Mchango wa Wanawake katika Hamasa ya 'Ashura
Bismillahir Rahmanir Rahim. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika sehemu ya kwanza ya makala hii inayozungumzia mchango wa wanawake katika hamasa wa 'Ashura. Mwezi wa Muharram mwaka 61 Hijria ulipambika kwa mapambano ya kishujaa ya Imam Husain AS na wafuasi wake. Mapambano hayo ya yaliyopelekea kumwagika damu nyingi, yalikuwa na lengo la kuwaamsha watu na kuleta marekebisho katika jamii ya Kiislamu ambayo ilikuwa chini ya utawala kandamizi wa mtawala dikteta ambaye hakujali matukufu ya Kiislamu. Imam Sadiq AS anasema hivi katika Ziara ya Arubaini ya Husain kwamba: "Damu yake (Imam Husain AS) aliimwaga katika njia Yako (Ewe Mwenyezi Mungu) ili awatoe waja Wako katika ujinga, kuchanganyikiwa na kupotea."
Wakati wanawake wa Bani Hashim waliposikia kuwa Imam Husain AS ameazimia safari, waliitisha kikao cha pamoja ili kutaamali nini cha kufanya. Walikuwa na yakini kwamba Imam Husain AS hatorejea salama katika safari yake hiyo. Akinamama hao waliamua kutumia vilio na hisia za kuungulika mtimani ili kuonyesha majonzi yao ya nyoyoni. Imam Husain akajongea karibu nao na kuwasemeza akiwaambia: "Nakunasihini kwa Dhati ya Mwenyezi Mungu, Allah Allah msije mkaitangaza habari hii, ikaja ikawa ni kukhalifu amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake."
Akinamama wa Banii Hashim wakanena: Vipi tutahimili kujizuia kulia wakati siku hii ya leo kwetu ni sawa na siku alipofariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, ni sawa na siku alipouawa shahidi Ali na Faatima na ni mithili ya siku walipofariki dunia Ruqayyah, Zaynab na Ummukulthum, mabinti wa Bwana Mtume SAW? Husain wetu mpendwa! Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba tuachie tutoe fidia roho zetu kwa ajili yako ili wewe ubakie salama, tunakuomba kwa kusisitiza ewe mpendwa wa waja wema unayetutoka...
Nasaha za Imam Husain AS hazikusadia kitu na hazikuwanyamazisha akinamama wa Bani Hashim. Akinamama hao wakaelekea kwa Ummu Hani, shangazi wa Imam Husain AS na kumwambia: Ummu Hani! Vipi umekaa kimya wakati Husain na aila yake ndio hao tena wanakwenda?!
Ummu Hani akatoka kwa haraka sana kuelekea kwa Imam Husain. Baada ya kumuona tu, Imam alimwambia: Shangazi yangu mpendwa, kwa nini uso wako umesawijika kiasi chote hiki?
Ummu Hani akasema: Vipi nisisawijike wakati naona mlezi wa mayatima na watu wasio na pa kwenda, ananitoka?
Huku akishindwa kujizuia kububujikwa na machozi, Ummu Hani akaanza kutoa sifa za Husain AS akinena: Husain ni shakhsia tukufu ambaye watu wanaomba kupata baraka za mvua kwa utukufu wake. Husain ni chemchemu ya furaha za mayatima na ni mlezi wa watu wasio na pa kukimbilia. Husain ni katika kizazi cha Hashim ambaye anajitolea muhanga kwa ajili ya wengine. Wakati wanyonge walineemeka kwa fadhila na ukarimu yake, Husain pia, ni kipenzi cha Mtume wa Allah SAW. Husain hakosei na huu msiba mkubwa (wa kuuawa kwake shahidi), unabainisha wazi utukufu wa sira yake."
Imam Husain AS akamwambia: "Shangazi yangu mpenzi! Usiwe na wasiwasi halilatotokea ila lililopangwa na Mwenyezi Mungu. Watu hao hawawezi kumshinda mwana wa mshindi wa vita vyote (yaani mwana wa Imam Ali AS). Masuala haya yanakwenda kwa qudra na elimu ya ghaibu ya Mwenyezi Mungu."
Akinamama wa Bani Hashim ambao walimaizi kuwa Uislamu ulikuwa umefikishwa mahala ambapo usingeliweza kuokoka ila kwa kujitoa muhanga Imam Husani AS, walijitolea kwa roho na nyoyo zao kuandamana naye kuelekea kwenye medani ya mapambano.
Tarikh ya Uislamu ya tangu kudhihiri kwake, muda wote imeshuhudia mchango mkubwa wa akinamama katika medani za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi. Nafasi muhimu ya wanawake katika kila lahdha na sekunde ya historia ya Uislamu ni kitu kisichoweza kukanushika kabisa. Mapambano ya Karbala ni katika matukio muhimu na ya aina yake kabisa katika tarikh ya Uislamu. Mapambano hayo ni matunda ya pamoja ya ushujaa na kujitolea muhanga wanawake kwa wanaume katika njia ya Haki. Kwa maneno mengine ni kuwa, kama Uislamu ulihuishwa kwa mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala, basi mchango mkubwa wa mapambano hayo ulitolewa na wanawake ambao hawajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia. Wanaume wote walioonyesha hamasa ya kupigiwa mfano huko Karbala walipata malezi kutoka kwa akinamama mashujaa waliopambika vizuri kiimani na weledi wa mambo, ambao walipata taufiki ya kuitunuku jamii ya Kiislamu watu mashujaa kama hao. Hivyo kuweko wanaume kama hao kwenye vita hivyo visivyo na mlingano sawa vya Karbala ni matunda ya kujitoa muhanga na kuwa na muono wa mbali akinamama. Subira na istikama ya wanawake waliokuwemo kwenye msafara wa Imam Husain AS nayo ilitoa mchango mkubwa sana kwa wafuasi wa Imam Husain AS waliopambana kiume hadi tone la mwisho la damu zao. Mchango huo wa akinamama ulianza hata kabla ya kuuawa shahidi Imam Husain AS kwa njia isiyo ya moja kwa moja na ulianza kwa kuwahamasisha waume na watoto wao kushiriki kwenye mapambano hayo matakatifu licha ya kujua kwamba wangeliuawa shahidi na mchango wao ulionekana zaidi baada ya tukio la 'Ashura ambapo akinamama hao walifanya kazi kubwa ya kutangaza malengo matukufu ya mapambano ya Karbala.
