Change Language: English

Mafundisho ya Imam Hussein AS (4)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo inakujieni katika siku hizi za msiba mkubwa, siku za kukumbuka kuuawa shahidi Mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake 72 Siku ya Ashura katika jangwa la Karbala.

Imam Hussein AS aliondoka usiku nyumbani kwake katika mji wa Madina kuelekea katika eneo salama la Haram takatifu ya Mwenyezi, lakini katika ardhi hiyo ya amani, hapakuwa na usalama kwa wana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW na hivyo walilazimika kuondoka Makka na kuelekea Kufa, katika Iraq ya leo.

Katika kipindi chote cha safari hii yake, Imam alikuwa ameandamana na familia yake. Alikuwa akifahamu kuwa, akiondoka Madina pasina kuandamana na familia yake, Yazid angewasumbua Ahlu Bayt wa Mtume SAW na kuwatumia kama wenzo wa kumshinikiza Imam.

Tabia bora za Maasoumina AS, ni bahari ya hekima zenye thamani kama lulu. Moja ya mandhari bora zaidi ya Sira ya Maasoumina AS ni muamala wao mzuri na familia zao. Namna walivyoamiliana na wake zao na watoto wao ni nukta inayoweza kuwa njia muafaka ya kutatua matatizo mengi ya jamii ya mwanadamu hii leo. Imam Hussein AS katika cheo chake cha Kiirfani na daraja ya juu aliyonayo mbele ya Mola Muumba, hakusita kubainisha mapenzi na mahaba yake kwa mke na watoto wake. Imam Hussein AS alitunga shairi mashuhuri sana kumhusu mke wake, Bi. Rabab na bintiye, Sukaina. Sehemu ya shairi hilo inasema : "Mimi ninaipenda nyumba ambayo Sukaina na Rabab wamo ndani yake. Nawapenda hao wawili na nitatoa mali yangu yote katika njia hii. Sitakubali waachwe pasina kuzingatiwa katika maisha yangu yote, hadi pale nitakapozikwa katika ardhi." Katika upande wa pili, Bi. Rabab naye baada kuuawa Shahidi Imam Hussein AS alisoma Shairi lifuatalo la maombolezo: "Ewe Mwenye mwangaza ambao ni chanzo cha nuru, umeuawa shahidi na kiwiliwili chako bado hakijazikwa Karbala. Ulikuwa jabali ambalo nilitegemea, na ulitutendea wema na ukarimu kwa mujibu wa dini. Je, baada yako ni nani atawaangalia mayatima, ni nani atakuwa muangalizi wa wanaohitajia, na ni nani ambaye atakuwa kimbilio la wasiojiweza".

Imam Hussein AS, alikuwa na mahaba makubwa na ya kuvutia kwa mke wake na alikuwa akimzingatia kwa njia maalumu na hili ni jambo ambalo lilipelekea hata baadhi ya masahaba na marafiki zake kumkosoa, Lakini pamoja na hayo, Imam alikuwa akiheshimu matakwa halali ya mke wake na alikuwa akiwapa wafuasi wake funzo kuhusu hilo. Katika riwaya tunasoma kuwa, watu walifika nyumbani kwa Imam Hussein AS, na wakaviona vitu vyake vya nyumbani ni maridadi na vya kupendeza kisha wakasema: "Ewe Mwana wa Mtume SAW! Katika nyumba yako tunaona vitu ambavyo havituridhishi, "Mtukufu huyo akasema: "Wake zetu, kwa mahari yao, hununua kile wanachopenda. Hakuna chochote unachokiona hapa ni milki yangu." Kwa kauli yake hiyo, Imam aliwaonyesha wafuasi wake kuwa familia huimarika kwa kuzingatia matakwa halali ya mwanamke na kwamba jambo hilo ni katika masuala ya dharura maishani.

