Change Language: English

Safari Ya Husein Kwenda Karbala Na Vituo Vyake

Taarifa katika siku hizo za kale na njia za mawasiliano zilikwenda pole pole sana kiasi cha kuwafanya watu wa Makkah kutoyasikia mabadiliko ya msingi ambayo yalikuwa yameathiri mpango wa kisiasa mjini Kufa na kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil na Hani bin Urwa kabla ya kuondoka kwa Husein miongoni mwao.

Kwa nini Husein aliondoka Makkah? Barua ya Muslim iliyopelekwa mwezi 12 ya Dhil Qadi1yaani siku 27 kabla ya mwisho wake wenye kuhuzunisha, ikimwomba Husein kuendelea kwenda Kufa katika kuitikia mialiko iliyopokelewa kutoka huko, na ikitaja mapokezi ya shauku kubwa aliyofanyiwa, haikuarifu kabisa kile kiwango cha umuhimu wa kuondoka kwake kwenda Kufa ambacho kingemshawishi Husein, hususan hasa kuhusu utekelezaji wa matendo yote yaliyoamriwa na Uislamu, kuondoka Makkah bila ya kutekeleza

Hijja kamili ambayo ingefanywa siku chache tu zijazo, na ambayo kwayo (hija) Waislamu hata kutoka sehemu za mbali ulimwengu mzima walikuwa wanakuja Makkah. Husein, hata hivyo, aliridhika mwenyewe kwa nafsi yake na utekelezaji wa ibada ya Umra, yaani hija ndogo. Sababu ya uondokaji wa haraka wa Husein kutoka Makkah ilikuwa kwamnba aligundua kuwasili kwa askari wakiwa katika mavazi ya mahujaji kwa uwazi kabisa kuja kumchukua yeye mateka hapo Makkah.

Husein alikuwa anatambua vyema kabisa mwisho wake wa msingi, yaani kifo cha kishahidi, na hili limeonyeshwa kwenye hotuba aliyoitoa wakati anaondoka Makkah, alisema: “Kifo ni kama shada la maua kwenye shingo ya mtu na ninatamani kukutana na wahenga wangu (mababu) kwa hamu kubwa sana kama vile Yaqub alivyokuwa na hamu kumuona Yusufu (mwanawe).

Ninaona kwa wazi kabisa kwa jicho langu la akili mandhari ya mahali pa tukio wakati maadui wa silika njema za kibinadamu, wakiwa kama wanyama wa mawindo watakapokuwa wanauchana vipande vipande mwili wangu. Hakuna ponyo dhidi ya hatima.

Sisi, watu wa nyumba ya Mtume, tunaridhia kimya kimya mapenzi ya Mwenyezi Mungu, tunakuwa wenye subira katika mitihani iliyoamriwa na Yeye, na tunapata ujira wa wale wanaojijanibu katika utashi Wake. Vipande vya nyama yake haviwezi kutenganishwa na Mtume. Yeyote yule ambaye yuko tayari kujitoa muhanga maisha yake pamoja nami na kukutana na Mungu wake anaweza kufuatana nami katika safari yangu.”

Katika kila kituo cha safari yake alikuwa mara kwa mara akikumbuka kifo cha kishahidi cha Yahya bin Zakariyya (Yohana mbatizaji) akisema kwam- ba mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu ilikuwa inatosha kuonyesha kotokuwa na thamani kwa ulimwengu huu kwamba kichwa cha Yahya kilikatwa kutoka mwilini mwake ili kikabidhiwe kama zawadi kwa kaha- ba miongoni mwa Waisraeli.2

Sababu ya kwa nini Husein alichagua kwenda Kufa ingawa alishawishiwa kuacha kufanya hivyo
na watakiaheri wa kweli, imeelezewa katika sura iliyopita nyuma na hakuna haja ya kurudia
kuitaja tena hapa.

