Change Language: English

Wasia wa Mtume (s.a.w.w)

KISA CHA UANDISHI WA BARUA (WASIA WA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W)Ufafanuzi wa kisa hicho ni kama ifuatavyo: (Pindi Mtume alipofikiwa na kipindi cha kuiaga dunia (kukata roho) –Ihtidhaar- na nyumbani kwake kukiwa na watu kadhaa miongoni mwao akiwemo Omar bini- Khattab, Mtume (s.a.w.w) alisema: Nileteeni kalamu na karatasi nikuandikieni mambo ambayo pindi mkiyazingatia na kuyafanyia amali hamtopotea kamwe baada yangu, Omar akasema: Hakika Mtume amezidiwa na maumivu (anaweweseka), nasi tunacho kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'an), kinatutosha, watu waliokuwa nyumbani kwa Mtume wakahitilafiana na kugombana pia kupigishana kelele, kati yao kukiwa na wale wasemao: Mpeni kalamu na karatasi ili Mtume akuandikieni mambo ambayo hamtopotea kamwe baada yake, na kati yao wamo waliokuwa wakisema kama yale aliyo yasema Omar, na pindi walipozidisha kelele natofauti mbele ya Mtume (s.a.w.w) Mtume wa Mwenyezi Mungu akawambia: Tokeni nje. Na Ibnu Abass baada ya tukio hilo akisema: (Hakika huzuni iliyokuwa kubwa zaidi ni kule kumzuilia Mtume wa Mwenyezi Mugu kupewa karatasi ili awaandikie usia ule kutokana na tofauti yao au kutofautiana kwao na kugombana kwao) . Sayyid Sharafud-din amesema akielezea juu ya tukio hilo: (Na hadithi hii ni hadithi ambayo hakuna tofauti juu ya usahihi wake wala juu ya kutoka kwake kwa Mtume, na kwa hakika bwana Bukhari ameipokea hadithi hiyo katika sehemu nyingi katika sahihi yake, na imetolewa na Muslim mwishoni mwa usia katika sahihi yake pia, na imepokelwa na Ahmad kati ya hadithi za Ibnu Abbas katika Musnadi wake, na waandishi wengine wa vitabu vya Sunan na vitabu vya hadithi). ( Na tukizingatia katika kauli yake Mtume (s.a.w.w) isemayo: (هلم اكتب لكم كتاباً لن تضلوا بعده) (Leteni kalamu na karatasi nikuandikieni mambo ambayo hamtopotea baada yake) na kauli yake iliyoko kwenye hadithi ya vizito viwili (Thaqalain) isemayo: اني تارك فيكم كتاب اللّه وعترتي أهل بيتي) ما إن تمسكتم به لن تضلواابدا : Tutafahamu ya kuwa makusudio ya hadithi hizo mbili ni moja, na kwamba Mtume (s.a.w.w) katika maradhi yake alitaka kuwaandikia ufafanuzi na uchambuzi wa yale mambo aliyo yawajibisha juu yao katika hadithi ya Thaqalaini. Na si vinginevyo aliacha kufanya hivyo kwa sababu yale maneno yao waliyo mshutukiza nayo yalimlazimisha kuacha kuandika, kwani hakukuwa kumebakia nafasi ya kuathiri maneno yake hata kama angeandika wasia ule au mambo yale isipokuwa fitina na tofauti baada yake, tofauti ya kuwa je alikuwa akiweweseka katika yale aliyoyaandika–Twajilinda na Mwenyezi Mungu kutokana na hayo-au hakuweweseka, kama walivyotofautiana katika hilo na kutoa maneno na kufanya zogo mbele yake, na siku hiyo hakuweza kusema lolote tofauti na kauli yake aliyo isema kuwambia: (tokeni) – kama ulivyokwisha sikia-, na lau kama ange ng'ang'ania kuandika usia na mambo yale bila shaka wange sisitizia juu ya kauli yao ya kuwa anaweweseka na wangeendeleza kelele