Yazid Ni Nani?
"Sisi tu watumwa wa Yazid na ni kwake yeye kutuweka huru au kutuuza kwenye soko."
Watu wa Madina walilazimishwa kuyasema maneno haya kama ishara ya kumkubali Yazid bin Muawiya ambaye alitawala dola ya Kiislamu toka mwaka wa 680 mpaka 683 miladi. Fikra hii ya kuwatawala raia kama watumwa wa mtawala ilikuwa kinyume kabisa na mafundisho ya Kiislamu. Maneno tuliyoyataja hapo juu ambayo yalikuwa ni kiapo kilicholazimishwa watu wa Madina katika mwaka wa 683 ni thibitisho tosha la kuonyesha fikra za Yazid pamoja na viongozi wengine wa utawala wake.
Uislamu ulileta mizani ya kubainisha haki za mtawala na raia. Qur'ani tukufu yaeleza haya:
"Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrishieni kurudisha amana kwa mwenyewe. Na mtakapo hukumu baina ya watu, hukumuni kwa uadilifu”. (Qur'ani 4:58)
Ikiwa mtawala hatekelezi majukumu yake kama inavyotakikana (Utawala wa Uadilifu) basi hupoteza hadhi ya kuwa kiongozi. Imam Ali bin Abi Talib anasema:
"Kwa kuniwekea majukumu yenu, Mungu ameifanya haki yangu kwenu nyinyi na vile vile nyinyi mnayo haki juu yangu".
Kwa ufahamu huu, ni kitu cha kusikitisha kuona historia baada ya miaka 50 tu, tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.w), mtu kama Yazid bin Muawiya kuwa kiongozi wa Waislamu! Kwake Yazid, raia walikuwa ni kama vitu alivyo virithi kutoka kwa babake.
Kwa ujumla, karibu Waislamu wote wa wakati huo walikuwa wamelazimishwa aidha kwa vitisho au kwa kuhongwa, kumkubali Yazid kuwa mtawala baada ya Muawiya, babake. Mipango hii ilifanywa mwishoni mwa utawala wa babake.
Wakati Yazid aliingia kwenye utawala, mtu wa pekee aliyekuwa na sifa na tabia nzuri na ambaye pia alikuwa tisho kwake ni Imam Husayn bin Ali, mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Husayn bin Ali ndiye tumaini la mwisho kwa Umma wa Kiislamu kupambana na Yazid. Na kweli Husayn hakuuvunja moyo Umma wa babu yake.
Roho Ya Karbala Matengenezo Ya Ummah Leo
Ili tuweze kuielewa roho ya Karbala, hatuna budi kuielewa Karbala yenyewe ni nini, na duri yake katika historia.
Karbala ni jina la mahali katika Iraq. Mahali hapo palitokea mapambano makali sana baina ya makundi mawili ya Waislamu. Kundi moja liliongozwa na Husayn bin Ali, na la pili liliongozwa na wafuasi wa Yazid bin Muawiya.
Katika mapambano hayo, wale wa jeshi la Husayn - waliopata watu 75 hivi, waume na wake - waliuwawa kikatili karibu waume wote, pamoja na Husayn "wao", isipokuwa wachache tu wakiwemo wanawake. Hivyo kidhahiri "ushindi" ukawa ni wa jeshi la Yazid lililokuwa na watu wasiopungua 60,000.
Kisa na sababu ya vita hivyo ni nini? Alivyosema Husayn, ambaye ndiye aliyetoka kwenda kupigana, ni kwamba hakutoka kwa sababu yoyote nyengine isipokuwa ni kwa kutaka "kuutengeneza" umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na "kutaka kuamrisha mema na kukataza maovu", na "kufuata sera" ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Lakini ni nani Husayn, na ni nani Yazid? Husayn ni mtoto wa Ali bin Abi Twalib kuzaa na Mwana Fatimah binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Na Yazid ni mtoto wa Muawiya bin Abi Sufyan. Na kila mmoja katika hao ameelezwa kwa sifa zake katika vitabu vya Kiislamu vya historia.
Kukielewa vizuri chanzo cha vita hivyo, bila ya kwenda nyuma sana katika historia, ni sharti tuelewe khalfia ya mkataba uliofanywa baina ya Muawiya bin Abi Sufyan, babake Yazid, na Hasan bin Ali bin Abi Twalib, ndugu yake Husayn, na jinsi ulivyovunjwa. Pia ni muhimu kuelewa tabia na khulka za wahusika wawili hao. Yazid na Husayn, na jinsi jamii ya Kiislamu wakati huo ilivyokuwa imezorota katika nyanja mbali mbali za maisha yao.
Katika hali kama hiyo, ile roho ya kiislamu ya kupambana na maovu ilipotea. Kitu kilikuwa na thamani zaidi kuliko utu! Dini haikuwa na uzito tena. Nyoyo zilijaa khofu; tamaa ikawa mbele. Waislamu waligawanyika kikabila na kitabaka. Rushwa ikawa ndiyo sera rasmi. Vitisho vikawa ni jambo la kawaida. Ukatili waliofanyiana Waislamu, wenyewe kwa wenyewe, hausemeki; na mengi mengineyo.
Ugonjwa ueneapo namna hiyo, na wale wa kuuganga wawapo hawana moyo wa kuuganga kwa khofu au ghafla zilizowashika, pafanyweje? Ni lazima papigwe mshindo mkubwa sana ili "waliokufa wafufuke." Na mshindo huo, zama hizo, ulikuwa ni shahada ya Imam Husayn (a.s.) huko Karbala. Asingejitolea yeye muhanga, na watu wake, Uislamu usingekuwako hadi hii leo.
Hiyo ndiyo roho ya Karbala’, Ilihitajika siku hizo Inahitajika leo, na itaendelea kuhitajika popote penye dhulma. Kama isemwavyo: "Kila siku ni Ashura, na kila ardhi ni Karbala”.
Hiyo ni khotuba iliyotolewa na Sheikh Abdillahi Nassir
kwenye semina ya Imam Husayn.