Change Language: English

Arubaini Katika Maneno ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (5)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein (AS) ambapo leo tutazungumzia kauli na maneno ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuhusu tukio hilo adhimu. Endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni.

Siku ya arubaini baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) haikuishia tu kuwa siku ya kuomboleza kwa ajili ya Hussein (AS) na wafuasi wake, lakini Arubaini ilikuwa tufani ya mayowe ya ushuhuda na usaidizi yaliyotoka kwenye koo kavu zilizochoka za mateka wa Karbala na ya kujengeka ndani ya nyoyo za watu ujasiri na uthubutu wa kutetea haki; na kwa mara nyingine tena kuihuisha anga ya Ashura, kufa shahidi na thamani za kusimama imara kukabiliana na dhulma.

Ayatullah Khamenei

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, anaielezea Arubaini kuwa ni muendelezo wa harakati ya Imam Hussein (AS) ya kupambana na dhulma, na somo lake kubwa ni kuhuisha utajo na kumbukumbu ya kufa shahidi kwa kukabiliana na propaganda za adui. Ayatullah Khamenei anasema: "Umuhimu ilionao Arubaini ni kwamba katika siku hii, kwa tadbiri ya Mwenyezi Mungu, kizazi cha Mtume SAW kiliifanya kumbukumbu ya harakati ya Imam Hussein ibakie milele na kuweka msingi wa jambo hilo. Kama manusura wa mashahidi na wahusika wakuu, katika matukio tofauti – kama kuuawa shahidi Hussein Ibn Ali (AS) katika Ashura – hawatofanya hima ya kuhifadhi athari na kumbukumbu ya waliokufa shahidi, vizazi vinavyofuatia havitonufaika sana na matunda ya kufa shahidi….. Laiti kama Zainab al-Kubra na Imam Sajjad (AS) wasingefanya jitihada kubwa, - iwe ni katika jioni ileile ya Ashura Karbala au katika siku zilizofuatia wakiwa njiani kuelekea Sham na Kufa na katika mji wenyewe wa Sham na baada yake katika kuzuru Karbala na baada ya kuondoka kuelekea Madina na kisha katika kipindi chote cha miaka mingi cha uhai wa watukufu hao – kama wasingefanya jitihada kubwa ya kufichua na kubainisha na kuelezea hakika ya falsafa ya Ashura na lengo la Hussein Ibn Ali na dhulma za adui, tukio la Ashura lisingeweza kubaki hadi hii leo likiwa hai na lenye mrindimo na mchemko. Kwa nini Imam Sadiq (AS) – kwa mujibu wa Hadithi – amesema yeyote atakayesoma ubeti mmoja wa shairi kuhusu tukio la Ashura na akawaliza watu kwa ubeti huo wa shairi Mwenyezi Mungu atamwajibishia Pepo? Kwa sababu vyombo vyote vya propaganda vilikuwa vimejizatiti kuliweka mbali na gizani suala la Ashura; na kiujumla suala la Ahlu Bayt ili watu wasiweze kufahamu kimetokea nini na kadhia yenyewe ikoje. Propaganda iko namna hii. Siku zile pia kama ilivyo leo madhalimu na waonevu wenye madaraka walizitumia ukomo wa uwezo wao propaganda za uongo, za kiadui na kiafriti. Katika anga ya aina hiyo ingewezekana kweli kadhia ya Ashura – ambayo pamoja na adhama yake, ilitokea kwenye jangwa katika pembe moja huko ya Ulimwengu wa Kiislamu – iendelee kubaki na mtikisiko na msisimko kama huu? Kwa yakini bila ya jitihada zile ingetoweka. Somo inalotupa Arubaini ni kwamba inapasa tudumishe kumbukumbu ya haki na kumbukumbu ya kufa shahidi kwa kukabiliana na tufani ya propaganda za adui".

Arubaini imebadilika kuwa ni uendelezaji kwa wakati unaotakiwa ukumbusho wa tukio la Ashura na kudumisha kumbukumbu ya kufa shahidi na kupambana na dhulma. Mkusanyiko mdogo uliokuwepo siku hiyo wa ukoo wa Imam Hussein (AS) na baadhi ya watu wa kizazi cha Bani Hashim ulikuwa ni kama kufunga ahadi na baia'h na hakika na thamani aali za kiutu. Lakini mtu wa mwanzo kabisa kufika Karbala kwa madhumuni ya kulizuru kaburi lenye manukato la Imam Hussein (AS) ni Jabir bin Abdullah Ansari.

