Change Language: English

Usimamizi mzuri wa Iraq katika kumbukumbu ya Ashura ya Imam Hussein AS

Pamoja na kuwepo makundi hatari ya kigaidi katika maeneo mbali mbali, maombolezo ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake watiifu, yalifanyika kwa mafanikio na usalama kamili nchini Iraq katika mji wa Karbala na kuhudhuriwa na mamilioni ya wafanya ziara.

Siku za tisa na kumi za Muharram pamoja na Arbaeen ya Imam Hussein AS, Imamu wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, ni kati ya hafla muhimu zaidi za Waislamu duniani ambazo hufanyika kila mwaka na kuhudhuriwa na mamilioni wafanya ziara ambao huwasili Iraq kutoka maeneo mbali mbali duniani katika fremu ya misafara kwa lengo la kuadhimisha siku hizo katika mji mtakatifu wa Karbala.

Hafla za Taasua (Tisa Muharram) na Ashura (Kumi Muharram) zilifanyika katika mji wa Karbala Iraq siku za Jumanne na Jumatano na kuhudhuriwa na wafanya ziara takribani milioni tano kutoka Iraq na nje ya Iraq. Mjumuiko huo mkubwa wa kidini umejiri pasina kuwepo tukio lolote la kuhatarisha maisha na jambo hilo ni ishara ya uwezo mkubwa wa vikosi vya usalama vya Iraq pamoja na kuwepo vitisho vya makundi hatari ya magaidi wakufurishaji hasa ISIS au Daesh katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Wakuu wa jeshi na polisi wa Iraq walikuwa wametangaza kuchukua hatua kali za usalama na kwamba maafisa 30 elfu wa usalama wangeongoza wafanya ziara kutoka katika mipaka na miji mbali mbali hadi Karbala.

Karbala, Iraq katika siku ya Ashura

Wakuu wa usalama Iraq wanasema kuwa kulikuwa na zaidi wa walinzi 2000 wa kujitolea wa kundi la kujitolea la wananchi la Al Hashad Al Shaabi ambao walilinda doria katika eneo la magharibi mwa mji wa Karbala linalopakana na mkoa wenye machafuko wa Al Anbar. Eneo kubwa la mkoa wa Al Anbar linakaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi la ISIS lakini kutokana na ulinzi mkali hakukuripotiwa tukio lolote la ukiukwaji usalama katika eneo hilo.

Kutumia makundi ya kujitolea ya wananchi, walinzi wanawake, makachero, ndege zisizo na rubani, vifaa vya kugundua mabomu n.k ni mambo ambayo yamepelekea kupatikana usalama kamili Iraq kuanzia tarehe Mosi Muharram hadi siku ya Ashura ya kukumbuka ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW na wafuasi wake Karbala.

Pamoja na kuwa oparesheni ya kurejea makwao mamilioni ya wafanya zaira ingali inaendelea, lakini usimamizi mzuri wa maafisa wa usalama wa Iraq ni jambo ambalo limepelekea kumbukumbu ya Ashura mwaka huu kufanyika kwa amani ikilinganishwa na miaka iliyipota.

Maafa ya Mina

Hii ni katika hali ambayo, Saudi Arabia, ambayo inahesabiwa kuwa nchi yenye uthabiti na watawala wake kujitangaza kuwa ni wahudumu wa Haram Mbili Takatifu za Kiislamu, wameshindwa kusimamia Ibada ya Hija ambapo Mahujaji huwa hawazidi milioni mbili kwa wastani. Ni kutokana na usimamizi huo mbovu wa Saudia ndio mwaka 2015 tukashuhudia maelfu ya Mahujaji wa nyumba ya Allah SWT wakipoteza maisha katika eneo la Mina na pia katika tukio la kuanguka winchi katika Masjid al Haram.