Mafundisho ya Imam Hussein AS (5)
Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya makala hii maalumu ya Mafundisho ya Imam Hussein AS, ambayo inakujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mapambano ya mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS ambaye alisimama na wafuasi wake katika ardhi ya Karbala mwaka 61 Hijria kukabiliana na jeshi ovu la mtawala dhalimu na mwovu Yazid bin Muawiya. Karibu kutegea sikio sehemu ya tano ya mfululizo huu.
Kwa hakika Imam Hussein AS alikuwa mrithi wa sifa njema za kiakhlaqi na kimaadili za Mtukufu Bwana Mtume SAW. Kama alivyokuwa babu yake, Imam Hussein pia alikuwa akitaabika na kuumia mno na kuona watu wakikengeuka na kupotoka. Imam Hussein AS alikuwa akihuzunika mno kuona watu wakikengeuka njia ya haki na kupita katika njia batili na ya ukafiri Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana licha ya kutambua kwamba, maadui walikuwa wakipuuza maneno yake, lakini alijitahidi kutoa nasaha hadi katika lahadha za mwisho na kuwaonea huruma.
اَلسَّلامُ عَلَیْکَ یا وارِثَ مُحَمَّدٍ حَبیبِ اللَّهِ
Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yako ewe mrithi wa Muhammad kipenzi cha Mwenyezi Mungu.
Kwa hakika Mtume SAW alikuwa akiumia sana alipokuwa akiona ujahili na upotofu ambapo Mwenyezi Mungu aliteremsha aya ya 3 katika Surat Shuaraa na kumliwaza akimwambia:
Huenda utaangamiza nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.
Kwa hakika Imam Hussein AS ni matunda ya mti wa risala ya Mtume SAW. Yeye ni mrithi wa Mtume na sehemu ya uwepo na ujudi wa Bwana Mtume SAW. Bwana Mtume SAW amenukuliwa aisema:
حُسَیْنٌ مِنِّی وَ أَنَا مِنْ حُسَیْنٍ
"Hussein anatokana na mimi na mimi ni ninatokana na Hussein".
Katika siku ya Ashura, licha ya Imam Hussein kukabiliwa na uadui wote ule na ukatili kutoka kwa maadui ambao walikuwa wakizuia kufikishiwa hata maji watoto wachanga na familia ya Imam Hussein AS, alikuwa akiwausia na kuwanasihi. Licha ya makelele ya jeshi la adui Yazid bin Muawiya, Imam Hussein alikuwa akiwahutubia na kuwanasihi. Kila neno katika hotuba yake lilikuwa na maana pana na mafuhumu ya ndani na ilihitajia tafisiri na ubainishaji.
Licha ya jinai za maadui, lakini Imam Hussein hakuacha kuwanasihi makamanda wa jeshi la Yazid mlaaniwa.
Lengo la Imam Hussein lilikuwa ni kuwaokoa watu waliohadaiwa na kuuza utu na dini yao ambao wasingepata lolote kwa kumuua shahidi Imam Hussein bighairi ya kujipalilia adhabu na kujiandalia makazi katika moto wa Jahanamu.
Katika siku ya Ashura wakati alipoonana na Omar bin Saad baina ya safu za majeshi mawili Imam Hussein alisema:
Ole wako ewe mwana wa Saad! Humuogopi Mwenyezi Mungu ambaye utarejea kwake? Pamoja na kutambua kwamba, mimi ni mtoto wa nani, bado unapigana na mimi? Achana na kaumu hiyo na uwe pamoja nami ili ujikurubishe kwa Mwenyezi Mungu."
Maneno haya yenye huruma ya Imam Hussein AS licha ya kuwa hayakuwa na athari katika nyoyo za wengi katika jeshi lile katili, lakini walikuwemo watu ambao waliyakubali maneno hayo na hivyo wakajiunga na jeshi la Imam Hussein na mintarafu hiyo wakapata saada ya milele na utukufu wa kudumu. Mbinu hii ya kuongoza ya mrithi wa Mtume hakuaiacha na kughafilika nayo hata katika lahadha na wakati nyeti kabisa.
