Bani Hashim Na Bani Umayyah
Habari zinaeleza kwamba wakati Hashim na Abd Shams, baba wa Umayyah walipozaliwa kama mapacha, kidole cha mmoja wao kilikutwa kimenasa kwenye paji la uso la mwingine. Kilikatwa ili kuwatenganisha vichanga hao, na damu ambayo ilitiririka kutoka kwenye jeraha ilichukuliwa kuonyesha ishara ya ndege mbaya ya kumwaga damu kati ya vizazi vyao.1
Umayyah alianza kusababisha nia mbaya kati yake na ami yake, Hashim. Kichocheo kikubwa cha wivu wake kilipatikana katika kipindi cha njaa ambayo iliipiga Makka, Hashim alipata kukubalika sana kwa umma kwa kule kuwagawia wakazi wa mji chakula kingi ambacho kilikuwa katika namna ya vipande vya mikate iliyovunjwa vunjwa na kuchovyekwa katika supu.
Umayyah akatafuta kwenda sambamba na ukarimu huu kwa kujitia kufanya vitendo vya ukarimu ambao hauna maana na mara baada ya muda mfupi wa kutosha uligunduliwa nia yake isiyo nzuri. Katika hali ya mfadhaiko, Ummayah alileta changamoto kwa Hashim la kushindania madai yake ya ubora mbele ya msuluhishi huru anayekubalika. Moja ya masharti lilikuwa kwamba upande utakaoshindwa utahamishwa kutoka Makka kwa kipindi cha miaka 10. Msuluhishi huyo aliamua dhidi ya Umayyah ambaye alihamia Sham (Syria) kwa miaka 10. Hivyo ukatokea uadui kati ya Bani Hashim na Bani Ummayah na uliendelea kuwepo kati yao kwa vizazi vingi.2
Kuzaliwa kwa Mtume miongoni mwa Bani Hashim lilikuwa pigo lililovunjavunja heshima ya Bani Umayyah. Kwa hiyo, wao waliutazama utume wa Muhammed kama ushindi wa Bani Hashim na walimfanyia upinzani mkali mno.