Change Language: English

Roho Ya Karbala Matengenezo Ya Ummah Leo

Ili tuweze kuielewa roho ya Karbala, hatuna budi kuielewa Karbala yenyewe ni nini, na duri yake katika historia.

Karbala ni jina la mahali katika Iraq. Mahali hapo palitokea mapambano makali sana baina ya ma­kundi mawili ya Waislamu. Kundi moja liliongozwa na Husayn bin Ali, na la pili liliongozwa na wafuasi wa Yazid bin Muawiya.

Katika mapambano hayo, wale wa jeshi la Husayn - waliopata watu 75 hivi, waume na wake - waliu­wawa kikatili karibu waume wote, pamoja na Husayn "wao", isipokuwa wachache tu wakiwemo wanawake. Hivyo kidhahiri "ushindi" ukawa ni wa jeshi la Yazid lililo­kuwa na watu wasiopungua 60,000.

Kisa na sababu ya vita hivyo ni nini? Alivyosema Husayn, ambaye ndiye aliyetoka kwenda kupigana, ni kwamba hakutoka kwa sababu yoyote nyengine isipokuwa ni kwa kutaka "kuutengeneza" umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na "kutaka kuamrisha mema na kukataza maovu", na "kufuata sera" ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Lakini ni nani Husayn, na ni nani Yazid? Husayn ni mtoto wa Ali bin Abi Twalib kuzaa na Mwana Fatimah binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Na Yazid ni mtoto wa Muawiya bin Abi Sufyan. Na kila mmoja katika hao ameelezwa kwa sifa zake katika vitabu vya Kiislamu vya historia.

Kukielewa vizuri chanzo cha vita hivyo, bila ya kwenda nyuma sana katika historia, ni sharti tuelewe khalfia ya mkataba uliofanywa baina ya Muawiya bin Abi Sufyan, babake Yazid, na Hasan bin Ali bin Abi Twalib, ndugu yake Husayn, na jinsi ulivyovunjwa. Pia ni muhimu kuelewa tabia na khulka za wahusika wawili hao. Yazid na Husayn, na jinsi jamii ya Kiislamu wakati huo ilivyokuwa imezorota katika nyanja mbali mbali za maisha yao.

Katika hali kama hiyo, ile roho ya kiislamu ya kupam­bana na maovu ilipotea. Kitu kilikuwa na thamani zaidi kuliko utu! Dini haikuwa na uzito tena. Nyoyo zilijaa khofu; tamaa ikawa mbele. Waislamu waliga­wanyika kikabila na kitabaka. Rushwa ikawa ndiyo sera rasmi. Vitisho vikawa ni jambo la kawaida. Ukatili waliofanyiana Waislamu, wenyewe kwa wen­yewe, hausemeki; na mengi mengineyo.

Ugonjwa ueneapo namna hiyo, na wale wa kuuganga wawapo hawana moyo wa kuuganga kwa khofu au ghafla zilizowashika, pafanyweje? Ni lazima papigwe mshindo mkubwa sana ili "walio­kufa wafufuke." Na mshindo huo, zama hizo, uli­kuwa ni shahada ya Imam Husayn (a.s.) huko Karbala. Asingejitolea yeye muhanga, na watu wake, Uislamu usingekuwako hadi hii leo.

Hiyo ndiyo roho ya Karbala’, Ilihitajika siku hizo Inahitajika leo, na itaendelea kuhitajika popote penye dhulma. Kama isemwavyo: "Kila siku ni Ashura, na kila ardhi ni Karbala”.

Hiyo ni khotuba iliyotolewa na Sheikh Abdillahi Nassir kwenye semina ya Imam Husayn. (Tarehe 28/5/2000)

Kama ilivyoahidiwa katika Torah, (Taurat) kitabu kita­katifu cha Musa na Injili (Biblia) ya Isa, Muhammad, muokozi wa Binaadamu, alizaliwa katika Al-Hijaz ambayo kwa sasa inajulikana kama Saudi Arabia miaka 53 kabla ya hijra (570 A.D). Na kulingana na ahadi hii ya vitabu vya kale, Qur’ani tukufu yasema:

“Na (wakumbushe) aliposema (Nabii) Isa bin Mariam (kuwaambia Mayahudi): “Enyi wana wa Israil, mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayejia nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad. (Muhammad).” (Qur'ani 61:6)

Na kutokana na Ibrahim na mtoto wake Ismail, Muhammad pia hutajwa kama Ahmad. Mtume alizaliwa akiwa yatima, maana babake Abdullah ibni Abdulmuttalib, alifariki kabla ya Mtume kuzaliwa.