Mbali na wale jamaa na ndugu zake wakuu ambao walifuatana naye kutoka Madina, wachache kati ya marafiki zake kutoka Hijaz na Basra pia walikwenda pamoja na Husein katika safari hiyo ya majaaliwa.3

Kwa kiasi kinachoweza kuyakinishwa, vituo mbalimbali vya safari ya Husein kwenda Karbala vinaweza kupangwa kwa utaratibu wa kituo na matukio katika mpango ufuatao:

Safah: Alipitia Safah bila ya kukaa hapo hasa. Hapa alikutana na al- Farazdaq,4mshairi ambaye akitoa makisio yake ya hali iliyokuwepo hapo Kufa, alisema; “Nyoyo za wakazi wa Kufa ziko katika upande wako, na panga zao ziko upande wa Bani Umayyah.” Husein alikubaliana na maoini ya al-Farazdaq na akasema kwamba angeshukuru kama amri ya Mwenyezi Mungu ingekubaliana na matakwa yake na kwamba kama mapenzi ya Mungu yalimzuia, ingekuwa si mafanikio haba kwa mtu yeyote yule ambaye nia zake zilikuwa halisi na dhamira safi.5

Tan’im: Husein alikodisha kiasi fulani cha ngamia hapa kutoka kwenye msafara wa watu wa Yemen kwa ajili ya usafiri wa vyombo vyake na baadhi ya sahaba zake. Hii inaonyesha kwamba alikuwa ameondoka Makkah bila ya maandalizi ya sawa sawa kwani wakati ulimtupa mkono. Ilikuwa ni katika hali hii kwamba Abdallah bin Ja’far, na Yahya bin Sa’id ibn al-Aas, ndugu yake gavana wa Madina na Makkah walimwona Husein ili kumshawishi asiendelee na safari ya kwenda Kufa. Abdallah alikuwa ni binamu yake Husein na hapo nyuma pia alijaribu kumshawishi kwa kumwandikia barua asiende Kufa.

Sasa, alipata hati ya maandishi kutoka kwa gavana wa Madina akitoa usalama kwa Husein, na ili kuupa nguvu zaidi na ustahili wa kusadikika utoaji huu wa usalama, alikuwa pia ameku- ja na ndugu wa gavana Yahya. Husein alijua thamani ya usalama aliopewa na mamlaka ya serikali za mitaa dhidi ya sera ya serikali kuu.

Hakukubaliana na mawazo ya Abdallah bin Ja’far kama hapo mwanzo. Akiwaacha watoto wake, Awn na Muhammad ili wafuatane na Husein, Abdallah bin Ja’far alirudi Madina.6

Dhat‘Irq: Baada ya kuondoka Abdallah bin Ja’afar, Husein alisimama hapa.7

Al-Hajir inBatnal-Rumma:Kutoka hapa Husein alipeleka barua kwa wakazi wa Kufa akiwaambia kuhusu kupata barua ya Muslim bin Aqil, kuondoka kwake mwenyewe kutoka Makkah tarehe 8 ya Dhil Hijja, na juu ya kuwasili kwake Kufa muda mfupi ujao, na kuwataka wao wafanye maandalizi yote muhimu.8

Mjumbe ambaye alikuwa anaichukua barua hii kuipeleka Kufa, Qays bin Mushir, alikamatwa katika sehemu iitwayo al-Qadisiyya na watu wa Ubaydullah bin Ziyad na alipelekwa kwa Ubaydullah (mwenyewe) ambaye alimtaka amnenee mabaya Ali bin Abi Talib kama alikuwa anataka kweli kuokoa maisha yake.
Qays alipanda juu ya mimbari na akamsifu sana Husein, na akamtaka kila mtu kuitikia wito wake. Hapa bila shaka kabisa alipoteza maisha yake.9

Wakati akiondoka kwenye kituo hiki, Husein alikutana na Abdallah bin Muti‘ ambaye alikuwa akitokea Iraq. Yeye pia hakukubaliana na mpango wake wa kwenda Kufa.

Zarud: Ilikuwa ni katika kituo hiki ambapo Husein alijipatia rafiki kutoka miongoni mwa watu wale ambao walikuwa kwao ni mamoja tu katika kuhusiana na jambo la watu wa nyumba ya Mtume. Zuhayr bin al-Qays alikuwa mmoja wa Waislamu wa namna hiyo, akiunga mkono lile kundi ambalo lilikuwa wakati huo likifahamika kama kundi la Uthman. Alikuwa njiani akielekea Kufa baada ya kutekeleza ibada ya Hijja, na alikuwa amepiga kambi karibu na sehemu inayoitwa Zarud. Imam Husein alimpelekea ujumbe akielezea haja ya kutaka kumwona.