Imam Hussein AS katika siku ya Ashura, wakati wa mapambano, alikuwa akirejea mara kwa mara katika hema za msafara wake huku akiwatolea wito wasichana na wanawake hapo kuwa watulivu na wenye subira. Wakati wa kuagana katika Siku ya Ashura, Sukaina, Bintiye Imam Hussena AS alikuwa akilia huku akiwa amejawa na majonzi. Imam AS Alimkumbatia bintiye azizi na kumbusu kisha akayafuta machozi yake. Alisoma shahiri ambalo tunalifasiri ifuatavyo: "Ewe Sukaina kipenzi! Fahamu kuwa baada ya mimi kuuawa shahidi utalia sana. Kwa hivyo usiniumize kwa kilio chako; maadamu mwili wangu haujatenganika na roho. Wakati nitakapouawa, wewe utakuwa karibu nami zaidi ya wote, hivyo wakati huo njoo pembeni yangu ulie, ewe mwanamke mteule!"

@@@@

Imam Hussein AS hakuwa na njia zaidi ya mbili, kwanza ima ambai Yazid, mtu ambaye alikuwa ni mfisadi na khabithi, kama Khalifa wa Waislamu au auawe.

Imam Hussein AS aliondoka usiku nyumbani kwake katika mji wa Madina kuelekea katika eneo salama la Haram takatifu ya Mwenyezi, lakini katika ardhi hiyo ya amani, hapakuwa na usalama kwa wana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW na hivyo walilazimika kuondoka Makka na kuelekea Kufa, katika Iraq ya leo.

Katika kipindi chote cha safari hii yake, Imam alikuwa ameandamana na familia yake. Alikuwa akifahamu kuwa, akiondoka Madina pasina kuandamana na familia yake, Yazid angewasumbua Ahul Bayt wa Mtume SAW na kuwatumia kama wenzo wa kumshinikiza Imam. Kwa msingi huo Imam aliwaweka chini ya bendera yake na hawakuachana hata lahadha moja.

Watu wa Sham walikuwa wameujua Uislamu kupitia watu kama vile Muawiyya ambaye alikuwa ametawala eneo hilo kwa takribani muda wa miaka 42. Katika kipindi hicho kirefu, watu walikuwa wamelelewa pasina kuwa na busara wale ujuzi wa dinia na hivyo walikuwa wakisalimu amri mbele ya matakwa ya watawala dhalimu pasina kuuliza lolote.

Watu wa Sham walikuwa mbali sana na Uislamu halisi. Kasri ya Muawiya ilikuwa ni kituo cha maasi, anasa, starehe, ubadhirifu wa mali ya umma. Mtawala huyo fasidi alijijengea makasri ya kifakhari huku akiwabaidisha, kuwafunga jela au kuwaua wapinzani wake. Maovu na maasi hayo ya watawala yalikuwa ni jambo la kawaida sana kwa watu wa Sham kiasi cha wao kuwa na dhana potofu kuwa, katika zama za Mtume SAW, utawala ulikuwa kama ambao walikuwa wakiuona. Kwa kuzingatia hali hiyo, lilikuwa jambo rahisi sana kwa watawala wa Bani Umayya kupotosha historia kuhusu harakati ya mwamko wa Imam Hussein AS na namna alivyouawa shahidi kidhalimu kama ambavyo walikuwa wameeneza uongo kuwa Imam Hassan AS alifariki kutokana na pneumonia.

Ni katika hali kama hivyo ndipo mtu mmoj alipouona msafara wa wafungwa wa Karbala ukiwa Damascus, mji mkuu wa Sham alimwambia Imam Sajjad AS, mwana wa Imam Hussein AS aliyenusurika maafa ya Karbala kuwa: "Namshukuru Mweneyzi Mungu kuwa mumeuawa na kuangamizwa na watu wamesalimika na shari yenu!

Imam Sajjad AS kwa kusikia maneneo ya mtu huyo aliyekuwa akiwatusi Ahul Bayt AS alisoma sehemu ya Aya ya 33 ya Sura Ahzab inayosema….."Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara."

Kisha akasema, "Aya hii imeshuka kwa ajili yetu, (Ahul Bayt)" Baada ya hapo huyo bwana alidiriki kuwa kile ambacho alikuwa amekisikia kuhusu mateka hao kilikuwa si sahihi na akajuta na kutubu kuhusu aliyokuwa ameyasema.