Wanawake wa Karbala walithibitisha kivitendo kuwa majukumu ya kijamii hayawahusu tu wanaume. Kila linapojitokeza suala la kuilinda dini na kusimamisha haki; wanadamu wote – iwe wanawake au wanaume – kila mmoja ana jukumu la kutoa mchango wake. Tab'an katika Uislamu si wajibu kwa wanawake kushiriki katika medani za mapambano na jihadi. Hata katika medani ya Karbala pia Imam Husain hakuwaingiza wanawake katika medani ya vita na ndio maana wanawake hawakushiriki kijeshi katika 'Ashura. Ni wanawake wawili tu ndio waliokwenda kwenye medani ya vita, lakini Imam Husain AS aliwashukuru na kuwaondoa kwenye medani hiyo. Mchango mkubwa wa akinamama katika kadhia ya Karbala ulikuwa ni kufikisha ujumbe wa mapambano hayo kwa walimwengu.
Kiujumla tunaweza kuugawa mchango wa wanawake kwenye hamasa ya Karbala katika mafungu matatu. Kabla ya 'Ashura, siku ya 'Ashura na baada ya 'Ashura.
Dulham, alikuwa mke wa Zuhayr ibn Qayn. Dulham alikuwa miongoni mwa wanawake ambao waliwahamisisha waume zao wajiunge na msafara wa Imam Husain AS katikati ya njia. Nafasi ya Dulham ilikuwa muhiumu kiasi kwamba kisa chake na mumewe Zuhayr ni vizuri nikikusimulieni hapa.
Wakati Zuhayr ibn Qayn alipokuwa anarejea kwao Iraq pamoja na kundi la watu wengine kutoka Makka walikotekeleza ibada ya Hija, alipata taarifa kuwa Imam Husain AS alikuwa amekataa kutoa bay'a na kutangaza utiifu wake kwa mtawala dhalimu wa wakati huo, Yazid bin Muawiya. Alipata taarifa pia kuwa Imam Husain alikuwa anaelekea Iraq na wafuasi wake na alikuwa na yakini kwamba uamuzi uliochukuliwa na Imam Husain AS ulikuwa wa haki, lakini hakutaka kuchanganya utamu wa ibada yake ya Hija na uzito wa vita na mapambano. Hivyo akajitahidi kadiri alivyoweza, ukwepa kukutana na msafara wa Imam Husain AS. Ikawa kila msafara wa Imam Husaini ulipokuwa ukipumzika, msafara wa Zuhayr uliendelea na safari na kila msafara wa Imam Husaini ulipoendelea na safari, msafara wa Zuhayr ulipumzika. Wakati msafara wa Zuhayr ulipokuwa amepiga kambi eneo la mbali na sehemu ya mahema yalipokuwepo Imam Husain kwa ajili ya kupumzika na kula chakula, ghafla Zuhayr alimuona mjumbe wa Imam Husain AS amefika kwake akimtaka Zuhayr aende kwa Imam. Watu wote waliokuwemo kwenye msafara huo wakapigwa na bumbuwazi na kila mmoja akawa anamuangalia mwenzake machoni. Zuhayr akajifanya hakusikia. Hapo hapo mke wa Zuhayr, yaani Dulham, binti wa Amru aliwashangaza wote aliposimama na kusema: Subhanallah! Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW amekutumia mjumbe uende kwake wewe hutaki kwenda?! Unaogopa kitu gani, nenda ukamsikilize anachokuitia, hiyo ndiyo busara. Maneno hayo yalimlainisha Zuhayr na kumfanya aitikie mwito wa Imam. Aliporejea, uso wake ulionekana umejaa nuru, akamtaka mke wake amkusanyie vitu vyake ili aende akajiunge na msafara wa Imam Husain AS. Hata hivyo akamwambia mkewe kwamba, hataki afikwe na chochote kibaya mikononi mwake, hivyo anampa talaka ili arejee kwa wazee wake. Lakini Dulham alikuwa na mapenzi makubwa kwa mumewe, walikuwa wameishi pamoja kwa miaka mingi, maneno ya mumewe ya kumpa talaka yalimchoma na kumuumiza sana. Hata hivyo mapenzi yake kwa mumewe hayakuwa chochote mbele ya matakwa ya mwana wa Mtume. Alichosema Dulham kumwambia mumewe ilikuwa: "Natawakali kwa Mwenyezi Mungu. Namuomba anisaidie na akusaidie na wewe. Nakuomba siku ya Kiama unishike mkono na kunipeleka kwa Aba Abdillahil Husain AS ili aniombee shufaa."
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.