Aliposikia ombi hili likikataliwa, mke wa Zuhayr alimkemea kwa ukali sana kwa ukosefu wake wa unyenyekevu kwa mjukuu wa Mtume kiasi kwamba (Zuhayr) alikwenda kwa Husein mwenyewe, na alivutiwa sana na uwazi wa hoja zake kiasi kwamba alielekeza kwamba mahema yake yapigiliwe karibu na mahema ya Husein. Alimtaliki mkewe na kumwambia kwamba yeye ameamua kufa kwa ajili ya Husein. Kisha kila mtu aliyefuatana naye pia aliondoka na kumwacha.10

Ilikuwa ni mahali hapa ambapo watu wawili wa kabali la Asad walimwona mtu anamkaribia Husein kutoka upande wa Kufa. Alipomwona mtu huyo Husein alimsimamisha ili kupata habari kutoka kwake juu ya vipi mambo yalivyokuwa yakiendelea huko Kufa. Mtu huyo, alipouona msafara wa Husein, alibadilisha njia ya safari yake, ambayo kwayo Husein aliendelea na safari yake. Watu wawili hao wa kabila la Asad, hata hivyo, walimfua- ta na kumkuta mtu yule ambaye aliwaambia kwamba wote Muslim bin Aqil na Hani bin Urwa walikwishauawa.11Walibakia kimya na taarifa hiyo na kuifikisha kwa Husein jioni iliyofuatia.

Tha’labiyya: Ilikuwa mahali ambapo watu wale wawili wa kabila la Asad walimwambia Husein, kwa idhini yake, mbele ya wengine wote waliokuwepo hapo wakati huo, habari za kuhuzunisha sana za kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil na kile cha Hani bin Urwa.

Viongozi wa watu kwa kawaida huficha misiba ya hasara kama hii ya wanajeshi na wafanyakazi ili kudumisha ari ya wafuasi wao. Hapa Husein alikwisha tambua mapema mno kwamba ushindi wa kimaada usingekuwa (upande) wake, na alikuwa hajali kabisa kuhusu idadi ya wafuasi wake. Kwa kweli, kiakili alikuwa tayari kuwaruhusu wote waondoke na kumwacha akutane na majaaliwa (ajali) yake, kwani alijua vyema kabisa kwamba ilikuwa ni damu yake tu (ndiyo) ambayo Yazid alikuwa anataka kuimwaga.

Kwa hiyo, alizipokea habari hizo za kuhuzunisha kwa kurudia rudia virai vya mazungumzo ya kawaida, “Hakika sisi tu wa Mwenyezi Mungu na Kwake tutarejea,” Na “Huruma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao.” Kisha aliendelea kunyamaza kimya.12Al-Dinawari anasema kwamba Husein alisema, “Tunatoa hesabu za maisha yetu kwa Mwenyezi Mungu,” akikusudia kwamba ‘tunatoa muhanga maisha yetu katika njia Yake na ni Yeye ambaye hutulipa ujira.”

Wale watu wawili wa kabila la Asad ambao walikuwa wameguswa sana na maendeleo ya kuhuzunisha waliona vigumu kuzishinda hisia zao zaidi. Walimwambia Husein: “Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, tafadhali sana usiyaache maisha ya familia yako nzima yote katika hatari na urudi nyuma kutokea kituo hiki hasa kwani hakuna mtu hata mmoja huko Kufa wa kukusaidia au kufanya nawe urafiki.

Kinyume chake tunahofia kwamba Kufa yote itakuwa ni yenye uadui juu yako.” Ushauri kama huu wenye uaminifu na huruma za dhahiri, pengine usingeweza kukataliwa vya kuridhisha kwa kutumia akili pekee.
Husein, tokea mwanzoni kabisa, alikuwa ameutambua mwisho wa kuhuzunisha wa safari yake ambayo alikuwa amekwishaianza, na zile habari za kusikitisha ambazo zilikuwa zimekwisha pokelewa hazikuleta tofauti yoyote ile kwake binafsi. Yeye, kwa hiyo alifikiria kwamba ingekuwa inafaa kwa ubora sana kuona vipi habari hizi zimepokelewa, kutoka kwenye kundi la watu wengine kabisa miongoni mwa sahaba zake. Akiwahutubia watoto wa Aqil, aliwauliza, “Ninyi mnafikiria nini sasa ambapo Muslim ameuawa kishahidi?”

