Change Language: English

Mapambano ya Imamu Husein

Kuwa na Kukumbuka ya Arubaini ya Imam Hussein (as) ni fursa nzuri ya kutafakari
kuhusu malengo ya mapambano ya mtukufu huyo na masahaba zake. Ushahidi wa
kihistoria unaonyesha kuwa mapambano ya Imam Hussein (as) ni miongoni mwa
harakati ambazo zinakuwa na taathira kubwa zaidi kadiri siku na miaka
inavyopita.

Japokuwa zimepita karne nyingi sasa tangu baada ya tukio la
Ashura lakini tukio hilo halikubakia katika jografia, eneo na zama zake, bali
limeendelea kuwa nuru na tochi iliyoendelea kuangazia historia ya mwanadamu na
kuwa na taathira kubwa kama jua. Kiongozi wa mapambano ya uhuru wa India Mahatma
Gandhi aliwazindua watu wa taifa lake akiwaambia kwamba njia pekee ya kushinda
wakoloni na dhulma ni kufuata nyayo za Hussein bin Ali (as). Akisema:
"Sikuwaletea jambo jipya wananchi wa India. Nilichoiletea India ni matokeo ya
uchunguzi na utafiti wangu kuhusu historia ya maisha ya mashujaa wa Karbala.
Iwapo tunataka kuikomboa India tunapaswa kupita katika njia iliyotumiwa na
Husssein bin Ali." Mwisho wa kunukuu.

Siku kama ya Arubaini ya Imam
Hussein (as) ni fursa nzuri ya kuchunguza tena ukurasa wa historia ya mapambano
yatakayodumu milele ya kiongozi huyo na kupata ibra na mafunzo yake. Baada ya
kuuawa shahidi Imam Hussein na masahaba zake waaminifu katika eneo la Karbala
Iraq, familia ya mtukufu huyo na jamaa wa mashahidi wa tukio la Ashura
walikamatwa mateka. Kiongozi wa msafara huo wa mateka alikuwa Bibi Zainab, dada
yake Imam Hussein (as). Wanahistoria wameandika kuwa Umar bin Saad, kamanda wa
jeshi la Yazid bin Muawiya alituma vichwa vilivyokatwa kwenye miili ya mashihidi
wa Karbala kwa Ibin Ziyad ambavyo viliambatanishwa na msafara wa mateka kuelekea
mji wa Kufa. Imenukuliwa katika historia kwamba miili ya mashahidi wa mauaji ya
Ashura ilibakia bila kuzikwa kwa kipindi cha siku tatu katika ardhi yenye jua
kali ya Karbala hadi watu wa kabila la Bani Asad walipofika mahala
hapo.

Watu hao waliswali miili mitakatifu ya mashahidi na kuizika. Wakati
huo msafara wa mateka wa watu wa nyumba ya Mtume (saw) ulikuwa ukielekea Kufa
katika hali ngumu na iliyojaa mashaka na baadaye ulipelekwa Sham kwa mtawala
Yazid bin Muawiya. Sayyid Ibn Tawus anasema katika kitabu cha Alluhuf fi Qatla
Tufuf kwamba: Gavana wa Yazid Umar bin Saad alisimamia msafara wa familia ya
Imam Hussein na jamaa wa mashahidi wa Karbala. Aliwapandisha wanawake katika
ngamia wasiokuwa na sogi wala mwavuli. Sehemu kubwa ya msafara huo iliundwa na
wanawake na watoto wadogo. Kati ya wanaume alikuwepo Ali bin Hussein Sajjad na
watoto wengine wawili wa Imam Hassan (as). Msafara huo ulipowasili katika mji wa
Kufa hali ya mji huo ilikuwa kama Ashura nyingine.

Bibi Zainab alikuwa katika hali ngumu mno kutokana na masaibu makubwa aliyokutana nayo safarini. Hata hivyo alisimama kidete na kutayarisha uwanja wa harakati za baadaye dhidi
ya watalawa dhalimu wa kizazi cha Bani Umayya. Bashir bin Khuzaim Asadi anasema:
"Siku hiyo Zainab bint Ali (as) alivutia mazingatio ya watu wote. Naapa kwa jina
la Mwenyezi Mungu kwamba sijawahi kuona mwanamke mwenye murua na mwenye
kuzungumza kwa ufasaha na ujasiri mkubwa kama yeye. Hakika alijifunza fani ya
kuhutubia kutoka kwa baba yake Ali bin Abi Twalib (as)."

Bibi Zainab (as) alihutubia umati wa watu wa mji wa Kufa akiwalaumu kwa kuvunja ahadi na kwa njia hiyo akavuruga ushindi wa kidhahiri wa Bani Umayya. Bibi Zainab aliwakemea mno
watu wa Kufa kwa makosa waliyofanya kiasi kwamba walianza kujilaumu na kuangua
vilio. Maneno ya Bibi Zainab yaliwabadili mno watu wa mji wa Kufa ambao
walianzisha harakati iliyopewa jina na Tawwabina au "Waliotubu". Sehemu moja ya
hotuba ya Bibi Zainab ilisema: "Enyi watu Wa Kufa! Enyi vigeugeu wasokuwa
waaminifu! Hivi kweli mnatulilia sisi? Naam, lieni mno na mcheke kidogo, kwani
mumepatwa na fedheha na aibu ambayo kamwe haitatoweka.

