Change Language: English

Arubaini, Safari ya Nyoyo za Maashiki (1)

Kwa kawaida safari ya kutembea kwa miguu kutoka mji wa Najaf al Ashraf kuelea Karbala inayofanywa kila mwaka na maashiki na wapenzi wa mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) huambatana na vuguvugu na msisimko wa aina yake. Mwanzoni mwa safari hiyo mazuwari huanza safari hiyo ya mahaba na upendo katika mji wa Najaf wakiwa na shanta dogo, viatu vyepesi na masurufu kiduchu ya kutumia njiani.

Huacha nyuma yao vitu vyao vya kimaada na vya kidunia kama mavazi ya fakhari, vito na kadhalika na kuanza safari hiyo kwa kutumia miguu ya nyoyo na roho zao. Fikra na nyoyo zao huwa na hamu kubwa ya kufika kwenye Haram, na mikono yao huwa na kiu ya ajabu ya kugusa kaburi la mtukufu huo. Sumaku na mvuto huo wa pendo kwa miaka mingi sasa umekuwa ukiwavuta watu wengi wanaoamua kuelekea Karbala kwa miguu ili asaa wakakutana na habibu na kipenzi chao, Hussein (as).

Minara ya Haram ya Imam Hussein (as), Karbala

Kusafiri kwa miguu kwa ajili ya kwenda kuzuru kaburi la Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) huko Karbala katika siku ya Arubaini tangu siku ya tarehe 10 Muharram alipouliwa shahidi, kuna asili katika historia ya Uislamu. Mwaka 61 Hijria swahaba mkubwa wa Mtume (saw), Jabir bin Abdillah al Ansari akiwa pamoja na ghulamu wake, Atiyya, aliondoka Madina kwa miguu na asubuhi ya siku ya arubaini ya kwanza baada ya kuuliwa shahidi mjukuu huyo wa Mtume, aliwasili Karbala na kuzuru kaburi la Bwana wa Mashahidi.

Kwa mujibu wa nukuu za vitabu vya historia, kuzuru kaburi la Imam Hussein (as) na wafuasi wake huko Karbala katika miaka ya baada ya kuuliwa shahidi mtukufu huyo kulikuwa kukizusha vuguvugu na harakati kubwa za mapinduzi na kuwafichua madhalimu na watawala maovu wa kizazi cha Banii Umayyah, kiasi kwamba, watawala hao hawakuwa na njia nyingine ya kusitisha misafara ya mazuwari na waumini waliokuwa wakienda kuzuru kaburi la mjukuu huyo wa Mtume (saw) na kupata ilhamu ya jinsi ya kupambana na madhalimu ghairi ya kuwashambulia na kupiga marufuku ziara hizo. Hata hivyo mapenzi ya Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume hususan Imam Hussein (as) linaloteka nyoyo za waumimi na uhamasishaji wa Maimamu Baqir na Swadiq (as) viliwafanya Shia na wapenzi wa mtukufu huyo kutumia giza la usiku na njia za hatari kubwa kwenda kuzuru kipenzi na mahabubu wao, na katika safari hiyo baadhi yao walikumbana na mateso kutoka kwa watawala wa Banii Umayyah, masaibu makubwa na pengine adhabu ya kifo. Baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Banii Umayyah watawala wa kizazi cha Banii Abbas hawakuwa na njia nyingine ya kuzuia Waislamu kuzuru kaburi la Imam Hussein (as) isipokuwa kuharibu na kufuta kabisa athari za kaburi la Haram ya mtukufu huyo. Watawala hao walisahau au kujisahaulisha maneno ya Mtume Muhammad (saw) ambaye ametutaka kumpenda Hussein akisema: Hussein ni kutokana na mimi, na mimi ninatokana na Hussein, Mwenyezi Mungu ampende anayempenda Hussein".

پذیرایی در مسیر

Licha ya mashaka, dhulma na ukatili wote huo ambao uliendelea hadi mwishoni mwa utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, maashiki na wapenzi wa Hussein (as) wanaendelea kuzuru kaburi na Haram ya Bwana wa Mashahidi na kuwa mithili ya vipepeo wanaozunguka ua la waridi. Ukatili, mateso na mauaji ya watu waliokuwa wakizuru kaburi la Imam Hussein havikuweza kukata uhusiano wa kiroho na kimaanawi baina ya waumini na Imam kipenzi chao, na Waislamu wameendelea kushikamana na sira ya babu wa Hussein, Mtume Muhammad (as) ambaye alimpenda Hussein na kuwataka Waislamu wampende Hussein.

Kutokana na wito huo wa Mtume, kwa sasa matembezi ya Siku ya Arubaini baada ya mauaji ya tarehe 10 Muharram, yanahesabiwa kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu duniani. Katika mkusanyiko huo adhimu utawaona watoto wadogo wanaonyonya, vijana na barobaro, watu wazima na hata wazee na ajuza wanaojikongoja na kustahamili mashaka ya safari kwenda kuzuru kipenzi na mahabubu wao. Katika safari hiyo ya miguu kutoka Najaf hadi Karbala kuna milingoti inayowaongoza mazuwari na kuwafahamisha ni masafa ya kiwango gani yaliyosalia hadi kufika Karbala. Kila unapuvuka mlingoti mmoja, shauku na hamu kubwa ya kukutana na kipenzi Hussein hutokota na kucharuka zaidi na zaidi.