Wote waliruka na kusimama kwa miguu yao na kusema kwa sauti kubwa, “Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu, hatutarudi mpaka tuwe tumelipiza kisasi kwa kifo cha Muslim au sisi wenyewe tuwe tumekunywa kikombe cha mauti kama ambavyo Muslim amefanya.” Kisha Husein aliwaambia wale watu wa kabila la Bani Asad, “Kama hawa wanayatoa maisha yao, kuishi kwangu kutahudumia lengo gani?”13Miongoni mwa wale ambao walikuwepo, mmoja wapo alisema kwamba Husein alikuwa na cheo kikubwa (hadhi) zaidi kuliko Muslim bin Aqil, na kwamba wakazi wa Kufa wangekimbilia kutoa msaada kwa Husein.

Husein hakuiunga mkono rai hii na aliamua kunyamaza.14Baada ya kuupitisha usiku ule hapa, na kujichukulia pamoja naye maji ya kutosha asubuhi na mapema, Husein alianza safari yake na aliwasili mahali paitwapo Zubala.15

Zubala: Ilikuwa ni mahali hapa ambapo Husein alipokea ujumbe16kutoka kwa Muhammad bin al-Ash’ath uliotumwa katika kutekeleza moja ya matakwa yake ya mwisho (wosia) ya Muslim bin Aqil kumwonya asiendelee na safari ya Kufa ambako asingeweza kupata msaada. Mjumbe huyo pia alileta habari kwamba Qays bin Mushir naye pia amekwisha uawa kwa upanga.

Inaonekana kwamba wale masahaba wa Husein ambao walisikia habari za kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil hapo Tha’labiyya walizihifadhi bila kusema.

Husein hakufikiria kwamba ni sahihi kuzuia taarifa hizi kwa jamaa wengine wa msafara wake ambao umekuwa katika mwelekeo wake umewavutia watu wengi ambao walifikiria kwamba Husein alikuwa anakwenda katika nchi ambako kwa uhakika angefanywa kuwa mtawala, na wangezawadiwa vizuri sana kwa kule kufuatana naye. Yeye alitaka kuziweka sawa fikra za watu hawa waliokuwa na mawazo potovu kama haya.

Akiwahutubia, akisema; “Nimepokea habari zenye kuumiza sana moyo kwamba Muslim bin Aqil na Hani bin Urwa wameuawa. Wale ambao waliotamka kwamba walikuwa tayari kutusaidia wamevunja ahadi zao. Kwa hiyo, yeyote yule awaye katika ninyi, anayependa kurudi atokako anaweza kufanya hivyo, sitamtaka kutoa maelezo kwangu.” Walipoyasikia maneno haya wengi katika kundi lake sasa waliondoka hivyo kwamba kundi hilo likabaki na watu wale tu ambao walifuatana naye kutoka Madina.17

Batnal-Aqaba: Husein alipata taarifa hapa kwamba Ubaydullah bin Ziyad amepeleka askari walinzi katika njia yote kati ya al-Qadisiyya na Udhayb. Alikuwa pia ameombwa kwa dhati kabisa na mtoa taarifa kwamba asiende Kufa bali arudi alikotoka. Husein alifanya mabadiliko kidogo katika mwelekeo wa safari yake, ili kuweza kuikwepa al-Qadisiya na akaendelea na safari yake.

