Arubaini, Kuenea Utamaduni wa Ashura
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi tena katika sehemu nyingine ya mfululizo wa makala hizi zinazokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib as.
Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi tamati ya sehemu hii ya pili ya mfululizo huu. Karibuni.
Inapowadia Arubaini ya Imam Hussein as nyoyo za maashiki na wapendwa wa Bwana huyu wa Mashahidi hutawaliwa na hamasa isiyo na mithili. Imekuja katika hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu watoharifu as kwamba, moja ya ishara na dalili za kuwa Muuumini ni kwenda kufanya ziara ya Arubaini ya Imam Hussein as. Ziara ya Arubaini ni kwenda Karbala katika kumbukumbu ya siku ya Arubaini tangu alipouawa shahidi Imam Hussein as. Lakini kile kinachoshuhudiwa katika siku ya Arubaini katika ardhi tukufu ya Karbala ni hamu na shauku ambayo kwa hakika ni zaidi ya maagizo na nasaha ya kulinda imani.
Ukweli ni kuwa katika vitabu vya hadithi kuna siku maalumu ambazo zimeelezewa umuhimu wake na kukokotezwa mno. Lakini inaonekana kuwa, Arubaini ya Imam Hussein as ina hesabu kando kabisa na siku nyingine za mwaka. Siku hii ina tofauti mno na siku na kumbukumbu nyingine. Katika siku hii mamilioni ya mazuwwar (wafanya ziara) huwasili katika Haram tukufu ya Imam Hussein as mahala ambapo aliuawa shahidi Imam huyo pamoja na masahaba zake wema na watiifu. Wakiwa na hamu, shauku na mapenzi makubwa yaliyoambatana na ikhlasi, mazuwwar hao hupuuza vitisho vyote vya ugaidi ambapo wakitembea kwa miguu kwa makumi ya kilomita na wengine mamia ya kilomita huelekea katika ardhi ya Karbala kwa ajili ya kwenda kufanya ziara siku ya Arubaini ya Imam Hussein as.
Swali linaloulizwa na wengi ni kuwa, mapenzi haya na hamasa hii ya kwenda kuzuru Haram ya Imam Hussein as katika siku ya Arubaini ni kwa ajili ya nini na inatokana na nini hasa?
Kwa hakika hii leo Waislamu wengi hususan Mashia wanatambua kwamba, maisha yao ni mdaiwa wa damu tukufu ya Imam Hussein iliyomwagwa kidhulma na jeshi batili la Yazid katika ardhi ya Karbala. Wanaamini kuwa, kama harakati ya Imam Hussein as isingelikuwepo, na kama Imam Hussein asingejitolea maisha yake yote na ya familia yake pamoja na masahaba zake watukufu namna ile katika ardhi ya Karbala, basi hii leo kusingekuwa na athari ya Uislamu wa kweli.
Imam Ja'afar Swadiq as alisema kumwambia Mwenyezi Mungu katika ziara ya Arubaini kwamba:
"Ewe Mwenyezi Mungu! Imam Hussein as alitumia kila kitu chake katika njia Yako kwa ajili ya kuwaokoa waja Wako na ujahili na upotofu, katika hali ambayo watu waliohadaika ambao waliuza utu na ubinadamu wao kwa dunia isiyo na thamani, walisimama dhidi yake na kumuua shahidi mtukufu huyo."
Katika ziara hiyo Imam Swadiq as anaashiria kile ambacho Imam Hussein as alikifanya katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya saada na ufanisi wa Mwanadamu. Hata hivyo kwa nini Imam Swadiq as anabainisha maneno haya katika siku ya Arubaini na anaifanya nafsi yake na watu wengine wazingatie umaanawi wa harakati ya Imam Hussein as?
Ukweli ni kwamba, katika historia kuna jinai nyingi zilizorekodiwa ambazo baadhi yake ni kubwa na mbaya zaidi ya tukio la Ashura na katika matukio hayo kuna watu wengi damu zao zilimwagwa na wakauawa shahidi, ambapo idadi yao ni kubwa kuliko idadi ya mashahidi wa Karbala. Lakini jinai na maafa hayo yamesahaulika na hayatajwi tena. Tukio pekee ambalo limebakia daima katika historia ni lile la Ashura. Hii ni kutokana na kuwa, Imam Hussein alisimama na kujitolea uhai wake kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu na kwa kuzingatia kwamba, dini ya Allah katu si yenye kufa, ndio maana jina lake daima limebakia katika kurasa za historia.
Baada ya tukio la Karbala na kuuawa shahidi Imam Hussein pamoja na masahaba zake, Bani Umayyah walikuwa wakidhani kwamba, Uislamu umeangamia na hakutabakia tena athari na ishara za dini hiyo tukufu. Kwa dhana hiyo potofu Yazid akasimama na kupiga ngoma ya kuangamia dini. Akishangilia kile alichokiona kuwa ushindi. Yazid alisema:
"Bani Hashim walicheza na Ufalme, hakuna habari iliyokuja wala Wahyi ulioshuka."