Eleweni kwamba mumetenda amali mbaya kwa ajili ya akhera yenu na mtapatwa na ghadhabu za
Mwenyezi Mungu." Hutuba za kuwazindua wananchi za shujaa wa Karbala Bibi Zainab
(as) ziliendelea hata huko Sham, makao makuu ya serikali ya Yazid bin Muawiya.
Suala hilo lilimtia kiwewe Yazid na kuamuru msafara wa mateka wa nyumba ya Mtume
urejeshwe Madina. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, katika siku ya arubaini tangu
baada ya tukio la Karbala au kwa mujibu wa riwaya nyingine katika siku ya
arubaini ya mwaka uliofuatia, familia ya Imam Hussein na masabaha zake
zilikwenda Karbala kuzuru makaburi ya mashahidi hao watukufu. Ahlul Baiti wa
Imam Hussein (as) na familia za mashahidi wa Karbala ziliathirika mno zilipofika
eneo hilo na kukumbuka yaliyotokea hapo. Kila mmoja alianguka kwenye kaburi la
shahidi wake na mandhari hiyo ilizusha simanzi na kilio kikubwa. Kwa utaratibu
huo, marasimu ya kwanza ya kuwakumbuka mashahidi wa Karbala yalifanyika katika
makaburi ya mashujaa hao wa historia ya mwanadamu.

Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe Hussein! Salamu kwa nyoyo za masahaba zako waaminifu na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Ahlubaiti wa Mtume waliouawa shahidi kwa
ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu. Baada ya tukio la Karbala Bani Umayya
walifanya propaganda kubwa za kuwaarifisha wapinzani wao kuwa ni waasi
wanaopigania madaraka na utawala. Walifanya njama za kuchafua sura na hakika ya
mapambano ya Karbala. Hata hivyo propaganda hizo chafu hazikufanikiwa kutokana
na kazi kubwa iliyofanywa na Bibi Zainab na Imam Sajjad (as).

Watukufu hawa wawili walibainisha ukweli wa mambo na malengo ya mapambano ya Imam Hussein katika nyakati tofauti na kufichua sura halisi ya Bani Umayya. Harakati hiyo
ilitayarisha uwanja wa harakati za mapambano zilizojitokeza baadaye dhidi ya
tawala dhalimu. Mapambano ya Tawwabin au Waliotubia, uasi wa watu wa Madina na
mapambano ya Mukhtar al Thaqafi huko Iraq yote hayo ni matunda ya hamasa ya
Karbala. Wimbi la mwamko lililojitokeza katika jamii lilionesha wazi jinsi umma
ulivyokuwa umeathirika na harakati ya Imam Hussein (as). Taathira hiyo ilikuwa
kubwa mno kiasi kwamba haikuishia kwenye wakati, zama au eneo makhsusi bali
imeendelea kufanyakazi yake kati ya wanadamu wote hadi katika zama hizi. Ukweli
huu umethibitisha msemo unaosema: "Kila siku ni Ashura na kila ardhi ni
Karbala."

Hapana shaka kuwa siri ya kubakia hai harakati ya Imam Hussein
imo katika dhati ya harakati hiyo yenyewe. Tangu mwanzoni mwa harakati yake,
Imam Hussein amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake alisisitiza juu ya misingi
inayokubaliwa na watu wote wenye hisi ya ubinadamu na maumbile safi. Kwani
wanadamu wote wanatukuza na kuheshimu mapambano ya kupigania uadilifu, kupinga
dhulma na uonevu na harakati za kusimamisha thamani za kibinadamu katika
historia ya kiumbe huyo. Harakati ya Imam Hussein (as) ilikusanya fikra na
thamani zote zinazowavutia wanadamu wa mirengo, dini na utaifa tofauti.
Mapambano hayo yalitoa taswira ya kupendeza kuhusu uungwana na thamani za
kibinadamu mkabala wa dhulma, uovu na ukatili.

Imam Hussein (as) alizongwa mno na ujahili wa watu kuhusu matukufu na thamani za kibinadamu na kwa msingi huo alikuwa akijaribu kuwaongoza na kuwazindua askari wa jeshi la Yazid
bin Muawiyya hata katika kilele cha mapambano ya Karbala na kuwalingania njia ya
kheri na uongofu. Imam aliutambua upotofu, dhulma na ufuska katika jamii kuwa ni
matokeo ya kuasi mafundisho ya dini na kupinga amri za Mwenyezi Mungu. Kwa
msingi huo alifanya kila awezalo kuwalingania watu mema na kukataza maovu japo
kwa kujisabilia yeye, jamaa na wafuasi wake katika njia hiyo.