Sharaf: At-Tabari na Shaykh al-Mufid wote wawili wameeleza kwamba Husein alihakikisha kwamba ngozi zote za maji na chupa za ngozi zilikuwa zimejazwa maji kabla yeye hajaondoka hapa.18Mwezi wa Muharam ulikuwa ndiyo kwanza umeonekana kwa mwaka wa 61 A.H, wakati Husein alipoanza safari yake. Walikuwa wamefika mahali karibu na al-Qadisiyya, wakati farasi fulani walionekana kwa mbali sana wakija kuwaelekea wao.
Dhu’ Husum: Husein kwa haraka sana alikwenda kwenye mlima Dhu’ Husum uliokuwa karibu ili kujilinda kutokana na kushambuliwa kutoka upande wa nyuma au kuzungukwa na maadui. Ilitangaa kwamba al-Hurr bin Yazid akiliongoza jeshi la askari elfu moja ametumwa kuja kumzuia Husein asiendelee mbele, kwani alijua yale mabadiliko ya njia ya Husein kupitia nje ya al-Qadisiyya ili kukwepa kukabiliana na jeshi hilo hapo. Ili kumfikia Husein, al-Hurr na watu wake walilazimika kufanya bidii sana katika joto la jangwani kiasi kwamba walipatwa na kiu kali sana yenye kuondoa nguvu na uwezo wa mwili. Farasi wao hawakuwa katika hali nzuri pia. Ilikuwa ni katika hali hii ya dhiki kubwa mno ambapo al-Hurr, watu wake na farasi zao walitokea mbele ya Husein ambaye kwa tabia ya kiungwana na huruma aliwapatia maji watu na wanyama pia, kiasi kwam- ba kiu yao ilikatwa kabisa. Swala za mchana ziliongozwa na Husein, na al-Hurr na watu wake walijiunga nao.19

Kabla ya swala Husein alimhutubia al-Hurr na wanajeshi wake akisema, “Sikuwajieni ninyi mpaka pale barua ziliponifikia zikiniita kuja kukuongozeni ili kwamba nyinyi labda mungeweza kuungana katika njia ya sawa na haki kwa kupitia kwangu mimi. Kama mtatimiza ahadi zenu mimi niko hapa tayari kulitimiza lengo langu. Hata hivyo, kama hamfurahii kuja kwangu kwenu mimi nitarudi kule nilikotoka.” Hakuna aliyetoa jibu lolote lile kuhusu maelezo haya.20

Wakati wa jioni hali kadhalika aliziongoza swala. Husein alimwambia tena al-Hurr na watu wake kwamba kama walikuwa na maoni tofauti na yale ambayo waliwasilisha kwake katika barua zao na kupitia kwa wajumbe wao, angeweza kurudi alikotoka. Al-Hurr alithibitisha kwa dhati kwamba alikuwa hatambui kabisa kuhusu barua hizo anazozizungumzia. Husein hapo hapo alitoa mifuko miwili ya shogi iliyojaa barua zikimwita Kufa kama alivyokwishaeleza.

Al-Hurr alijibu kwamba hakuwahi kutuma barua yoyote katika hizo, na vile vile aliweka wazi kwamba yeye alipewa jukumu kumwandama Husein ili kumpeleka kwa Ubaydullah bin Ziyad. Alipoyasikia haya, Husein alimwambia kwa sauti kubwa, “Kifo kitakuwa karibu zaidi na wewe.”21

Kisha Husein aliliacha wazo la kwenda Kufa na akiwahutubia sahaba zake, alisema sana juu ya mabadiliko ambayo yametokea na jinsi gani nyakati zilivyoteguka juu ya watu wema na waadilifu, na akasema kwamba ilikuwa ni laana kuishi katikati ya dhulma hizi.

Kisha Zuhayr bin al-Qays alismama ili kumhakikishia Husein kuhusu utiifu wake kwake, akisema, “Hata kama ulimwengu ungekuwa umemalizika kwetu sisi, na kuachana nao kumejitokeza tu kutokana na kutoa msaada wetu na kukuonea huruma wewe, tungechagua kukupa msaada wewe zaidi kuliko kubakia kuishi katika ulimwengu huu.”

Naf’i bin Hilal akitaja usaliti na utovu wa uaminifu wa baadhi ya marafiki wa babu mzaa mama wa Husein, yaani Mtume, na wa baba yake, Ali bin Abi Talib, alisema kwamba ilikuwa sasa ni zamu yake kukabiliwa na hali hizo hizo. Kisha alimhakikishia Husein kuhusu upendo wake kwake usiobadilika na uamuzi wake kumfuata yeye popote pale ambako angetaka kumchukua. Burayr bin Budayr al-Hamadan pia alizungumzia katika mkazo huo huo.