zao ili kuthibitisha kuwa anaweweseka- Twajilinda na Mwenyezi Mungu kutokana na hayo-na kuandika ngano na uzushi wao, na kuyaandika pia kuyajaza mabuku yao kwa jibu la usia ule na mambo yale aliyo yaandika na kwa yule ayatoleayo hoja. Kutokana na hayo na kutokana na hekima yake ya hali ya juu ilimlazimu Mtume (s.a.w.w) kuacha kuandika wasia ule na mambo yale aliyotaka kuyaandika na kuachana nayo ili watu hao wapingao pamoja na wafuasi wao wasije wakafungua mlango wa kuanza kutia shaka na kuutuhumu utume- Twajilinda na Mwenyezi Mungu na twajikinga nae- na kwa hakika Mtume (s.a.w.w) aliona kuwa Ali (a.s) na wafuasi wake ni wenye kutii madhumuni ya wasia na mambo yale aliyotaka kuyaandika, kwao ni sawa aadike au asiendike, na wengine si wenye kuyatekeleza na hawatayapa umuhimu hata kama ataandika, kwa hivyo basi - hekima-na kutokana na hali ilivyo kuwa ilikuwa ikimwajibisha kuacha kuandika usia huo kwani hakuna athari yoyote itakayotoa baada ya upinzani ule na upingaji ule ulio jitokeza isipokuwa fitina kama ionekanavyo) . MAIMAMU WA MADHEHEBU YA IMAMIYYAH (ITHNA ASHARIA Na katika madhehbu ya Shia Imamiyyah (ithna-asharia) uimamu unafuatana katika maimamu kumi na mbili, kama wafuatao: 1-Ali bin Abi twalib alie fariki mwaka 40 hijiria. 2-Hasani bin Ali Alie fariki mwaka 50 hijiria. 3-Husein bin Ali alie fariki mwaka 61 hijiria. 4-Ali bin Husein Zainul-aabidiin alie fariki mwaka 94 hijiria. 5-Muhammad bin Ali Al-baqir alie fariki mwaka 114 hijiria. 6-Jaafar bin Muhammad As-swaadiq alie fariki mwaka 148 hijiria. 7-Mussa bin Jaafar Al-kadhim alie fariki mwaka 183 hijiria. 8-Ali bin Musa Ar-ridhaa alie fariki mwka 203 hijiria. 9-Muhammad bin Ali Al-jawaad alie fariki mwaka 220 hijiria. 10-Ali bin Muhammad Al-haadiy alie fariki mwaka 254 hijiria. 11-Hasan bin Ali Al-askariy alie fariki mwaka 260 hijiria. 12-Muhammad bin hasan Al-mahdiy alie zaliwa mwaka 255 hijiria. Na walitoa dalili za kuthibitisha uimamu wao kwa dalili zilizo tajwa kwenye vitabu vya hadithi na vitabu vielezavyo suala la uimamu, na baadhi ya hadithi hizo ni zenye dalili ya wazi juu ya maimamu kumi na mbili, na zingine zikiwa ni dalili juu ya kila mtu mmoja mmoja kidhati yake. Na kati ya dalili hizo ni zile ambazo ni mutawaatir kilafudhi, (zimenukuliwa katika lafdhi moja) na zingine zikiwa ni mutawaatir kimaana.(zimenukuliwa katika maana moja). Na jambo la msingi tulipatalo katika hadithi hizo ni kuwa: Kumfahamu Imamu kunatimia kwa kuthibitishwa kwa dalili ya wazi ya alietangulia kumtambulisha ajae. Pamoja na dalili zile walizozitaja kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ziwaelezeazo wote pamoja na majina yao, na hadithi au dalili tulizo zitaja hapo mwanzo kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) zihusianazo na mtoto wa ami yake Ali bin Abi Twalib (a.s) pekee na walizitolea ushahidi hadithi zilizo pokelewa na Ahli sunna katika vitabu vyao sahihi na Musnadi zao kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ya kuwa Mtume (s.a.w.w) alitoa dalili