Katika kuelezea shakhsia ya Jabir na kisa cha mapenzi na heshima yake isiyo na kifani kwa Imam Hussein (AS), Ayatullah Khamenei anasema: "Jabir bin Abdullah Ansari ni mmoja wa mujahidina wa zama za mwanzoni mwa Uislamu; ni katika masahaba wa vita vya Badr; yaani kabla hajazaliwa Imam Hussein, Jabir bin Abdullah alikuwa akihudumu kwa Mtume na kupigana jihadi bega kwa bega pamoja naye. Alijionea kwa macho yake kuzaliwa, enzi ya utotoni na kuchuchuka kwa Hussein Ibn Ali (AS). Ni hakika kwamba Jabir bin Abdullah alimwona mara kadhaa Mtume Mtukufu akimbeba na kumkumbatia Hussein Ibn Ali, akimbusu macho yake, akiubusu uso wake; Mtume akimlisha chakula na kumnywisha maji Hussein Ibn Ali kwa mkono wake mwenyewe; kuna uwezekano mkubwa sana kwamba Jabir bin Abdullah aliyaona hayo kwa macho yake. Ni hakika kwamba Jabir bin Abdullah atakuwa amemsikia kwa sikio lake Mtume akisema Hassan na Hussein ni mabwana wa vijana wa Peponi. Muda mrefu baadaye pia baada ya Mtume, nafasi ya Imam Hussein na shakhsia ya Imam Hussein, iwe ni katika zama za makhalifa, zama za Amirul Muuminin na alipokuwa Madina au Kufa, yote hayo yalionekana mbele ya macho ya Jabir bin Abdullah Ansari. Sasa Jabir anasikia kwamba watu wamemuua shahidi Hussein Ibn Ali. Wamemuua shahidi mjukuu mpenzi wa Mtume huku midomo yake ikiwa imekauka kwa kiu. Jabir akaondoka Madina; kutoka Kufa akafuatana pamoja na At'iyah.

A'tiyah anasimulia kwamba katika siku ya Arubaini: "Jabir bin Abdullah alikwenda kando ya Mto Furat; akakoga josho, akavaa nguo safi nyeupe kisha akaanza kutembea taratibu na kwa heshima kuelekea kwenye kaburi la Imam Hussein (AS). Alipofika kaburini alisema kwa sauti kubwa mara tatu: "Allahu Akbar, Allahu Akbar, Allahu Akbar"; yaani anaamua kupiga takbir baada ya kuona namna gani mwana yule kipenzi cha Mtume na Zahra alivyouliwa shahidi kidhulma namna ile na mikono ya waporaji waovu. Kisha At'iyah akaendelea kwa kusema: "Kutokana na kuelemewa na huzuni na majonzi mengi Jabir bin Abdullah alinyong'onyea; akazirai na kuanguka juu ya kaburi la Imam Hussein.” Sijui kilichotokea lakini katika hadithi hii anaeleza kuwa wakati alipopata fahamu, alianza kuzungumza na Imam Hussein kwa kusema: "Assalamu Alaykum Yaa Aala-Allah, Assalamu Alaykum Yaa Saftwata Allah". (Amani ya Allah iwe juu yenu enyi watu wa Mwenyezi Mungu, Amani ya Allah iwe juu yenu enyi wateule wa Mwenyezi Mungu).

Watu wenye mapenzi na wenye kukipa heshima maalumu kizazi cha Ahlu Bayt (AS), kwa miaka na miaka sasa, kama alivyofanya Jabir wanafunga safari Siku ya Arubaini kuelekea kwenye Haram yenye nuru ya Imam Hussein (AS) katika mji wa Karbala. Arubaini, imefungua njia kwa safari ya miguu ya nyoyo kuelekea kwenye Haram hiyo ya Wilaya. Watu hao, mithili ya vipepeo vinavyoyazunguka maua, hufika huko wakitembea kwa miguu kutoka masafa na njia za mbali na karibu; na kama alivyo Jabir bin Abdullah hawafanyi hivyo kwa sababu nyingine isipokuwa mahaba na mapenzi yao kwa Ahlu Bayt (AS).