Kisha Husein aliamuru kwamba, kila mtu aliyekuwa pamoja naye apande mnyama na kwamba warudi kupitia njia ile ile ambayo wamejia. Al-Hurr aliwazuia wasifanye hivyo, kwani alitaka kumchukua (Husein) kumpaleka kwa Ubaydullah bin Ziyad. Husein aliapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba ilikuwa haiwezekani kwa matakwa yake haya kutekelezwa.

Baada ya mabishano makali iliamuliwa kwamba kwa vile al-Hurr alikuwa ameelekezwa kumfuata Husein mpaka atakapofika Kufa ambako sasa kulikuwa kumekoma kuwa mwisho wa safari ya Husein, Husein anapaswa achukue njia ambayo ilikuwa haielekei imma Madina wala kwenda Kufa, na kwamba al-Hurr angekuwa anamfuata tu kama alivyoagizwa.

Al-Bayda: Katika hotuba iliyotolewa kwa watu wa jeshi la al-Hurr na sahaba zake mwenyewe, Husein aliwakumbusha hadithi ya Mtume kwamba yeyote yule amwonaye mtawala ambaye anawakandamiza na kuwatesa raia zake, akahalalisha ambayo Mungu ameharamisha, anavunja viapo vyake kwa Mwenyezi Mungu, anapinga mafundisho na matendo ya Mtume na anawatendea uovu viumbe wa Mwenyezi Mungu, na anaruhusu mambo haya yafanyike bila ya kupingwa kwa maneno yake na vitendo vyake na hakufanya jaribio lolote la kurekebisha mambo hayo, basi huyo anastahili kuhesabiwa na Mwenyezi Mungu kwa namna ile ile kama ya mtawala huyo.

Akielezea juu ya hali katika nchi, Husein alisema, “Bani Umayyah wamechukua njia za shetani, wamekana kusalimu amri kwenye maamrisho ya Mwenyezi Mungu, wanatumia vibaya kile kinachowahusu Waislamu, wamehalalisha kile ambacho Mwenyezi Mungu ameharamisha, na wameharamisha kile ambacho Mwenyezi Mungu amekihalalisha. Katika mazingira haya, ni juu ya nani wajibu wa kutengeneza mambo haya upo zaidi kuliko juu yangu mimi?”22

Udhayb al-Hijarat: Watu watano, yaani Amr bin Khalid al-Saydawi, mtumwa wake Sa’d, Mujammi‘ bin Abdallah al-Aidhi, mtoto wake Aidh, na Janada bin Harith al-Salmani walifika kutoka Kufa wakiwa wamepanda juu ya farasi na pia wakiwa wameleta pamoja nao farasi mmoja. Al- Hurr alitishia kuwakamata kwani wao hawakuwa miongoni mwa kundi la masahaba wa Husein. Husein, hata hivyo, alisihi sana kwamba walikuwa marafiki zake na washirika na walikuwa chini ya ulinzi wake. Al-Hurr hakuleta matatizo baada ya hapo.

Mujammi bin Abdillah alimwarifu Husein kwamba watu muhimu wa Kufa wamehongwa sana ili kumpinga yeye, na kwamba wakati nyoyo za watu wengine zilikuwa bado ziko katika kumsaidia yeye, mikono yao na panga zao zingeamshwa dhidi yake. Al-Tirimma alimwambia Husein kwamba ameona jeshi kubwa mjini Kufa kiasi kwamba kamwe hajawahi kuona mfano wake kabla, na kwamba kwa vile ingekuwa ni kitu kisichowezekana kupigana vita na jeshi kubwa namna hiyo, alimshauri Husein kufuatana naye kuenda kwenye mlima Aja ambako watu 20,000 wa kabila la Tayyi wangekuwa katika huduma yake (kumhudumia) katika nchi ambayo wafalme wenye nguvu sana katika nyakati zilizopita walishindwa kuwashinda. Husein alikataa kulikubali ombi hilo.23

QasrBaniMuqatil: Husein alimuona Abdallah bin al-Hurr al-Jufi, mpandafarasi shujaa na maarufu sana wa Kufa akiwa anaishi hapa, na akamwomba msaada wake. Abdallah bin al-Hurr alikataa kumsaidia, laki- ni akajutia sana kukataa kusaidia kwake huku kwa kipindi chote cha maisha yake yaliobakia. Mwishowe aliungana na wale ambao walisimama kulipiza kisasi cha mauaji ya Husein.

