Hapana shaka kuwa mtaweza kunufaika vya kutosha na mfululizo huu kwani Mtume SAW, dhuria na watu watoharifu wa nyumba yake ni bustani iliyojaa manukato ya maarifa yasiyo na kifani; na bila shaka kuvuta pumzi katika bustani hii humfanya mtu apate nishati na nguvu mpya sambamba na maarifa mapya yenye maana na madhumuni aali. Tunamuomba Allah atupe tawfiki, msaada na auni ili tuweze kubainisha mitazamo na maarifa haya ya Mtume SAW na Ahlul Bayt wake wema kwa njia bora kabisa. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami katika dakika hizi chache katika sehemu hii ya kwanza ya mfululizo huu. Karibuni.

Imani na masuala ya kiitikadi ni mambo ambayo yana umuhimu mkubwa katika maisha ya mwanaadamu. Hii inatokana na kuwa, fikra na mitazamo ni jiwe la msingi la shakhsia ya mtu; na vitendo, amali na miamala yote ya mwanadamu huafanyika kwa mujibu wa imani na itikadi zake. Fikra za mwanaadamu huwa na taathira katika engo na nyuga zote za maisha.

Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, akthari ya miamala isiyofaa, tabia mbaya na maadili machafu, chimbuko lake ni itikladi zisizo sahihi na vile vile kutokuwa na ufahamu mwanaadamu kuhusiana na misingi ya utu na ubinaadamu. Kwa msingi huo lengo kuu la dini za Mwenyezi Mungu ukiwemo Uislamu, lilikuwa ni kuleta mabadiliko katika itikadi na fikra za mwanaadamu. Mwanzoni wakati Bwana Mtume saw anaanza da'wa na kazi yake ya kuwalingania watu dini alisema kuwa, njia ya wokovu ni kuwa katika kivuli cha Tawhidi na kutanguliza mbele fikra za Kitawhidi. Hivyo alikuwa akiwaambia watu:

"قولوا لا اله الا الله تفلحوا"

"Semeni, Hapana Mola, apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, ili mpate kufaulu."

Kwa maana kwamba, Enyi watu! Ondoeni katika fikra zenu mitazamo na fikra batili ambazo zimeingiwa na shirki, ili kwa njia hiyo muweze kudhihirikiwa na mielekeo ya wazi ya wokovu, saada na ufanisi. Mwenyezi Mungu SWT alimfanya Mtume Muhammad SAW kuwa Mtume wa Mwisho na akaifanya Qur'ani Tukufu kuwa nuru ya hidaya na uongofu na akayafanya mambo hayo kuwa ratiba na mipango bora kabisa kwa ajili ya saada ya mwanaadamu humu duniani na kesho akhera.

Hivyo basi, Uislamu ulikuwa zawadi na hiba ya mwisho yenye thamani kubwa ya Mwenyezi Mungu ambayo alimpatia Mtume SAW ili awaletee wanaadamu. Mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu akipata msaada wa maarifa asili na hakika ya Uislamu, alifanikiwa kwa muda mfupi tu kuijenga kimaadili jamii ambayo ilikuwa imenasa katika dimbwi cha ujahilia na taasubi zisizo na kikomo. Hatua muhimu kabisa zilizochukuliwa na Bwana Mtume SAW zilikuwa ni kuimarisha misingi na nguzo za kifikra na kimuamala katika kivuli cha mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Katika kipindi cha miaka 23, Allah SWT aliteremsha sheria na kanuni anazohitajia mwanaadamu katika fremu ya aya Tukufu za Qur'ani; na Bwana Mtume SAW aliwafikishia watu bila ya kuzifanyia mabadiliko. Kando ya misingi na mafundisho hayo, muamala na maneno ya Bwana Mtume SAW yalikuwa ni ubainishaji na kamilisho la mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Licha ya kuweko upinzani, uadui na ukwamishaji mambo uliokuwa ukifanywa na watu majahili, maktaba ya Kiislamu iliweza kusonga mbele katika njia yake ya saada na ukamilifu, na kupata wafuasi wakweli na wenye ikhlasi. Katika kipindi hicho, kuna baadhi ya watu waliingia katika Uislamu na kuikubali dini hii kidhahiri ili waweze kunufaika na baadhi ya mambo. Lakini katika batini yao walikuwa na chuki, uhasama na uadui mkubwa na Uislamu katika nyoyo zao; na walikuwa wakisubiri ipatikane fursa tu ili wadhihirishe uadui wao. Hii ni hatari ambayo ilikuwa ikiikabili dini tukufu ya Kiislamu. Hata hivyo, tadbiri na mipango ya Mtume SAW kwa ajili ya kulinda dini hii ya mwisho ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ipi?