za wazi ya kuwa maimamu ni kumi na mbili na wote wanatoka katika kabila la kikuraishi. Na katika upokezi wa Bukhari kuna riwaya isemayo: (اثنا عشر أميراً كلهم من قريش ) (Maamiri ni kumi na wawili na wote wanatoka katika kabila la kikuraishi). Na katika upokezi au riwaya ya Muslimu imepokelewa kuwa: (اثنا عشر خليفة كلهم من قريش ) (Makhalifa ni kumi na mbili na wote wanatoka katika kabila la kikuraishi). Na mfano wa hizo ni riwaya za Tirmidhiy na Ibnu Hajar na Bwana Haakim. Na katika riwaya ya Ahmad bin Hanbali kutoka kwa Masrouq, amesema: Tulikuwa tumekaa kwa Abdallah bin Masoud, huku akitusomea Qur'an, mtu mmoja akamwambia: Ewe baba wa Abdur-rahman je mlimuuliza Mtume wa (Mwenyezi Mugnu (s.a.w.w): Ni Makhalifa wangapi watakao miliki na kuutawala umma huu? Abdalah akasema: Hakuna yeyote alie wahi kuniuliza kuhusu suala hilo tangu nilipo kuja Iraq kabla yako wewe. Kisha akasema: Ndio, kwa hakika tulimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), (Nae akasema) Ni kumi na mbili kama idadi ya wateule wa bani Israili). Ustadhi Sayid Muhammad Taqiy Al-hakiim anasema: “Tunacho faidika nacho kutoka kwenye riwaya hizi ni kuwa”: 1-Idadi ya watawala na Makhalifa haivuki watu kumi na mbili, na wote wanatokana na kabila la kikuraishi. 2-Hakika watawala hao wameteuliwa kwa dalili za wazi, kama inavyo lazimu hali ya kufananishwa kwao na wateule wa Bani Israili kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo: (ولقد أخذنا ميثاق بني اسرائيل وبعثنا منهم اثني عشر نقيباً) (kwa hakika tulichukua ahadi kwa bani Israili na tukawatuma miongoni mwao wateule kumi na mbili). 3-Hakika riwaya hizi zimefaradhisha kubakia kwa watawala hawa maadamu uislamu ungali upo, au hadi kitakapo simama kiama, kama riwaya ya Muslimu iliyo tangulia ilivyo elezea, kisha riwaya yake nyingine ikasema wazi katika mlango huo huo kama ifuatavyo: لا يزال هذا الامر في قريش ما بقي من الناس اثنان)) Jambo hili litabakia kuwapo katika kabila la kikuraishi hata kama watabakia watu wawili tu). Ikiwa faida hii tuliyo faidika nayo itakuwa ni sahihi basi haiwiani isipokuwa na itikadi ya Imamiyyah katika idadi ya maimamu na kubakia kwao na kuwa wao wameelezwa na kuteuliwa kwa dalili za wazi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), na natija hiyo itakuwa iko sambamba sana na hadithi ya Thaqalaini (vizito viwili) na kubakia kwao vikiwa pamoja hadi kuingia au kurejea kwake kwenye Hodhi. Na usahihi wa faida hii tuipatayo unategemea juu ya msingi kuwa maana ya kubakia kwa jambo lao kwao ni kubakia kwa uimamu na ukhalifa-kwa kuwa wao ndio wanaostahiki-na sio utawala wa dhahiri. Kwa sababu khalifa wa kisheria huuchukua utawala wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na utawala wake unakuwa katika misingi na mipaka ya utawala wa kisheria si wa kimaumbile, kwa sababu aina hii ya utawala ndiyo ambayo inamlazimu kutekeleza wadhifa wake na kufanya kazi kwa mujibu wa matakwa ya muweka na mtunga sheria, na hilo halipingani na kutoweka utawala wa kidhahiri kwao na kutokuwa