Katika kuondoka sehemu hii, Husein alikuwa bado hajakwenda mbali wakati alipojisikia ni mwenye usingizi na akaota kwamba alimwona mpanda farasi akisema, “Watu hawa wanaendelea na safari yao, na mauti yanawakaribia.” Hapo hapo aliurudia msemo wa kawaida, “Hakikasisitu waMwenyeziMungunakwahakikakwaketutarejea.”

Aliisimulia ndoto yake kwa mwanawe, Ali Akbar ambaye alidadisi kama pengine walikuwa hawafuati njia ya sawa. Husein alimwambia kwamba kulikuwa hakuna shaka yoyote juu ya hilo. Ali Akbar kisha alisema kwamba katika hali hiyo hawana haja ya kujali kuhusu mauti.

Nineveh: Mpanda farasi mwenye silaha alileta barua kutoka Kufa itokayo kwa Ubaydullah bin Ziyad kuletwa kwa al-Hurr katika kituo hiki. Ilimwelekeza al-Hurr kumzuia Husein asiendelee zaidi na safari yake, popote ambapo barua hii ingemfikia. Iliendelea kusema kwamba mjumbe alikuwa amedhaminishwa kuambatana na al-Hurr na kumtaarifu Ubaydullah bin Ziyad juu ya hatua zinazochukuliwa na al-Hurr, na asimwache mpaka amri hiyo iwe imetekelezwa kikamilifu.24

Yawezekana Ubaydullah alikuwa amesikia tabia ya huruma ya al-Hurr kuhusu Husein, na amekuja kuonyesha wasiwasi kuhusu uaminifu wake. Al-Hurr alimzoesha Husein kwa ukamilifu yale yote yaliyomo ndani ya barua na, kwa hiyo, alilikataa ombi la Husein la kushuka kwenye kituo chochote kile zaidi ya mahali alipokwishafika.
Karbala: Husein alizuiwa na Al-Hurr hapo Karbala ili asiendelee mbele zaidi, na kwa hiyo aliweka kambi yake hapa. Ilikuwa ni siku ya pili ya mwezi wa Muharam mwaka wa 61 A.H, wakati Husein alipofika hapa.

Ile inayoitwa Karbala sasa hapo nyuma ilikuwa kwa kweli ni mkusanyiko wa vitongoji vingi mbalimbali, majina ya baadhi yao kama vile Nineveh na Ghadariyya bado yanasikika katika muktadha wa matukio ya Karbala. Mto wenyewe hasa wa Furati hauhusiki moja kwa moja na eneo la Karbala.

Tawi dogo la mto huo limejitenga lenyewe kutoka mto wenyewe katika sehemu iitwayo Ridhwaniyya na kupindapinda kuelekea eneo ambako kuna kaburi la Abbas, ndugu yake Husein na mshika bendera wake. Tawi hili la mto linaitwa Alqama, na kwa sababu ya chanzo chake wakati mwingine huitwa Furati pia.

Linakutana na mto wenyewe upande wa Magharibi wa Dhu Kifli. ‘Taff’ maana yake ni ufukwe wa mto, na neno hilo lilitumiwa kwa ufukwe ule wa Furati ambao ulipanuka katika upande wa Kusini kutoka Basra mpaka Hit, na kwa hiyo lilitumika kwa ufukwe ule wa Al-qama ambapo Karbala ndipo ilipojengwa. Karbala pia inaitwa Shatt al-Furat.Pengine, ingefaa kueleza tena kwa muhtarasi baadhi ya vipengele vya safari ya Husein kama ifuatavyo hapa chini:

Husein kamwe hakukusudia kufanya vita dhidi ya Yazid kwa kutumia nguvu za kizana ili kujipatia mamlaka ya kidunia. Alikusudia tu kuwatia nguvu Waislamu kutokana na hali ya utepetevu na kutojali kujihusisha na amri za sheria za Qur’an, na mafundisho ya Mtume, na kuleta mapinduzi ya kiroho ili kuwawezesha kuliona tishio baya sana ambalo kupanda cheo kwa Yazid kwenye ukhalifa kumelishikilia juu ya Uislam.

