Aina tatu za Kifo na Maisha
Imetajwa katika hadithi kwamba kila mtu hufa aina tatu za vifo na dhidi ya vifo hivi vitatu mwanadamu huishi aina tatu za maisha. Mwanadamu lazima aishi aina zote tatu za maisha kwa wakati mmoja ili kuchukuliwa kama anayeishi na kama akifa vifo vyote vitatu basi hutoweka. Aina tatu za kifo na maisha haziko katika mpangilio; lazima mtu aishi aina zote za maisha kwa pamoja.
Aina moja ya kifo ni kifo cha mwili, kingine ni kifo cha moyo na cha tatu ni kifo cha kijamii. Kifo cha mwili ni kifo ambacho kwa kawaida tunakiona kwa macho yetu katika misingi ya kawaida. Mwili wa mwanadamu umejengwa kwa vitu viwili; mwili na roho. Mwili ni sehemu ya umbo na roho ni sehemu isiyo na umbo. Wakati mwili na roho vinashirikiana pamoja haya ni maisha ya kimwili ya mwanadamu. Utenganisho wa roho kutoka kwenye mwili matokeo yake ni kifo cha mwili. Kifo hiki ni kifo tu cha mwili na sio cha roho; muungano kati ya viwili hivi unavunjika na mwili hufariki lakini roho bado inaishi na huingia kwenye hali nyingine tofauti.
Sasa hebu tuelewe aina nyingine ya kifo ambayo ni kifo cha moyo. Inawezekana kwamba mwanadamu yuko hai kimwili wakati ambapo mwili wake unafanya matendo yote ya kawaida kama kunywa, kula, kulala, kutembea, kuzaa na uko katika harakati, lakini bado moyo wake unaweza kuwa mfu. Hapa moyo haina maana ya pande la nyama ndani ya vifua vyetu ambalo linasukuma damu. Pande hili la nyama limeitwa tu moyo lakini sio moyo halisi. Kazi ya moyo huu ni kusukuma damu ili izunguke kwenye mishipa; pande hili la nyama linafanya tu kazi ya kibaiolojia lakini halina hisia zozote. Moyo kiuhalisia ni ule wa roho na sio ule wa mwili. Huwa tunatumia misemo hii mara kwa mara kwamba ‘moyo wangu unatamani’, moyo wangu hauko tayari kulibali hilo’, nk. Moyo katika semi hizi sio ule ulioko ndani ya vifua vyetu; ni moyo wa roho (nafsi). Moyo huu ndani ya mbavu zetu hauna uhusiano na moyo wa roho. Kama moyo wa mwili unafanya kazi sawasawa basi hii haina maana kwamba moyo wa roho (nafsi) nao vilevile una siha nzuri na hai.
Moyo huu wa roho vilevile hufa na hiki ni kifo cha roho na utu. Swali ni lini hutokea? Wakati muungano kati ya roho na mwili unapovunjika husababisha kifo cha mwili, halikadhalika roho hufariki pia wakati muungano wake na kitu kingine unavunjwa. Ni pamoja na nani roho imeunganishwa; ambapo utenganisho wake husababisha kifo? Hii ni sawa na Yule anayesema:
“Basi nitakapomkamilisha na nikampulizia roho Yangu…” (Surah Hijr; 15: 29)
Mtukufu Mtume (saww) alisema katika hadithi yake kwamba moyo ambao hauna ukumbusho wa Allah hufariki. Mwili uko hai na katika mwendo lakini roho imekufa. Utakuwa umewahi kuona maeneo ya makaburi ambako imezikwa miili ya wakubwa zetu, jamaa zetu na ndugu zetu, lakini wakati roho au moyo unapokufa hivyo nao una maeneo ya makaburi. Maeneo ya makaburi ya roho sio sawa na yale ya mwili. Mwili unazikwa sehemu fulani na roho sehemu fulani tofauti. Maeneo ya makaburi ya roho ni pale ambako roho na mioyo huzikwa. Eneo la makaburi la roho ni ile nyumba ambako kuna mchezo wa pumbazo; ni chumba kile ambako kuna uchupaji wa mipaka na uovu, eneo lile ambalo katika mkusanyiko wake hakuna utajo wa Allah (s). Haya ni maeneo ya makaburi ya nyoyo na roho.