Alilelewa na Babu yake Abdulmuttalib, hata alipo­fikisha umri wa miaka 6, mamake mzazi Amina binti Wahab, alifariki pia, vile vile baada ya kifo cha babu yake Abdulmuttalib, alilelewa na Ammi yake Abu Talib, ambae alimtunza kwa mapenzi kama mzazi wake na juu ya hayo alijitolea kumridhisha na kum­tekelezea kila alilohitaji.

Muhammad alitambuliwa kitambo kwa tabia zake njema, utukufu na uaminifu aliokuwa nao hata kabla ya kutangazwa kwake Utume. Alidhihirika wazi kama huyo ndiye Mtume wa mwisho kama ilivyo­teremshwa aya:

“Muhammad, si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali yeye ni Mtume wa Mungu na wa mwisho wa mitume na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.” (Qur'ani 33:40)

Mjumbe wa mwisho wa Allah alizaliwa katika enzi ambapo wanawake hawakuwa wakinyanyaswa tu, bali wakidhulumiwa na kuchukiwa. Watoto wa kike walizikwa wakiwa hai. Hii ilikuwa ni desturi ya watu hao katika enzi hiyo. Na kuipinga na kuio­ndosha desturi hii isiyokuwa ya haki katika jamii, kukawa ndio mwanzo wa jukumu la utukufu wa kazi yake.

Mnamo mwaka 23 K.H. (599 A.D), alizaliwa mtoto aliyeitwa Ali kwa Abu Talib, ndani ya Al-Ka’ba, nyumba takatifu ya Allah katika mji wa Makkah. Ali alikusudiwa kuwa mtetezi imara, na mfuasi mtiifu wa Mtume Muhammad.

Katika umri wa miaka 25, Mtume alimuoa mjane aliyeitwa Bibi Khadijah ambae alikuwa mwanamke mfanyibiashara mashuhuri katika nyakati zake. Khadijah alivutiwa na kupendezwa na tabia za utukufu wa adabu na uaminifu wa Mtume, hata akaamua kufunga nae ndoa ambayo Mtume hakuikataa. Aliku­bali ingawa bibi Khadijah alimpita kwa umri wake.

Kutokana na ndoa hiyo, Mtume alijaliwa mtoto mmoja tu wa kike, ambae ni Fatimah aliyezaliwa katika Makkah mwaka wa 6 K.H (616 A.D) nae hakuwa ni kipenzi cha moyo wake tu bali alitokea kuwa mfano mwema na wakuigizwa katika mwendo wa wanawake ndani ya Uislamu.

Mtume aliwatoa watu Gizani na kuwafunza utu kamili, aliwafunza jinsi mwanamke na cheo chake ipasavyo, kama ilivyotakiwa na Mwenyezi Mungu.

“Enyi, Mulioamini! si halali kwenu kurithi wanawake kwa jeuri. Wala msiwazuie (kuolewa na waume wengine kwa kuwa hamuwataki wala hamtaki kuwaacha ila kwa pesa) ili mpate kuwanyang’anya baadhi ya vile mlivyowapa. (Hapana ruhusa haya) isipokuwa wawe wamefanya uovu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na kama mkiwachukia basi (msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.”
(Qur'ani 4:19)

Mtume alimuheshimu mno binti yake kama itaki­wavyo katika utukufu wa sharia na kadhalika ali­sema, Fatimah ni pande la nyama yangu na yeyote anayemfurahisha yeye, atanifurahisha mimi na yeyote yule anayembughudhi huwa amenibughudhi mimi, na anayenibughudhi mimi anambughudhi Mwenyezi Mungu.

Mtume alipofikisha umri wa miaka 40 mwaka 13 K.H. (610 A.D), malaika mtakatifu Jibril alim­wasilishia ujumbe wa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kuutangaza utume wake ambapo Muhammad aliwaita watu wote wa jamii katika dhifa na kutaka maoni na rai zao kuhusu ukweli na uaminifu wake nao waliku­bali kwa kauli moja.

Ndipo alipowatangazia ujumbe wake:

"Semeni hakuna mungu apasaye kuabudiwa ila Allah, nanyi mtapata kufanikiwa” ‘kisha aliwajulisha habari za utume wake, ambapo baadhi ya jamaa zake waliokuwepo ma-ami zake na wengineo isipokuwa Sayyidna Ali walimpuuza na kumfanyia stizahi kwa kutoamini ndipo Mtume alipomtangaza hadharani Sayyidna Ali aliyekuwa na umri wa miaka 11 kama msaidizi na khalifa wake pasikuwajali waliokuwepo.’