Change Language: English

Pamoja na Imam Hussein (AS), kutoka Madina hadi Karbala (3)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika sehemu nyingine ya makala maalumu ya Mwezi wa Muharram ambapo leo tutaendelea kuangazia baadhi ya maneno aliyoyasema Imam Hussein AS akiwa Makka na katika njia ya Madina kuelekea Karbala. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Kutokana na kuwa watu wa Kufa walikuwa wamefahamu kuwa Imam Hussein AS alikuwa amekataa kumbai Yazid na kwamba Mtukufu huyo yuko Makkah, walimtumia barua binafsi na za pamoja wakimwambia:

"Sisi tunamhitaji Imam na Kiongozi ambaye atatuondoa katika upotofu na kuiongoza meli yetu iliyokumbwa na dhoruba katika pwani. Sisi watu wa Kufa tunampinga Nu'man bin Bashir ambaye ni gavana wa Yazid katika mji huu. Hatushirikiani naye na hata hatusali naye sala ya jamaa. Tunasubiri uwasili hapa na tutafanya kila tuwezalo kufanikisha malengo yako. Tutatoa mali na nyoyo zetu muhanga kwa ajili yako."

Kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, katika kujibu barua hizo ambazo zilipindukia elfu 12, Hussein bin Ali AS aliandika hivi:

"Kwa jina la Allah Mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu. Kutoka kwa Hussein bin Ali kwa wakuu na viongozi wenye Imani wa mji wa Kufa. Ama Baad... Mimi ni ndugu na binamu yake -Muslim bin Aqil-. Ni jamaa yangu ambaye ninamuamini na nimemtuma kwenu. Nimemtaka awe nanyi ili aweze kuzifahamu fikra zenu kwa karibu na kisha anifahamishe natija. Iwapo takwa la waliowengi pamoja na weledi na wajuzi wa Kufa ndilo lililo katika barua zenu na zimeakisiwa na wajumbe wenu, basi mimi pia, inshaAllah nitakuja kwenu kwa kasi. Naapa kuwa Kiongozi wa kweli na Imamu wa Haki ni yule ambaye anatekeleza maamurisho ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kuchagua njia ya uadilifu sambamba na kufuata haki na usawa. Nimeitoa nafsi yangu wakfu na najitolea muhanga kwa ajili ya maamurisho ya Allah na Uislamu."

Imam alimpa barua hiyo Muslim bin Aqil ili aipeleke Kufa na kabla ya kuagana alimfahamisha hivi: "Mimi ninakutuma wewe kwa watu wa Kufa na namuomba Allah akupe taufiki kwa kile kitakachomridhisha na kumfurahisha. Nenda na Allah atakulinda na ni matumaini yangu kuwa mimi na wewe tutafikia daraja la mashahidi."

Imam Hussein AS katika barua hiyo sambamba na kujibu matakwa ya watu wa Kufa na kutangaza kumtuma mjumbe wake ambaye alikuwa ni ndugu yake aliyemuamini alitangaza kuwa Imam na Kiongozi ambaye kila Muislamu anapaswa kumtii ni yule ambaye anatimiza sharti la kutekeleza mafundisho ya Kitabu cha Allah sambamba na kuzingatia haki na uadilifu na pia kuitoa waqfu nafsi yake katika njia ya Allah. Aidha alimtuma Muslim bin Aqil mjini Kufa ili kupata yakini kuhusu ushirikiano wa watu wa mji huo. Jambo hili linaonyesha kuwa Imam Hussein AS hakutosheka tu na madai ya watu wa Kufa kuwa ni watiifu kwake.

Wakati msimu wa Hija unapokaribia, Mahujaji Waislamu huanza kuingia katika mji mtakatifu wa Makka. Mwanzoni mwa Mwezi wa Dhul Hijja, Imam Hussein AS alipata habari kuwa, kwa amri ya Yazid bin Muawiyya, Umar bin Sa'ad bin Aas aliteuliwa kidhahiri kuwa Amiri wa Mahujaji lakini lengo laki kuu la kuingia Makka lilikuwa ni kutekeleza njama hatari. Yazid alimpa Umar bin Sa'ad jukumu la kumuua Imam Hussein AS pahala popote pale atakapoweza mjini Makka. Kwa kuzingatia hilo Imam aliamua kuwa, ili kulinda heshima ya Makka, aondoke pasina kutekeleza ibada ya Hija na badala yake alitekeleza Umrah Mufrada na hivyo tarehe Nane Dhul Hijja aliondoka Makka na kuelekea Iraq. Kabla ya kuondoka, Imam alitoa hotuba hii mbele ya watu wa Bani Hashim na kundi la Mashia wake ambao walijiunga na mtukufu huyo katika kipindi alichokuwa Makka. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo:

"Shukrani zote anastahiki Allah, kile akitakacho Allah ndicho kitakachokuwa. Hakuna nguvu inayoweza kutawala ila kwa irada yake Allah. Salamu za Allah ziwe juu ya Mtume wake. Sisi tunafurahi kwa kila ambacho kinamridhisha Allah. Tunapokumbana na balaa pamoja na mitihani, tunasubiri na kuwa na istiqama. Yeye ndiye atakayetulipa kwa ajili ya subira yetu. Hakutakuwepo na utengano baina ya Mtume na watu wa nyumba yake na watakuwa pamoja peponi. Hii ni kwa sababu -Ahlul Bayt- walikuwa chanzo cha furaha na nuru katika macho ya Mtume na ni wao ndio watakaokuwa njia na wenzo wa kufikiwa ahadi ya kuasisiwa utawala wa Allah SWT. Mfahamu kuwa kila mmoja kati yenu ambaye anataka kujitolea muhanga kwa damu na roho yake katika njia yetu hii ili afikie daraja ya shahada na akutane na Mola wake, basi awe tayari kuondoka nami ili kesho asubuhi tuanze safari, Insha Allah."