Katika kipindi cha uhai wake, Bwana Mtume SAW sambamba kufanya kila awezalo kueneza mafundisho ya Kiislamu, alivumilia na kustahamili, taabu, mashaka, maudhi na matatizo mengi kwa ajili ya kulinda mafundisho sahihi ya Uislamu na kuzuia upotofu wa kifikra na kivitendo; huku akisimama na kutoa miongozo ya lazima. Aidha katika kipindi cha uhai wake alitumia minasaba mbalimbali kuwaenzi Ahlul Bayt wake watoharifu AS na kuonyesha umuhimu walionao dhuria wake hao wema.

Wakati aya ya 33 ya Suratul Ahzab isemayo, "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi watu wa nyumba (ya Mtume), na (anataka) kukutakaseni kabisa kabisa" iliposhuka; katika kutoa ufafanunuzi wa aya hiyo Bwana Mtume SAW alisema kwamba: " Kwa hakika mimi na Ahlul Bayt wangu ni wasafi na hatuna uchafu wa madhambi."

Tangu awali yaani mwanzoni mwa risala yake Bwana Mtume SAW alikuwa akifahamu juu ya uwezekano wa kujitokeza hitilafu baina ya umati wake. Moja kati ya mipango na tadbiri zake za kuzuia hili, alifanya hima kubwa ya kuwatambulisha Ahlul Bayt AS pamoja na daraja yao ya juu baina ya Waislamu. Ni kwa muktadha huo ndio maana tunapata kuna hadithi nyingi mno za Bwana Mtume SAW zinazowazungumzia Ahlul Bayt wake watoharifu pamoja na daraja yao kubwa walionao. Miongoni mwa hadithi mashuhuri kabisa na ambayo inapatikana pia katika vitabu mashuhuri wa Waislamu wa Kisuni ni Hadith Al- Thaqalein yaani Hadithi ya Vizito Viwili. Bwana Mtume SAW anasema katika hadithi hiyo kwamba:

Hakika mimi nimekuachieni vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na dhuria na Ahlul Bayt wangu na viwili hivi kamwe havitotengana hadi vitakaponijia kwenye hodhi".

Ibn Hajar Al asqalani anasema kuhusiana na hadithi hii: "Tambua kwamba, hadithi hii imenukuliwa kwa njia tofauti na masahaba zaidi ya ishirini na wakaibaibnisha kwa njia tofauti. Kukaririwa riwaya na hadithi hii katika vitabu mbalimbali ni ishara ya mazingatio maalumu na msisitizo mkubwa wa Bwana Mtume SAW kwa Kitabu cha Qur'ani na Ahlul Bayt AS wake watoharifu."

Katika hadithi hii tukufu ya Thaqalein (vizito Viwili) kuna madhumuni aali, maana na siri kubwa. Kuwekwa Ahlul Bayt AS pamoja na Qur'ani katika hadithi hii ya Bwana Mtume SAW kuna maana ya kuwa, shakhsia hawa wakubwa wana udiriki na ufahamu mkubwa wa maana na mafahimu ya Qur'ani Tukufu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kushikamana na Qur'ani na Ahlul Bayt wa Mtume kwa pamoja, ni kinga na ngao ya kutopotea na kukengeuka watu. Kwani Ahlul Bayt AS ndio watekelezaji, wafasiri na wajuzi zaidi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Nukta nyingine muhimu na ya kuzingatiwa ni hii kwamba, kutotengana Qur'ani Tukufu na Ahlul Bayt AS ni ishara na ithbati ya kubakia na kudumu Uislamu asili na Sunna za Mtume SAW kupitia sira na mwenendo wa dhuria hawa watoharifu wa Mtukufu Mtume SAW.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya kwanza ya mfululizo wa kipindi hiki cha Bustani ya Uongofu inakomea hapa kwa leo; nina matumaini kwamba, mumenufaika vya kutosha. Ninakuageni nikiwa na matarajio ya kukutana nanyi juma lijalo Inshallah katika sehemu nyingine ya kipindi hiki. Wahadha Salaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.