Ayatullah Khamenei anaizungumzia heshima na mapenzi hayo kwa kusema: "Kuna kitu kisicho na mfano na ambacho hakijawahi kushuhudiwa ambacho kimejitokeza katika miaka ya karibuni; nacho ni kutembea kwa miguu kutoka Najaf hadi Karbala au kutoka baadhi ya miji ya mbali zaidi na Najaf hadi Karbala. Baadhi wanaondoka na kutembea kwa miguu kutoka Basrah, baadhi kutoka mpakani na baadhi kutoka miji mingine. Harakati hii ni harakati ya mapenzi na imani; na sisi tunaitazama harakati hii kutokea mbali na kuwahusudu wale watu ambao wamepata taufiki hii."

Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS)

Kiongozi Muadhamu anaitakidi kuwa watu hao wanaokata masafa hayo na kutekeleza harakati hiyo ya kimapenzi na ya kiumini, wanafanya jambo kubwa na sahihi kabisa na wao wanahuisha sha'ar na alama moja kubwa. Kwa sababu katika jambo hili kuna imani na itikadi ya moyoni na ya kweli, chachu ya harakati na matendo na vilevile mahaba na mapenzi.

Ayatullah Khamenei anaielezea fikra ya Ahlu Bayt (AS) na fikra ya Kishia kuwa ni mchanganyiko wa akili na hisi za upendo na mchanganyiko wa imani na mapenzi; na anaitakidi kuwa hiki ndicho kitu ambacho kukosekana kwake kunahisika waziwazi katika madhehebu nyingine za Kiislamu.

Ayatullah Khamenei anaitaja sifa nyingine maalumu ya Arubaini na mjumuiko adhimu wa Waislamu kuwa ni athari yake katika kuleta umoja na anaeleza kuhusu izza inayopatikana katika mjumuiko wa Waislamu katika matembezi ya Arubaini kwa kusema: “Kama sisi sote tutakuwa kitu kimoja, nchi za Kiislamu, mataifa ya Waislamu – Sunni na Shia na madhehebu tofauti za Kisunni na Kishia – wote wakasafiana nia, wakawa hawadhaniani vibaya, hawadhamiriani kutendeana mabaya na hawatusiani, mtaona nini kitatokea duniani; ni izza kubwa kiasi gani utapata Uislamu! Umoja; ni umoja.”

Masunni katika matembezi Arubaini ya Imam Hussein (AS)

Naam; katika zama ambapo kundi moja la wanywaji damu wasio na chembe ya utu wamelichafua jina la Uislamu; na kwa kutumia jina la dini wanaeneza ulimwenguni chuki na hofu na kila linalokinzana na utu na kuuaibisha Uislamu na Waislamu; inatangazwa ulimwenguni habari ya hii kwamba watu milioni 20, Waislamu, Mashia na Masunni, wenye mapenzi yasiyo na kifani, waliojawa na hisi nyofu za kiutu na katika upeo wa anga yenye adhama ya usafi na upendo wamehudhuria katika ardhi ya Karbala na mbele ya haram ya Imam Hussein (AS), habari ambayo inawapa walimwengu msisimko maalumu. Na hapo ndipo wasio Waislamu wanapojiuliza akilini mwao, huyu Hussein ni nani hasa aliyeziteka na kuzivuta nyoyo za watu wote hao na kwa nini hatujawahi kuelezewa Uislamu wa aina hii; bali kile ambacho kimekuwa kikitangazwa kila mara katika vyombo vya habari vya Magharibi ni Uislamu wa Kiwahabi na Kisalafi tu ulio mbali hata na harufu ya utu na ubinadamu?!

Hivi sasa tukio hili adhimu na huenda lisilo na mfano wake ulimwenguni na katika zama za historia limezielekeza nyoyo kwenye haki na ukweli na kuzusha masuali mengi ndani ya akili za watu kuhusu shakhsia ya Imam Hussein (AS) na haki na ukweli. Ni kwa sababu hiyo Ayatullah Khamenei anaamini kuwa Arubaini katika tukio la Karbala lilikuwa kianzio na mwanzo. Ni mwanzo wa kutambua hakika na ukweli. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../