Change Language: English

Mamilioni ya Waislamu waadhimisha Arubaini ya Imam Hussein as Karbala Iraq

Mamilioni ya Waislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia leo wameshiriki katika shughuli ya Siku ya Arubaini ya Imam Hussein (as) katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq.

Maadhimisho hayo ambayo hukumbusha siku ya arubaini baada ya kuuawa mjukuu huyo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw), jamaa na masahaba zake katika medani ya Karbala mwaka 61 Hijria katika vita baina ya haki na batili, yamefanyika chini ya uangalizi mkali wa usalama.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Iraq imesema kuwa, zaidi ya wafanyaziara milioni tatu kutoka Iran na nchi nyingine, waliingia nchini humo siku chache zilizopita kwa ajili ya kumbukumbu hizo, huku wengine zaidi ya milioni 17 wakitoka miji tofauti ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Maadhimisho ya Arubaini ya Imam Hussein as katika mji wa Karbala, Iraq

Waislamu kutoka Iran, Bahrain, Saudia, Qatar, Kuwait na nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya, waliwasili nchini humo kwa ajili ya maombolezo hayo. Jeshi la Iraq limetangaza kuwa zaidi ya askari elfu 30 wa usalama wamesimamia usalama katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu. Kabla ya kufika mjini Karbalaa, wafanya ziara hufanya matembezi ya miguu kwa kilometa kadhaa, kumuenzi Imam Hussein (as) na watu wake wa karibu waliouawa kikatili na jeshi la mtawala dhalimu Yazid Mwana wa Muawiya mwaka 61 Hijiria, katika jangwa la Karbala.

Takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 25 wameshiriki katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein as mwaka huu.