Mbali na milingoti hiyo, kandokando ya barabara ya kuelekea Karbala utaona makundi ya watu wenye azma na shauku kubwa ya kukutana na sayidi na Imam wao. Utawaona watu wa Iraq wakiwahudumia waumini wanaoelekea Karbala na kutoa kila walichonacho kwa mazuwari wa Imam Hussein bila ya kutarajia chochote kutoka kwa watu hao isipokuwa thawabu na radhi za Allah na Mtume wake. Wairaq hao huchinja wanyama kama mbuzi na kondoo, kupika chakula na kuwakirimu waumini wanaosafiri kwa miguu.

Bwana mmoja ambaye ni mkuu wa familia yake anasimulia akisema: Katika Kipindi cha mwaka mzima mimi huwa natenga sehemu ya kipato changu kwa ajili ya siku hizi, na katika siku za Arubaini ya Imam Hussein (as) huwa ninatumia fedha hizo kwa ajili ya kuwahudumia watu wanaokwenda kumzuru mtukufu huyo. Bwana huyo anaendelea kusimulia kwamba: "Tangu nilipoweka nadhiri hii kwa ajili ya Imam Hussein (as), Mwenyezi Mungu (SW) ameyapa baraka makhsusi maisha yangu", mwisho wa kunukuu.

Ukweli ni kwamba, kumuashiki na kumpenda Imam Hussein (as) ambaye kama alivyotwambia Mtume wetu Muhammad (saw), ni Bwana wa Vijana wa Peponi, hakuwezi kupimwa wala kuelezeka kwa maneno bila ya mtu kwenda mwenyewe na kujionea kwa macho. Huko utaona jinsi watu makarimu wa Iraq wanavyowabembeleza waumini kupumzika walau kidogo katika mahema yao na kupata chochote katika yale waliyowatayarishia kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuonesha upendo wao kwa Mtume na Ahlubaiti wake.

Ukiwa njiani pia utaona mahema ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ambayo yanatoa huduma za afya na tiba bure kwa vipenzi wa Hussein. Utawaona madaktari na wauguzi wa kujitolea wanaoshiriki kutoka huduma kwa mamilioni ya waumini wanaotembea kwa miguu kwenda kukutana na mahabubu wao kwa ajili tu ya kupata thawabu na radhi za Mwenyezi Mungu SW. Vilevile utawaona watu wanaoketi kandokando ya bararaba waliojitolea kushona au kupiga rangi viatu vya waumini wanaoelekea Karbala au kuosha na kukanda miguu ya waliochoka na kupatwa na maumivu katika safari hiyo ya upendo na mahaba.

Picha hii ya watu wanaojitolea kukanda miguu ya waumini waliochoka njiani wakielekea Karbala kwa hakika ni miongoni mwa vielelezo vya hali ya juu vya upendo na mahaba ya wahudumu hawa kwa Mtume na Ahlibaiti wake watoharifu. Wahudumu hao wa kujitolea huamiliana na waumini wanaokwenda kuzuru kaburi la mjukuu wa Mtume kama wauguzi wenye huruma na kumfanya muumini anayehudumiwa ajiulize maswali mengi na kuona jinsi anavyopewa hadhi na heshima kubwa. Naam, kumzuru Hussein ndiko kunakopandisha juu hadhi yao na kuwapa heshima na taadhima hiyo.

Sambamba na mandhari hizo za kibinadamu na za kuvutia utawaona baadhi ya watu wakitembea huku wakilia, wakiomba dua na pengine kuimba qasida zenye beti zinazomsifu Mtume (saw) na Ahlibaiti wake. Utaona waandishi habari na hata watalii wanaokwenda kushuhudia kwa karibu mandhari hizo za kipekee. Utawaona hata Wakristo na wafuasi wa dini nyingine wanaojiunga katika msafara wa mahaba na upendo ili kupata tajiriba hiyo ya aina yake.

Waislamu kutoka mabara mbalimbali ya Afrika, Asia, Ulaya na America wanaonekana pamoja na waumini wengine katika safari hiyo ya mamilioni ya watu wanaotembea kwa miguu kutoka Najaf hadi Karbala.

Mataifa mbalimbali yanashiriki katika matembelezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as)

Imepokewa kutoka kwa Imam J'afar Swadiq (as) kwamba amesema: Mtu anayeondoka nyumbani kwake kwa ajili ya kumzuru Imam Hussein (as) Mwenyezi Mungu humuandikia jema kwa kila hatua anayopiga na kumfutia baya. Na anapofika kwenye Haram ya Hussein (as) Mwenyezi Mungu humuweka katika watu wema, na anapokamilisha ziara yake husajiliwa katika watu waliofuzu....".