Kwa hiyo alikataa kula kiapo cha utii kwa Yazid ambaye aliagiza kwamba Husein auawe. Husein hakupenda kujitoa mhanga mjini Madina, kwani mtu angeweza kukodishwa kama Ju’da, mke wa Hasan ambaye alimtilia sumu mume wake, kumuua yeye pia, akiachwa mchochezi wa kosa hilo, Mu’awiyah, akiwa hafahamiki kabisa.

Hili lingeunyima mhanga wa Husein moja ya malengo yake makuu, ambayo ni kumweka wazi khalifa asiyefaa kwenye kutokukubalika kwa ulimwengu wote.

Kisha Husein alikwenda Makkah ambako alitumia muda wake kwa amani. Kwa ujio wa msimu wa Hijja, Husein aliona miongoni mwa makundi yanayokusanyika ya mahujaji, wauaji waliovaa kama mahujaji waliokuja ili kumchukua kama mateka au kumuua.

Tishio juu ya maisha yake lilizidi kukua kwa kiasi kikubwa kwamba ingawa ni siku chache tu zilizokuwa zimebaki kwa ajili ya ibada ya Hijja Husein aliridhika yeye mwenyewe binafsi na utekelezaji wa Umra (hija ndogo) na aliondoka Makkah na watu wa familia yake na marafiki.

Husein hakupenda kujitoa mhanga mjini Makkah kwani kufanya hivi kungevunja utakatifu wa Ka’abah. Aidha, katika mkusanyiko mkubwa wa mahujaji, muuaji angeweza kutoweka kwa urahisi, na kufanya utambulisho wake kama wakala wa serikali usiwezekane.

Kwa hali yoyote ile uondokaji wake kutoka Makkah wakati ambao haswa Waislamu kutoka nchi zote za Kiislamu walikuwa wanaingia, kulipata utangazwaji mkubwa katika rasi (peninsula) hiyo ya Uarabuni, na maelfu ya watu kutoka nchi za mbali na karibu watakuwa wamelazimika kujadiliana na kufanya midahalo kuhusu sababu za kuondoka kwa Husein, na kusalia kwa maoni ya umma lazima yalikuwa yameelekea kwenye upande wake.

Ilikuwa itegemewe tu kwamba Husein angekuwa lazima sasa aende huko Kufa ambako kutoka huko alikuwa amepokea mialiko yenye msisitizo kwa ajili ya kwenda huko kuwaongoza watu kwenye umoja wa kidini. Asingeweza kukataa kulichukua jukumu hili la kusifika na kuyakataa maombi ya watu wa Kufa kwa sababu ya utovu wao wa uaminifu uliokisiwa. Au basi ndio ingekuwa Husein aende mahali penginepo pale kama mgeni asiyealikwa?

Inaweza ikaonekana kwamba baadhi ya ndugu zake na wale marafiki zake watiifu na wale wote ambao walikutana katika vituo mbalimbali vya safari yake kuelekea Kufa walikuwa wakijaribu kumshawishi Husein asiende Kufa; katika kuunga kwao mkono, baadhi yao waliukiri utovu wa uwaminifu wa wakazi wa mji ule, wengine walithibitisha kudhihiri kwa uadui kwa watu pale (mjini Kufa), na wengine walisisitiza sana kutokuwezekana kulikabili kwa mafanikio lile jeshi kubwa lililojikusanya Kufa ili kupigana naye.

Lakini kwa vile Husein hakufanya safari hii kwa matumaini yoyote yale ya kufanikiwa katika kiwango cha kimaada, hata zile habari hasa zenye kuhuzunisha za kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil zilishindwa kumshawishi kufanya mabadiliko yoyote yale katika azimio lake.