Change Language: English

Ukweli kuhusu fungaYa Siku ya Ashura

Historia ya Uislamu iliingia doa na majonzi pindi mjukuu wa Mtume (s), Imam Husayn (a) ambaye ni sahaba na kipenzi cha Mtume (s) aliyesifika kwa sifa za ukamilifu na utukufu, mrithi wa Mtume (s) kwa hulka na tabia, akiwa na pote la watu 72 tu aliridhia kujitoa muhanga na kufa kishahidi ili kuunusuru Uislamu. Ni yeye alisikika akisema: “Ikiwa dini ya Muhammad (s) haitasimama ila kwa kuuliwa kwangu, basi enyi panga njooni mchukue uhai wangu.” Aliyeamrisha mauaji haya ya kikatili alikuwa ni Yazid bin Muawiya bin Abu Sufyan wa ukoo wa Bani Umayyah. Ni yeye ndiye alimpa amri gavana wake wa mji wa Kufa, Ubaydullah bin Ziyad, kutekeleza kitendo hicho kwa ukatili na ushenzi ambao hajawahi kufanyiwa binadamu. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya Ashura yaani tarehe 10, mwezi wa Muharram, mwaka wa 61 H. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya majonzi kwa Ummah wa Kiislamu, kwa watu wa Madina, kwa wote Bani Hashim na kizazi cha Mtume (s), kwa wote wapenzi wa Mtume (s) na kizazi chake, kwa mbingu na ardhi na vilivyomo… Ama kwa Yazid na Bani Umayyah na mashia wao walisheherekea na kumshukuru Mungu! Damu hii tukufu, yenye enzi ya Sayyidna Husayn (a) na kizazi cha Mtume (s) pamoja na mashia wao iligeuka kuwa ni Dhulfikari iliyomuangamiza Yazid na mashia wake na baadae kuutokomeza utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Baada ya mauaji ya Karbala, waumini na wapenzi wa haki waliitikia mwito wa Sayyidna Husayn (a) wa kumnusuru kwa kuweka hai muhanga huu adhimu na malengo yake ya kupambana kulinda dini na kutokomeza utawala dhalimu. Ni dhahiri kwamba kumbukumbu za mauaji ya Imam Husayn (a) ni nakma na balaa kwa watawala wote madhalimu, kwani ni joto ndani ya nyoyo za waumini kuwapa nguvu kuangusha utawala wa watu jeuri. Hii ndiyo sababu kuu ya watawala kufanya kila jitihada kuhakikisha nuru hii ya tawhidi inazimika. Watawala wa Bani Umayyah waliokabiliwa na fedheha hii ya kumwaga damu ya Mtume (s) na waja wema, walitumia kila njama kufuta athari za tukio hilo na kuwasahaulisha Waislamu yaliyotokea hapo Karbala, siku ya Ashura. Njia ya mkato ilikuwa ni kuzusha hadithi nyingi zenye kutukuza siku ya Ashura kama siku ya Baraka na furaha! Ni dhahiri kwamba Maimamu wa Ahlul Bayt (a) walihuisha kumbukumbu za mauwaji ya Ashura hapo Karbala na kuifanya Ashura kuwa ni siku ya majonzi, msiba na kuomboleza. Zipo hadithi nyingi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (s) kuhusu kufunga siku ya Ashura na fadhila zake. Kitabu hiki kinarejea hadithi hizo za Mtume (s) na kuchambua ukweli wa hadithi hizo kwa kuchunguza wapokezi wa hadithi (Sanadi) na madhumuni ya hadithi (matini, nasi).