Ukweli ni kuwa, Imam Hussein AS ni fimbo ya Utume na matunda ya mti wa Uimamu ambapo sira na mwenendo wake wa kimaadili unaonyesha thamani aali za Qur'ani. Katika upande wa sifa njema, alikuwa amebobea zaidi kati ya watu wa zama zake, na katika utukufu, uungwana, wema na kadhalika, ni mambo yaliyomshangaza rafiki bali hata adui yake. Kuweko bahari ya uungwana, wema na hisani katika chombo kidogo cha akili na kalamu zetu ni jambo ambalo haliwezekani, lakini kutoa wasifu wa sifa zake njema ni jambo linalokata kiu chetu.
Inanukuliwa katika historia kwamba, Bwana mmoja mwenyeji wa Sham (Syria ya leo) ambaye alikuwa na chuki na uadui mkubwa moyoni mwake dhidi ya Ahlul Bayt AS na Imam Hussein AS kutokana na propaganda chafu za Muawiya dhidi ya dhuria wa Mtume SAW alifanya safari katika mji wa Madina. Alipokutana na Imam Hussein alianza kumshambulia kwa matusi na maneno ya kashfa na dharau. Imam alimtazama kwa huruma na mapenzi na kumwambia: Endapo utanitaka msaada nitakusaidia na kama kuna kitu unataka nitakupatia na vile vile kama unataka maelekezo na muongozo basi sitasita kukupatia."
Bwana yule mtoa matusi, alitahayari na kuona haya na kutokana na kuwa Imam aliona katika uso wake hali ya kujutia akamwambia:
Lawama na majuto hayapaswi kuwa kwako, Mwenyezi Mungu akurehemu kwani Yeye ndiye Mwingi wa rehma. Bwana yule wa Sham akaingiwa na soni na haya kubwa na kuondoka hali ya kuwa, alikuwa akihisi joto la huba na mapenzi ya Ali AS na Ahlul Bayt AS.
Dhihirisho bora kabisa la uungwana linaweza kushuhudiwa katika muamala mfano wa Imam Hussein AS katika tukio la Karbala. Msafara wa Imam Hussein ukiwa njiani kuelekea katika mji wa Kufa njiani ulikutana na jeshi la Hurr bin Yazid al-Riyahi. Jeshi hilo lilikuwa limepewa amri ya kumfungia njia na kumzuia Imam Hussein na kumuacha katika ardhi kavu isiyo na maji wala majani. Lakini wanajeshi wa Hurr bin Yazid al-Riyahi wenyewe pia walikumbwa na kiu kikali baada ya akiba ya maji waliyokuwa nayo kumalizika. Imam Hussein alitoa amri wanajeshi hao na hata vipando vyao vipatiwe maji. Mmoja wa wanajeshi wa jeshi la adui ambaye alifika amechelewa alikuwa na kiu kikali kiasi kwamba, hakuwa na nguvu hata za kushuka kutoka katika kipando chake ili anywe maji. Imam alishuhudia hali hiyo, hivyo alimuedea na alipomkaribia alimlaza mnyama wake chini kisha akamnywesha maji askari yule. Lakini maadui hao hao siku ya Ashura walizuia kupatiwa maji hata mtoto mdogo wa miezi sita wa Imam Hussein katika jangwa la Karbala na badala yake walikilenga kwa mishale kikoromeo na koo lake dogo kuliko mshale wenyewe akiwa katika mikono ya baba yake na kumuua shahidi.
Uungwana mwingine wa Imam Hussein AS ni ule ulioshuhudiwa alasiri ya siku ya Ashura. Wakati maadui walipokuwa wamefikia katika kilele cha ukatili na uovu wao huku wakiwauwa hata watoto wadogo kabisa wasio na hatia, Imam Hussein AS hakuacha kuonyesha uungwana wa hali ya juu hata katika mazingira magumu kama ya medani ya vita, uungwana ambao unatukumbusha uungwana wa baba yake yaani Imam Ali bin Abi Twalib AS.