Wakati mtu ambaye hana utajo wa Allah katika moyo wake anajenga nyumba kutokana na pato la rushwa, wizi na unyang’anyi, anapoulizwa ni kitu gani anafanya? Jibu lake litakuwa kwamba ninajenga nyumba; lakini kama utaiuliza roho yake ni kitu gani kinachofanywa, roho itajibu kwamba hapa linajengwa kaburi langu. Mwili ambao unazikwa chini ya tani kadhaa za mchanga hauwezi kutoka nje, kwa sababu wakati ukiulizwa utasema kwamba nina mzigo wa tani kadhaa za mchanga juu yangu; na siwezi kutoka hapa. Hivyo mtu yeyote ambaye amezikwa chini ya mzigo wa tani kadhaa za udongo, mzigo ule ni kaburi lake. Hivyo kama mtu anaambiwa aje kuelekea kwa Allah na kama akisema kwamba niko chini ya mzigo wa kazi au uwajibikaji wa matumizi ya nyumbani au mafunzo au kazi nyingine kwa hakika amezikwa chini ya kaburi na hayuko huru. Kuna watu wengi ambao wana furaha kwamba wameishi maisha ya anasa, lakini hawatambui kwamba haileti tofauti yoyote na kaburi, ima limejengwa kwa udongo wa kawaida au kwa marumaru za ubora wa hali ya juu; kaburi ni kaburi bila kujali urembo wake wa nje.
Nilikwenda kwenye mji mmoja ambako kijana mmoja alisimama na kusema siwezi kuelewa unachokisema kwa sababu ili kuelewa unachosema huhitaji wakati mwingi. Na kwetu sisi wakati tukiamka asubuhi tunaona ankara ya umeme juu ya mlango wetu, kisha baada ya siku kidogo ankara za gesi, ankara za kadi ya mkopo (credit card,) kodi za nyumba na kufikia mwisho wa mwezi tunakuwa takriban tumezikwa chini ya mzigo wa ankara na kwa hiyo hatuna muda wa mazungumzo ya aina hiyo. Ni kama mtu aliyekufa anayesema kutoka kaburini mwake kwamba sielewi Sura hii ya Fatiha unayoisoma juu ya kaburi langu kwa vile niko chini ya mzigo wa udongo. Utamjibu kwa kusema kwamba sababu inayoacha nisome Sura hii ya Fatiha juu ya kaburi lako ni kwa ajili ya kukupunguzia mzigo huu, Sura hii ya Fatiha sio ya kukuondolea mzigo wako wa udongo bali mzigo wa dhambi zako. Hivyo nilimjibu kijana yule kwamba sababu ambayo inaacha niseme yote haya ni kwa ajili ya kukuondolea wewe mzigo kutoka kwenye moyo wako na maisha yako.
Sasa, kama huziki mwili uliokufa utaoza na kuleta harufu mbaya sana. Kama mtu ana mapenzi ya hali ya juu sana kwa jamaa yake na akaacha kumzika na akauweka mwili wake ndani ya nyumba yake, basi kwa siku chache tu mwili huanza kutoa harufu mbaya na harufu hii itaanza kuenea nje ya nyumba mpaka nyumba za jirani; kisha katika eneo lote na kila mtu ndani na nje ya nyumba katika eneo lote ataathiriwa na harufu hii. Kwa hiyo, tumeambiwa kuzika mwili mapema iwezekanavyo kwa vile ni vizuri kwa marehemu na halikadhalika kwetu sisi.
Vivyo hivyo kama moyo uliokufa hautazikwa basi hilo pia huleta harufu na kila mtu ndani ya nyumba, majirani na eneo hilo husumbuka kwa ajili yake. Kifo cha moyo kama kilivyotajwa na Qur’ani Tukufu hutokea kwa hatua, katika hatua ya kwanza moyo hupata maradhi, kisha taratibu hupata tabaka za uchafu juu yake, kisha hufungwa na kupigwa muhuri, na kisha hatimaye moyo huu hufariki. Kama mwili uko hai na moyo umekufa basi mtu kama huyo huchukuliwa kama maiti inayoishi, ni maiti inayotembea.
Kuna aina ya tatu ya kifo kwa sababu kuna aina tatu za maisha pia ambazo mwanadamu huishi. Hii aina ya tatu ya maisha na kifo ni ile ya Umma (taifa). “Umma” maana yake jamii na taifa au watu ambamo mwanadamu hupitisha maisha yake. Moja ya kipengele muhimu cha maisha ya mwanadamu ni jamii. Mwanadamu anaishi maisha ya mwili, roho na pia maisha ya kijamii. Watakuwepo wale ambao miili yao ni hai, na mioyo yao pia ni hai na vilevile kijamii wako hai, lakini kisha kuna wale ambao miili yao ni hai na huwenda na mioyo yao pia ni hai, lakini kijamii ni wafu, wamekufa kifo cha kuwa “Umma”. Wamekufa kifo cha kijamii na kijumuiya, na hivyo nao pia ni kama miili iliyokufa inayotembea katika jamii. Ngoja nikufafanulie hili kwa mifano ili kwamba upate kulielewa hili kwa uzuri.