Change Language: English

Pamoja na Imam Hussein AS kutoka Madina hadi Karbala (1)

Mwezi wa Muharram unatukumbusha mapambano ya Karbala ambayo Imam Hussein (as) alikuwa mbeba bendera wake, mapambano ambayo yameacha athari kubwa katika historia ya mwanadamu. Huenda wewe pia ndugu msikilizaji ukawa unajiuliza swali hili kwamba je, ni nini kilichotokea katika umma wa Kiislamu baada ya kupita miaka 50 tokea kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw), kiasi cha kuufanya uruhusu kutoka kwa tukio chungu la kuuawa kinyama Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Mtume (saw)? Harakati ya Imam Hussein (as) kutoka Madina hadi Karbala nchini Iraq imejaa mafunzo na ibra ambazo zinaweza tu kufahamika kwa kuzingatia kwa makini hotuba na msimamo ya Imam Hussein (as) katika mapambano hayo. Harakati ya Imam Hussein (as) kutoka Madina hadi Makka na kutoka huko hadi Karbala na hatimaye kuuawa katika mapambano ya siku ya Ashura ni mambo yaliyochukua muda wa karibu siku 160. Ili kuepuka kumpa baia Yazid siku 12 baada ya kufaaga dunia baba yake Muawiyya, Imam Hussein aliamua kuondoka Madina kuelekea Makka tarehe 27 Rajab ambapo aliwasili katika mji huo mtakatifu wa Wayhi tarehe 3 Shaaban. Alikaa katika mji huo katika miezi ya Shaaban, Ramadhan, Shawwal na Dhul Qaada hadi tarehe 8 ambapo aliamua kuelekea Karbala kwa lengo la kuanzisha harakati kubwa ya mapambano dhidi ya dhulma kubwa iliyokuwa ikienezwa katika umma wa Kiislamu na utawala mbovu wa wakati huo wa Bani Ummayia. Miongoni mwa masuala muhimu yanayopasa kuchunguzwa kuhusiana na mapambano hayo ni sababu zilizompelekea mtukufu huyo kuamua kusimama dhidi ya dhulma iliyokuwa ikiendeshwa na watawala hao waliokanyaga wazi misingi ya dini.

Matukio yaliyojiri baada ya kuaga dunia Mtume (saw) yanaonyesha wazi kwamba baadhi ya watu walifanya juhudi kubwa za kuhuisha mila na itikadi za kijahili na wengine kuwasaidia kufikia lengo hilo kwa kukaa kimya kutokana na imani zao dhaifu. Licha ya kuwa Mtume Mtukufu (saw) alikuwa ameleta mabadiliko makubwa katika jamii ya Kiislamu kutokana na muujiza wake wa kudumu milele pamoja na shakhsia yake tukufu ya kimaanawi, lakini makundi ya yaliyotaka kuhuisha tabia, desturi na mila za kijahili yalikuwa yamefanikiwa pakubwa katika kuzusha bidaa katika jamii ya Kiislamu. Bidaa hizo zilifikia kilele katika utawala wa Muawiyya na hasa wa mwanawe Yazid.

Katika hali kama hiyo Imam Hussein (as) hangeweza kukaa kimya na kutazama tu dini tukufu iliyoletwa na babu yake Mtume (saw) ikipotoshwa na watu wasiofaa kuwa viongozi wa Kiislamu. Hotuba na maneno pamoja na barua nyingi alizoandika mtukufu huyo katika safari yake kutoka Madina hadi Karbala na kufikia wakati wa kuuawa kwake shihidi katika ardhi ya Karbala, zinaweka wazi matukio machungu yaliyojiri katika zama hizo katika jamii ya Kiislamu na wakati huohuo kubainisha wazi malengo ya Imam Hussein katika kuanzisha mapambano yake dhidi ya makundi hatari yaliyotaka kupotosha malengo na ujumbe wa dini tukufu ya Kiislamu. Ili kunufaika na baadhi ya hotuba na maneno ya Imam Hussein (as) tokea mwanzoni mwa safari yake mjini Madina kuelekea Makka na kisha Karbala, tunaashiria hapa baadhi ya hotuba hizo.

Muawiya alipokufa katikati ya mwezi Rajab mwaka wa 60 Hijiria, mwanawe Yazid alitwaa ukhalifa na kuwaandikia barua magavana na makamanda wa maeneo mbalimbali ya ardhi ya Kiislamu kuhusiana na suala hilo. Aliwabakisha kwenye nyadhifa zao hizo na kuwataka wawakusanye watu waliokuwa chini ya mamlaka zao na kuwalazimisha wampe baia na kumtii kama khalifa wa umma wa Kiislamu. Alimwandikia barua kama hiyo Walid, gavana wa Madina, lakini akaongeza barua nyingine ndogo pembeni yake, ambapo alimtaka achukue beia kutoka kwa shakhisa wengine watatu mashuhuri wa mji huo ambao hawakuwa tayari kumbai Yazid wakati wa uhai wa Muawiya. Shakhsia hao watatu walikuwa, Hussein bin Ali, Abdallah bin Omar na Abdallah bin Zubeir. Yazid alimtaka Walid achukue beia kwa njia yoyote ile kutoka kwa shaksia hao bila kuwapa fursa ya kukwepa.

