Funga ya Karbala ilifaradhishwa
Baadhi ya riwaya katika vitabu vya hadithi vya Ki-Shia zinaonyesha kwamba kabla ya kuteremka aya ya funga ya Ramadhani, funga ya Ashura ilikuwa wajib. Mafaqihi wa ki-Shia walitosheka na kunakili riwaya na hitilafu bila kutoa rai maalum ila wachache kama vile al-Muhaqqiq Najafiy na al-Muhaqqiq Al-Qummiy waliosema kwamba ni wajib. Ama Mafaqihi wa ki-Sunni, Abu Hanifa anasema ilikuwa wajib. Wengine wakasema haikuwa wajib.
3.
Tunapowarejea ulamaa na wahakiki na tukachuguza ukweli wa historia, tunapambanua yafuatayo:
- Mwaka wa kiyahudi siyo Qamariyyah (kufuata mwezi) bali ni Shamsiyyah (kufuata jua).
- Mayahudi hawakuwa na saumu katika Ashura wala katika Muharram.
- Pia siku aliyoangamizwa Firauni kwa gharika, mayahudi wanaikumbuka kama ‘Pesach, Passover .’ Hii ni siku ya 14 mwezi wa Nisan ambao ni mwezi wao wa kwanza kidini na wa nane kikalenda. Mayahudi wanaadhimisha kumbukumbu hii kwa siku 7 hadi 8 kwa kula vyakula maalum, kwa swala na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda na kuwaokoa. Hawafungi.
- Ama funga ya mayahudi katika siku ya 10, siyo katika mwezi wa Muharram bali ni katika mwezi wao wa kwanza ambao ni Teshri na wanaiita siku hiyo ‘yaum kipur’ - yaani siku ya kafara - na ni siku ambayo waisraeli walipokea ubao wa pili katika mabao kumi ya sharia. Kwa hiyo ‘yaum kipur’, siyo siku ya kuokolewa, bali siku hiyo ni baada ya kuokolewa na Musa (a) kwenda miqaat na kutokea fitna ya kuabudu ndama na kurejea Musa (a) na kutangaza sharti ya kukubaliwa toba yao kwa kuua baadhi yao baadhi, na kwa kupata msamaha wa rafiki zao. Ndio maana siku kabla ya Kipur ni maalum kwa kusameheana. Na siku ya Kipur ni kwa ajili ya funga, swala na kutafakari. Hii ni siku takatifu kuliko zote.
- Pia namna ya kufunga kwa mayahudi inahitilafiana na ile ya kwetu Waislamu. Wao wanafunga kuanzia kuzama jua (maghrib) hadi kuzama jua siku ya pili.
Kwa hivyo hakuna hoja yoyote yenye kusimama ndani ya riwaya kutoka kwa Mtume (s) eti mayahudi walikuwa wakifunga siku ya Ashura, tarehe kumi Muharram.
Hoja za kitaalamu:
1. Katika gazeti la Al-Haady, Saghaf anaandika ya kwamba: “katika hali yetu hivi sasa hatuoni myahudi yeyote ambaye anafunga tarehe kumi ya Muharram au anayeisheherekea kama sikukuu. Hakuna katika rekodi za historia kiashirio chochote kwamba mayahudi walifunga siku ya kumi ya Muharram na kuisheherekea sikukuu. Bali mayahudi wanafunga siku ya kumi mwezi wa Tishrin ambao ni mwezi wa kwanza wa mwaka wao katika kalenda yao. Siku hiyo wanaiita ‘Yom Kipur’ na siyo Ashura.”
Pia anasema: “mayahudi wana kalenda yao binafsi inayotofautiana na kalenda yetu ya kiarabu (ya Kiislamu) kwa tofauti iliyo bayana. Mwezi wa kwanza ni Tishri na wa kumi na mbili ni Eylul. Kila mwaka mrefu, mwezi mmoja unaongezwa ambao ni Adhar Thani baina ya Adhar (mwezi wa sita) na Nisan (mwezi wa nane) na kuufanya mwaka kuwa na miezi kumi na tatu. Idadi ya siku katika mwaka ni siku 353, 354 au 355. Ama katika mwaka mrefu ni siku: 383, 384, 385.”
2. Mwanafalaki Mahmud Pasha anasema: “Inadhihirisha kwamba mayahudi miongoni mwa waarabu walikuwa pia wakiita Ashura siku ya kumi ya mwezi wa Tishri ambao kwao ni mwezi wa kwanza kisekyula na wa saba kidini. Mwaka kwa mayahudi ni shamsiyyah na siyo qamariyyah. Kwa hiyo Ashura aliyoghariki Firauni haiwezi ikawiyana na Ashura ya Muharram, bali siku hiyo iligongana na siku aliyowasili Mtume (s) Madina.
3. Abu Rayhan anasema: “Tishri ni siku 30… na tarehe kumi ya mwezi huo ndiyo funga ya Kipur na inaitwa Ashura. Ni funga ya lazima, kuanzia dakika thelathini kabla ya kutua jua siku ya tisa hadi nusu saa baada ya kutua jua siku ya kumi, kwa maana masaa 25… na saumu yake ni kafara ya kila dhambi …”
4. NATIJA:
Ashura ni siku ya kumi ya mwezi wa Muharram. Ni neno la Kiislamu wala halikujulikana zama za ujahiliyyah.
Siku waliyookolewa mayahudi na akaangamizwa Firaun, mayahudi wanaisheherekea katika mwezi wa Nisan, tarehe 14 ambao ni mwezi wa nane (ni mwezi wa kwanza kidini). Ama tarehe 10 ya mwezi wa kwanza (Tishri) wanaikumbuka kama Yom Kipur (siku ya Kafara)”.
Hijra ya Mtume (s) kwenda Madina ilikuwa katika mwezi wa Rabiul Awwal na siyo katika mwezi wa Muharram.