Hivyo, kwa hatua ya watu wa familia ya Imam Hussein AS kuenda nyumba hadi nyumba sambamba na hotuba bainifu za Imam Sajjad AS na Bibi Zainab AS pamoja na wengine waliokuwa nao, waliweza kusambaratisha upotoshaji wa miaka kadhaa wa watawala wa Bani Ummaya na hata katika Sham, kitovu cha utawala wao, watu waliweza kufahamu ukweli.

@@@@@

Alikuwa mvulana mwenye maarifa, alikuwa mvulana chipukizi na alikuwa ni shujaa na mtiifu. Hakuwa amebaleghe. Katika usiku wa Ashura, wakati Imam Hussein AS alifahamishwa kuhusu kuuawa masahaba zake, Qasim alisimama mbele yake na kumuuliza: "Ewe Amu yangu! Je, kesho nami nitauawa shahidi au la? Imam alimkumbatia na kumuambia hivi: "Ewe mwanangu! Unakitazama vipi kifo? Qassim akajibu kwa kusema: Ni kitamu zaidi ya asali"

Imam kwa kusikia maneneo hayo alifurahi na kusema: "Wewe utauawa baada ya balaa kubwa na Ali Ashgar pia atauawa shahidi."

Katika siku ya Ashura, Qassim alijitayarisha kwa ajili ya mapambano na akaubeba upanga wake. Kutokana na kuwa alikuwa na umri mdogo na mwili mdogo pia, alikuwa akiuburuza upanga wake ardhini. Imam Hussein AS aliufunga upanga wake kwa njia ambayo haungeburuzwa chini. Qassim alikuwa na hamu sana ya kuenda katika medani ya vita lakini Imam hakuwa anamruhusu. Pamoja na hayo Hadhrat Qassim AS aliendelea kusisitiza na hatimaye Imam akamruhusu. Alipoingia medani, alijiarifisha na kusema: "Enyi maadui wa Mwenyezi Mungu! Iwapo hamnitambui mimi ni mwana wa Hassan bin Ali bin Abi Talib na huyo ambaye mumemzingira ni ami yangu, Hussein AS." Ujasiri na ushujaa wake ulidhihirika katika uso wake mchanga.

Hamid Bin Muslim, mmoja kati ya wanajeshi katika medani hiyo anasema hivi: "Kutoka katika hema la Hussein, aliibuka mvulana aliyekuja katika medani ya vita, uso wake ulikuwa umeangaza kama mwezi. Alikuwa na upanga na shati refu. Umar ibn Sa'ad akasema: "Wallahi nitamshambulia vikali mvulana huyu ." Nikamwambia: "Ajabu, unamtakia nini huyu mvulana? Akinilenga sitamnyoshea mkono. Acha tukabiliane na wale waliokandoni mwake. Umar ibn Sa'ad alijibu kwa kusema: Wallahi! Lazima nimshambulie na nimkamate."

Wakati wa vita, Umar ibn Saad alikata sehemu ya kichwa cha Qassim kwa upanga. Hapo Qassim alianguka chini, na kuanza kupaza sauti kwa kusema: Ewe Ami yangu! Nisaidie. Imam Hussein AS alisikia sauti ya Qassim AS na kupanda farasi kwa kasi akielekea upande alipokuwepo katika medani. Alpofika hapo aliketi na kuweka kichwa cha Qassim katika mapaja yake na katika lahadha hiyo akasema: "Wallahi! Nni hali ngumu kwa ami yako asikie sauti yako na akiitikia au asitikie, isiwe ni kwa faida yako.

Imam Hussein AS alichukua mwili wa Qasim uliokuwa umetoka uhai na kuupeleka kwenye hema na akauweka pembizoni mwa mwili wa Ali Akbar AS ambaye tayari naye alikuwa ameshauawa na kusema: "Enyi binamu zangu na enyi jamaa zangu! Mumestahamili, Wallahi baada ya hapa hamtaonja tena machungu.