Yazid alisema maneno hayo katika hali ambayo, maeneo mengi ya Asia ya Kati na sehemu ya Ulaya ilikuwa ni sehemu ya utawala wake na watu wote walilazimika kutoa kodi kwa utawala wake akiwa kama Khalifa na Kiongozi wa Waislamu. Tawala mbili kubwa za Iran na Rumi zilikuwa zimeporomoka na zilikuwa chini ya mamlaka ya Waislamu na utawala wa Yazid ndio uliokuwa utawala mutlaki ulimwenguni.
Zaynab al-Kubra as aliyekuwa pamoja na Imam Hussein daima, baada ya kusikia maneno hayo ya Yazid hakunyamaza kimya, bali alisimama na kutoa hotuba. Alisimam kwa ushujaa na kuwaambia Bani Umayyah kwamba:
Ninaapa kwa Mola! fanyeni kila hila, lakini katu hamtaweza kufuta jina na utajo wetu katika kumbukumbu.
Kwa hakika ukweli ndio ulivyo, kwani kwa maneno ya Bibi Zaynab na Imam Sajjad as iwe ni mjini Kufa au njiani au hata walipokuwa Sham, kidogo kidogo yaliwafanya watu kuanza kufahamu ukweli. Hata hivyo dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayyah uliwafanya watu kutokuwa na ujasiri wa kuukosoa utawala wa Bani Umayyah au kusimama na kukabiliana nao.
Siku zikapita, hatimaye ikawadia siku ya Arubaini tangu alipouawa Imam Hussein na masahaba zake. Kafila na msafara wa mateka ambao walikuwa wakitoka Sham kuelekea Madina, ukasimama Karbala. Katika siku hiyo Jabir bin Abdillah al-Ansari na Atiya bin Aufi na watu kadhaa kutoka Bani Hashim walikuwepo hapo. Arubaini ya kwanza ikafanywa kwa ajili ya Imam Hussein na masahaba wake watiifu kando ya kaburi la Imam Hussein as. Mkusanyiko huo wa kwanza wa Arubaini ya Imam Hussein ukawa mwanzo wa kufikiwa malengo ya Imam Hussein as.
Katika Qur'ani Tukufu Waumini wameusiwa juu ya kumbukuka Siku za Mwenyezi Mungu ili siku kubwa za Allah zisije kusahaulika.
Arubaini ya Imam Hussein ni katika mwendelezo wa tukio la Karbala na kwa msingi huo kwa ajili ya kuadhimidsha Siku ya Ashura ambayo ni moja ya siku kubwa kabisa za Mwenyezi Mungu, katika siku ya Arubaini, maashiki na wapendwa wa Imam Hussein wakiwa na lengo la kujadidisha baia, hujadidisha hilo kwa njia bora kabisa yaani ya kufanya ziara huko Karbala. Hii ni kutokana na kuwa, Imam Hussein alikuwa ni kigezo na ruwaza njema ya kupigania haki ya Mwenyezi Mungu na kuleta marekebisho ya kidini na alitoa kila alichonacho katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Mkabala na kujitolea kwake huko na ikhlasi aliyonayo, Mwenyezi Mungu ameifanya daraja na nafasi Imam Hussein as kuwa ya juu na adhimu kiasi kwamba, kila mwaka mamilioni ya maashiki na wapendwa wa Bwana huyo wa Mashahidi humiminika katika siku ya Arubaini kwa ajili ya kwenda kufanya ziara katika Haram yake tukufu na kuonyesha huba na mapenzi yao kwa Imam mwema huyo, ambaye ameondokea kuwa kigezo cha mapambano dhidi ya dhulma na ukandamizaji.
Wananchi wa Iraq ambao ni wenyeji wa mazuwwar wa Imam Hussein hususan wakazi wa vijijini ambao kimaisha wana uwezo mdogo, hutoa kila walichonacho hata kiwe kidogo kiasi gani kwa ajili ya kuwahudumia na kuwakirimu mazuwwar wa Imam Hussein as. Huu ni ukweli ambao wafanya ziara wa Imam Hussein huushuhudia wakiwa njiani kuelekea Karbala ambapo kila mahala huonekana vibanda ambavyo ni maalumu kwa ajili ya vyakula mbalimbali vya Mazuwwar ambavyo hutolewa bure.
Katika matembezi makubwa ya siku ya Arubaini watu kutoka mataifa mbalimbali ya Iran, Iraq, Afghanistan, Sweden, Marekani, Canada, Afrika Mashariki kama Tanzania, Kenya na Uganda na kwingineko huonekana wakishiriki katika matembezi ya siku ya Arubaini kuelekea katika Haram ya Imam Hussein huko Karbala. Ukweli wa mambo ni kuwa, mazuwwar wa Arubaini ya Imam Hussein hufanya matembezi ya siku hiyo wakishikamana na sifa nzuri ya msafara wa Imam Hussein na hufanya bidii ya kuinua kiwango cha maarifa na utambuzi wa Ashura.
Kile ambacho tunaweza kusema tukielekea ukingoni mwa makala hii maalumu ni kwamba, tukio la Ashura lililotokea mwaka 61 Hijria, lilikuwa kama wimbi lililoanzia katika nukta ambayo, kadiri muda unavyosonga mbele linakuwa na nguvu na kuenea katika kila kona ya ulimwengu. Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein ni sehemu tu ya wimbi lenye kugubika ambalo siku baada ya siku litaikumba dunia yote.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…