Baada ya kupokea barua hiyo Walid alimshauri Marwan bin Hakam aliyekuwa gavana katika utawala wa Muawiya na kwa pamoja wakaamua wawatake shakhsia hao wafike kwenye baraza la Walid na kumbai Yazid kabla habari za kifo cha Muawiya hazijaenea mjini. Walid alipomtaka Imam Hussein ambai Yazid, Imam alimjibu kwa kusema: "Sisi ndio kizazi cha Mtume na chimbuko la ujumbe (wa Mwenyezi Mungu). Kizazi chetu ndipo mahala pa kuteremka na kupaa malaika na sehemu ya kuteremka rehema ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu aliuanzisha Uislamu kwenye kizazi chetu na atauendeleza kupitia kwetu. Ama kumhusu Yazid, mtu huyu ambaye unatarajia mimi nimbai, ni mnywaji pombe ambaye mikono yake imejaa damu ya watu wasio na hatia. Huyu ni mtu ambaye amevunja sheria za Mwenyezi Mungu na kufanya ufuska na ufisadi waziwazi mbele ya watu. Je, inafaa kwa mtu kama mimi aliye na historia inayong'ara na chimbuko la kizazi safi kama hiki kumbai mtu kama huyu fasidi? Nyinyi na sisi tunapasa kuutazama mustakbali kuhusiana na suala, ili tupate kutambua ni nani kati yetu ni mbora na anayefaa kupewa beia ya kuwa khalifa na kiongozi wa umma wa Kiislamu."

Kwa maneno hayo, Imam Hussein aliweka wazi kabisa msimamo wake kuhusiana na beia ya Yazidi mwana wa Muawiya na uamuazi wake wa kutotambua rasmi utawala wake. Kwa kutaja sifa zake bora na za kizazi chake, na wakati huohuo kuweka wazi upotofu na ufuska wa Yazid, Imam Hussein (as) aliwataka Waislamu kutambua na kuzingatia hali hizo mbili na kuona ni nani kati yake na Yazid alifaa kuwa kiongozi wa umma wa Kiislamu. Kwa hutuba hiyo Imam Hussein (as) alitaka kuvunja njama za watu waovu ambao walitaka kupora na kudhibiti matukufu ya Waislamu na kueneza ufuska na ufisadi katika jamii yao. Imam Hussein alitambua vyema kwamba Yazid alitaka kufikia malengo ya ukoo wa babu yake Abu Sufyan ya kupambana na Uislamu na Qur'ani Tukufu, kupitia unafiki alioufunika kwa vazi la Uislamu.

Ni wazi kuwa kulikuwepo na watu mashuhuri walioonyesha wasiwasi mkubwa kuhusiana na msimamo huo wa Imam Hussein (as) akiwemo Muhammad bin Hanafiya, mmoja wa wana wa Imam Ali (as). Kwa mujibu wa riwaya iliyonukuliwa na Tabari na wanahistoria wengine mashuhuri, Muhammad Hanafiya alimwendea Imam Hussein (as) na kumshauri yeye na familia yake wahamia sehemu ya mbali ambapo haingelikuwa rahisi kwa Yazid na vibaraka wake kumfikia, na kisha atume wajumbe wake kwa watu ili wapate kumbai. Alisema kama wangelimbai ingelikua ni sawa na kheri kwake na kama wangelikataa kufanya hivyo, bado asingelidhurika kutokana na njama za Yazid.

Katika kumjibu Imam (as) alimwambia: "Kaka! Elewa kwamba hata kama nitakosa sehemu ya kujificha katika dunia hii pana, bado sitambai Yazid bin Muawiya." Baada ya Imam Hussein kuona kwamba ndugu yake Muhammad Hanafiya alikuwa akimtakia kheri kwa kumsisitizia akimbilie sehemu nyingine ili apate kuokoa roho yake, alimjibu kwa kusema:

"Kaka! Mwenyezi Mungu akulipe heri kwa kutekeleza wadhifa wako wa kunitakia wema. Ama mimi (ninafahamu vyema majukumu yangu kukuliko) nimeamua kwenda Makka, na mimi, ndugu zangu na watoto wao pamoja na wafuasi wangu kadhaa tumejiandaa kwa ajili ya safari hii. Hii ni kwa sababu watu hawa wanaafikiana na mimi, na lengo na matakwa yao ni sawa na lengo na matakwa yangu. Ama jukumu lako wewe ni uendelee kubaki mjini Madina na kuchunguza kwa karibu nyendo za siri za vibaraka wa Bani Umayia nitakapokuwa nimeondoka, na hatimaye unipashe habari zao."

Kabla ya kuelekea Makka na kuanza kukabiliana moja kwa moja na utawala wa Yazid, Imam Hussein (as) alizuru mara nyingi, kuliko kawaida, kaburi la babu yake, ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na kuomba dua nzito za kimaanawi kuhusiana na umma wa Kiislamu. Katika dua hizo Imam (as) aliashiria umuhimu wa safari yake ya kupambana na dhulma na kusisitiza kwamba alipendezwa mno na mambo ya kheri na kuchukizwa na ya shari na munkari. Alimwomba Mwenyezi Mungu amuwezeshe kupambana na batili na kumfanikisha katika kudhihirisha haki na wema kwa maslahi ya umma wa Kiislamu, hata kama jambo hilo lingemlazimu kutoa maisha yake ili kufikia lengo hilo.