Kwa maeleo hayo tunaona namna Imam alivyotoa wito kwa wafuasi wake watiifu waandamane naye ili kila ambaye moyo wake ulikuwa umefungamana na mambo ya dunia aweze kubaki. Katika hotuba hiyo, Imam alizungumza kwa uwazi kuhusu kufa shahidi. Aliwafahamisha wafuasi wake kuhusu suala hili ili nao wawe tayari kujtolea muhanga, wawe tayari kumwaga damu zao kwa njia ya Allah SWT.

Wakati Hussein bin Ali AS alipotangaza kuanza harakati yake ya kuelekea Iraq, kundi la watu lilijitokeza kuipinga safari hiyo. Walimsihi mtukufu huyo afutilie mbali safari hiyo. Sababu ya upinzani wa watu hao ambao walikuwa wakimtakia mema na walioona mbali ni kuwa, watu wa Kufa wakati huo walijulikana kuwa wenye kuvunja mikataba na wasio watiifu. Ushauri huu wa kujaribu kumshawishi Imam Hussein AS asiende Kufa ulianzia Madina na kushika kasi alipofika Makka baada ya kubainika wazi kuwa ana azma imara ya kuendeleza safari hiyo hadi Karbala.

Kati ya waliomsisitizia Imam abaki Makka walikuwa ni Ibn Abbas na Ibn Zubair

Imam hakukubali ombi hilo na katika kumjibu Abdullah bin Zubair alisema: "Iwapo mimi nitabakia Makka au sehemu yoyote nyingine ile hata katika kiota cha ndege, watawala hawatasita kunisaka kwani hitilafu zangu na utawala haziwezi kutatuliwa. Hii ni kwa sababu wananitaka nifanye jambo ambalo kamwe siwezi kukubali na mimi ninawataka wafanye jambo ambalo hawawezi kuliafiki."

Moja ya hotuba muhimu zaidi za Imam Hussein AS kuhusu Karbala ni wakati alipokutana na malenga maarufu aliyejulikana kama Farazdak. Wakati walipokutana Imam Hussein AS alikuwa ameanza safari yake kutoka Makka kuelekea Iraq. Farazdak naye alikuwa ametoka Kufa akielekea Makka kwa ajili ya ibada ya Hija. Alikutana na Imam nje ya mji wa Makka. Malenga huyo mashuhuri wa Kiarabu alishangaa kumuona Imam akiwa na haraka na alimuuliza hivi: "Ewe mwana wa Mtume! Unaenda wapi haraka hivi?" Ilimbainikia Farazdak kuwa Imam alikuwa ameanza safari yake kabla ya kumalizika Hija. Katika kujibu, Imam alisema: "Iwapo singeharakisha, wangenikamata na kunisumbua."

Kimya cha Farazdak kiliashiria kudiriki kwake hali ya Makka na tadbiri ya Imam. Hapo Imam alimuuliza: "Watu wa Kufa wakoje?" Farazdak katika jibu lake fupi lakini lililojaa busara alisema: "Nyoyo za watu ziko nawe lakini panga zao ziko dhidi yako."

Kwa maneno hayo ya Farazdak ilibainika kuwa watu wa Kufa ni wenye kutetereka kishakhsia na wenye kuvunja ahadi. Imam alinyamaza kimya kwa lahadha kisha akasema:

"Allah SWT atafanya kila atakalo. Kila siku Mola wetu anafanya kitu kipya. Iwapo irada ya Allah ni kile kile ambacho tunataka na tunafuatilia, tunamshukuru kwa neema zake. Lakini iwapo baina yetu kuna matakwa na matamanio ambayo yako mbali na irada ya Allah basi tusifikie tunayoyataka. Kile ambacho ni haki, chenye msukumo wa takwa na chenye kufuata njia na maamrisho yake basi hakitakuwa mbali na ukweli."

Kwa maneneo hayo Imam alikuwa ametoa tathmini ya kiirfani iliyobainisha namna ambavyo kushindwa au kufanikiwa katika njia ya haki yote huwa ni sawa. Nadharia kama hii huleta matumaini, usalama wa ndani ya nafsi na kuwepo msimamo sahihi mbele ya matukio na kuvuka kwa hekima matukio mbali mbali. Nadharia kama hii hufanya machungu kuwa matamu na huzuni kuwa furaha.

Katika sehemu nyingine ya maneneo ya Imam kwa Farazdak alimfahamisha: "Ewe Farazdak! Hawa - yaani Bani Umaya - ni watu walio pamoja na shetani na hawamfuati Mwenyezi Mungu Mwenye Rehma. Wameeneza ufisadi katika ardhi na wamekiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Wanakunywa pombe na wamenyakua mali za mafukara na masikini. Mimi ninapaswa kusimama kuisaidia dini ya Mwenyezi Mungu, kueneza mafundisho yake na kufanya Jihadi kwa njia yake."

Hatimaye Farazdak aliendelea na safari yake ya kuenda Hija naye Imam akiwa na msafara wa wafuasi wake wachache, aliekelea Kufa. Akiwa kati kati ya safari Imam alipata habari ya kuuawa shahidi Muslim bin Aqil, mjumbe wake huko Kufa.

Akiwa karibu na Kufa, jeshi la Hurr lilifunga njia ya Imam na wafuasi wake na kumzuia kuendelea na safari yake kuelekea mji huo, na hivyo kumlazimu kuelekea katika ardhi ya Karbala.