nao na kuonekana kidhahiri kwa watu wengine wajitokezao na kuwatawala na kuwakalia kwa mabavu. Na ukweli ni kuwa riwaya zitabakia bila kuwa na tafsiri lau kama hatutazifasiri na kuiacha maana tuliyo ibainisha hapo juu, kutokana na kuwa wazi kuwa utawala wa dhahiri ulichukuliwa na kuendeshwa na watu wa kikuraishi wanaozidi idadi hiyo kwa mara kadhaa, ukiachilia mbali kuanguka na kutoweka utawala na dola lao na yeyote kati yao kuto kuwa na nassi na dalili ya wazi ya kuthibitisha utawala wake-kama vile bani umayyah na bani Abbas- kwa makubaliano ya waislaam wote. Na ni vema kusema ya kuwa riwaya hizi zilikuwa zikipatikana katika vitabu sahihi na masaanidi zao kabla ya idadi ya maimamu kukamilika, kwa hivyo basi hakuna ihtimali ya kuwa huenda zikawa ni riwaya zilizo pandikizwa baada ya kukamilika kwa idadi iliyo tajwa, kwa kujua kuwa wapokezi wake wote ni katika wapokezi wa Ahli sunna na watu wenye kuaminika kwa masunni., Na huenda kutatizwa kwa maulamaa wengi kuzitolea tafsiri na kutoa muelekeo wa hadithi hizi kuwa sambamba kwake na uhakika wa historia ulivyo na ilivyo tokea, chanzo chake kilikuwa ni kutoweza kwao kuzikanusha hadithi hizo, kutokana na hali hiyo ndio maana tunakuta rai zao ni zenye kupingana na kupishana katika kutoa muelekeo na tafsiri ya hadithi hizo na kubainisha maana na makusudio ya hadithi hizo. Na bwana Suyuutwiy (baada ya kutoa maneno yaliyo semwa na maulamaa kuhusiana na hadithi hizi zilizo kuwa ngumu katika kuzifasiri alitoka na rai ya ajabu na tutainukuu hapa ili wasomaji waweze kujishuhudia wenyewe, nayo ni kama ifuatayo: (Na juu ya msingi huu walipatikana kati ya Makhalifa kumi na mbili: Makhalifa wanane na Hasan na Muawiah na ibnu Zubairi na Omar bin Abdul-azizi na hawa ni wanane na kuna ihtimali kujumuishwa na watu hao Mahdiy mmoja kati ya watawala wa Bani Abbasi, kwani yeye kati ya bani Abbas ni kama vile Omar bin Abdul-azizi kati ya bani Umayyah, vile vile kidhahiri kutokana na kusifika kwake na uadifu, na wanabakia wawili wenye kusubiriwa mmoja wapo ni: Mahdiy kwa sababu yeye ni katika Aali na jamaa wa Muhammad) na hakubainisha wa pili anaengojewa na kusubiriwa, na Mwenyeezi Mungu amrehemu yule alie sema maneno yake kuhusiana na bwana Suyuutwiy: Hakika yeye alichanganyikiwa na kutoa fahamu ukweli). Na yasemwayo kutoka kwa Suyuutwiy, husemwa pia kutoka kwa Ruuzbahan katika kumjibu kwake Allama Al-hilliy, nae akijaribu kuzielekeza na kuzitolea tafsiri hadithi hizo. Na ukweli ni kuwa hadithi hizi hazikubali tafsiri yoyote itolewayo isipokuwa muelekeo na tafsiri ya madhehbu ya Imamiyyah kuhusiana na maimamu wao. Na kuzizingatia kuwa ni katika dalili za utume katika ukweli wake katika kueleza habari za ghaibu, ni bora zaidi kuliko majaribio ya kuamsha shaka kuhusiana na hadithi hizo kama walivyo fanya baadhi ya watafiti na wasimuliaji wa hadithi wakizivuka kwa kufanya kwao hivyo kanuni zote za kielimu, na hasa baada ya kuthibiti ukweli wake kwa kuwa kwake sambamba na zikiwiana kwke na maimamu kumi na wawili (a.s)