Tamim bin Qahtabah mmoja wa wapiganaji wenye nguvu wa jeshi la adui wakati alipokuwa akipigana na Imam Hussein AS alipoteza mguu wake mmoja na kuanguka chini. Qahtabah ambaye alikuwa akiyaona mauti mbele yake alimuomba Imam Hussein ampe amani na asimuue. Imam akampa amani na kwa kuitikia takwa la Tamim aliruhusu jeshi la adui kumchukua na kumpeleka katika kambi yao. Hii ni katika hali ambayo, Imam Hussein na watu wa nyumba yake walikuwa na machungu makubwa kutokana na jinai za jeshi la Yazid huku watoto wadogo wakiwa wanataabika kwa kiu kikali baada ya maadui kuwanyima maji. Pamoja na hayo yote, Imam Hussein alionesha uungwana mkubwa na kuamiliana namna hii na adui aliyekuwa amejeruhiwa katika medani ya vita.
Baada ya masahaba wote wa Imam Hussein As kuuawa shahidi na Imam kushuhudia kuuawa shahidi watoto na masahaba wake wote alichukua uamuzi wa kuingia yeye mwenyewe katika medani ya vita ili akapambane na maadui ambao walikuwa wameazimia kumuua.
Imam alianza kwa kutoa mwito akasema: "Je kuna mtetezi atakayeitetea heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w)?"
"Je kuna mchamungu amuogopaye Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu sisi? (kizazi cha Mtume)."
"Je yupo mwenye kutoa msaada hali ya kuwa anatarajia mema kwa Mwenyezi Mungu katika kutusaidia sisi?"
"Je kuna mwenye kutunusuru ambaye anatarajia radhi ya Mwenyezi Mungu kwa kutunusuru sisi?"
Mwito huu wa Imam Husein (a.s.) uliwafanya wanawake waliokuwepo hapo walie kwa sauti na makelele mengi yakasikika.
Imam Hussein (a.s.) akaenda mpaka kando ya hema walikokuwa wanawake akamwambia dada yake yaani Bibi Zaynab: "Hebu nipe huyo mwanangu mdogo Ali Asghar ili nimuage.
Imam Husein (a.s.) akamchukua mtoto huyo na kumkumbatia. Kisha Bibi Zaynab akasema, Ewe kaka yangu, mtoto huyu ana kiu, muda mrefu hajanywa maji. Liombe jeshi la maadui maji japo kidogo ili tumpatie mtoto huyo ambaye midomo yake imekauka kutokana na kiu kikali. Imam Hussein akiwa amemnyanyua juu mtoto wake mchanga Ali Asghar aliwahutubu maadui na kuwaambia, muoneeni huruma mtoto huyu mchanga, kwani hamuoni kwamba, anafungua na kufunga midomo yake kutokana na kiu kikali? Imam Hussein kabla hajamaliza kusema maneno hayo, Harmalah bin Kahil al-Assadi kwa amri ya Omar bin Saad akamlenga kwa mshale mtoto yule, ukampata shingoni akamuua.
Kuuawa shahidi mtoto mchanga wa Imam Hussein Ali Asghar kulimuumiza sana Imam, kiasi kwamba, alilia kwa uchungu na akapaza sauti akimwambia Mwenyezi Mungu:
"Ewe Mwenyezi Mungu, tuhukumu baina yetu na watu hawa, wameniita ili nije niwasaidie, lakini sasa wamejipanga kwa ajili ya kuniua."
Kisha Imam Husein akamwambia Bibi Zainab mchukue mtoto huyu kisha Imam akakinga viganja vyake, damu ya mwanaye ikawa inatiririka katika viganja. Pindi viganja vyake vilipojaa damu, Imam aliirusha damu ile juu mbinguni kisha akasema "kila msiba utakaonipata sio mzito kwangu mimi; kwa kuwa yote yanatendeka mbele ya (macho ya) Mwenyezi Mungu Mtukufu".
اَلسَّلامُ عَلَیْکَ یا اَبا عَبْدِاللهِ وَعَلَى الاَرْواحِ الَّتی حَلَّتْ بِفِنائِکَ عَلَیْکَ مِنّی سَلامُ اللهِ اَبَداً ما بَقیتُ وَبَقِیَ اللَّیْلُ وَالنَّهارُ وَلا جَعَلَهُ اللهُ آخِرَ الْعَهْدِ مِنّی لِزِیارَتِکُمْ ، اَلسَّلامُ عَلَى الْحُسَیْنِ وَعَلى عَلِیِّ بْنِ الْحُسَیْنِ وَعَلى اَوْلادِ الْحُسَیْنِ وَعَلى اَصْحابِ الْحُسَیْنِ
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh