Change Language: English

Mafundisho ya Imam Hussein AS (1)

Daima kumekuwepo na swali hili kwamba je, ni nini hasa lengo la mapambano ya Imam Hussein (as)? Je, lengo lake lilikuwa ni kuchukua utawala au lilikuwa ni kuleta mabadiliko na marekebisho kwenye jamii ya Kiislamu? Je, Imam (as) hangeweza kutumia njia nyingine ya amani ili kufikia lengo hilo bila kufanya mapambano ambayo yalisababisha uporaji, kutekwa nyara na umwagaji damu ya Watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saW)?

Mbali na kujaribu kujibu maswali haya katika vipindi kadhaa tulivyokutayarishieni kwa mnasaba wa kuwadia mwezi wa machungu na huzuni kubwa wa Muharram tutachunguza pia kwa kifupi maisha ya mtukufu huyo (as), Karibuni. Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Hussein (as) ni taa ya mwongozo na safina na uongofu.' Bila shaka kufuata maisha na maadili ya Imam huyo humletea mtu binafsi na jamaii nzima saada ya humu duniani na ya huko Akhera. Katika hadithi sahihi ambayo imeandikwa na wanahadithi kutoka madhehebu zote mbili za Shia na Suni, inasema kwamba siku moja Imam Hussein (as) katika siku zake za utotoni alimjia babu yake yaani Mtume Mtukufu (saw). Mtume alipomwona alimwambia: 'Karibu ewe Hussein! Pambo la mbingu na ardhi' Ubeyy bin Ka'b ambaye alikuwa mmoja wa masahaba wa Mtume Mtukufu (saw) na waandishi wa Wahyi ambaye alikuwa ameketi pembeni ya Mtume alimuuliza: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, sipokuwa wewe kwani kuna mtu mwingine ambaye ni pambo la mbingu na ardhi?' Mtume akasema: 'Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye alitutuma kwa haki kuwa Mtume, sehemu ya Hussein mbinguni ni bora zaidi kuliko ya ardhini! Na huko ndiko ambako kumeandikwa: 'Hussein ni taa ya mwongozo, safina ya uongofu na kiongozi asiyeteleza.'

Hussein ni taa ya mwongozo, safina ya uongofu na kiongozi asiyeteleza.

Jambo la kwanza na ambalo ni muhimu zaidi kuhusiana na Imam Hussein (as) ni kuwa yeye alikuwa mfano wa wazi zaidi wa maana halisi ya neno 'mtumwa' au 'mtumishi" wa Mwenyezi Mungu. Kabla ya kitu chochocte kingine alikuwa 'Abdullah' yaani mja wa Mwwenyezi Mungu, na ibada halisi ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ikionekana katika kila pande za maisha yake. Hakuwa akifikiria jambo jingine lolote isipokuwa kumridhisha Mwenyezi Mungu na utulivu na upazaji sauti wake wote ulifanyika kwa msingi huo. Katika kipindi cha utawala wa dhalimu Muawiyya bin Abi Sufyan, alifanya subira kubwa kwa lengo la kulinda dini ya Muumba wake na alipoona ridhaa ya Mwenyezi Mungu ikiwa katika kusimamisha mapambano dhidi ya dhulma ya Yazid bin Muawiyya alifanya hivyo mara moja bila kusita na kuamua kutoa muhanga wapendwa wake wote katika njia hiyo huku akisema: ' Ewe Mwenyezi Mugu! Amepata nini yule aliyekupoteza wewe, na amepoteza nini aliyekupata wewe?

Kunia yake ya Aba Abdillah' inatokana na wingi wake wa kufanya ibada kwa ikhlasi na mapenzi makubwa kwa Muumba wake, ibada ambayo aliikamilisha kwa kutoa damu yake na wapendwa wake bila kusita. Katika kitabu cha 'Sifa mahususi za Imam Hussein (as)' pameandikwa kama ifuatavyo: 'Hussein ni nembo ya ibada! Mitume wote wa Mwenyezi Mungu na viongozi maasumu walikuwa wakimuabudu Mwenyezi Mungu wao kwa ikhalsi na mapenzi makubwa; ama Imam Hussein alikuwa akimuabudu kwa njia maalumu. Tokea nuru ya uwepo wake ilipodhihiri kwenye tumbo la mama yake Bibi Fatimah (as) hadi wakati wa kutundikwa kichwa kilichong'ara kwenye mikuki (ya waliomuua) daima na kila sehemu alikuwa akisifu, kutukuza, kushukuru na kumsabihi Mweyezi Mungu na kusoma Qur'ani Tukufu.'

Imam Hussein (as) alifanya Hija mara 25 na kuswali rakaa 1000 kila mchana na usiku. Hamu ya Imam Hussein (as) kwa ibada ilikuwa kubwa kiasi kwamba katika mkesha wa siku ya Ashura ambapo jeshi la maadui lilikuwa limejitayarisha kuhujumu na kushambulia mahema ya Aba Abdillahi al-Hussein (as), Imam Hussein (as), aliwaomba muda maadui ili wampe fursa ya kufanya ibada ambapo alifanya ibada hiyo usiku kucha hadi asubuhi. Katika tukio la Karbalaa pia, ambapo misiba na matatizo yalimzidia Imam (as), katika medani ya vita na kuhuzunishwa na jinsi maadui walivyokuwa wakiwafanyia ukatili na unyama wa kupindukia familia yake, ndivyo kadiri subira ya Imam na imani yake kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu ilivyokuwa ikiongezeka na akisema: 'Ewe Mwenyezi Mugu! Mimi Ninakiridhia kile unachokiridhia Wewe.'

Yaa Aba Abdillah!

Upotovu na maovu ambayo yalianza baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) yalikuwa yakiongezeka kadiri wakati ulivyokuwa ukizidi kusonga mbele. Watawala wa Bani Ummayyia ambao walianza kutawala Sham katika kipindi cha ukhalifa wa Othman mwaka 41 Hijiria walitwaa rasmi ukhalifa wa Umma na jamii ya Kiislamu. Baada ya kuingia madarakani Ummayyia bin Sufyan ambaye alikuwa adui mkubwa wa Mtume katika kabila la Qureish, thamani za Kiislamu zilibadilika pakubwa kwa kadiri kwamba hakuna chochote kilichosalia kwenye thamani hizo isipokuwa jina tu. Jina hilo pia lilidhoofika na kukosa maana baada ya kuaga dunia Muawiyya na kuingia madarakani mtoto wake yaani Yazid. Kwa kadiri kwamba Yazid alipinga kila kitu katika Uislamu na kutangaza wazi kwamba, 'hakuna habari yoyote iliyotoka mbinguni wala Wahyi ulioteremka.'

Ili kuimarisha utawala wake, Yazid bin Muawiyya alipanga njama ya kuchukua baia au kiapo cha utiifu kutoka kwa Imam Hussein (as) kwa gharama yoyote ile. Baia ina maana ya chombo kinachotangaza utayarifu wa mtu kutekeleza amri na maagizo ya khalifa halisi, wa kweli na anayefaa wa Mtume Mtukufu (saw) na kuwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya kutekeleza amri zake. Sasa baia ya aina hiyo hata kama ingekuwa ni ya kidhahiri tu na kwa ajili ya kuepusha hatari basi ingekuwa na maana ya kutia saini rasmi kuidhinishwa kwa utawala wa ufuska, upotovu, maovu na dhulma ya Yazid. Baia hiyo ilikuwa na maana ya kuahidi kushirikiana na Yazid kwa ajili ya kufanya mauaji dhidi ya watu wasio na hatia na kukanyaga heshima na utukufu wa watu na Uislamu, jambo ambalo halingekubaliwa hata kidogo na Imam Hussein (as). Kwa msingi huo wakati ambapo Yazid alitaka kuketi kwenye kiti cha utawala na kuchukua sehemu ya Mtume Mtukufu (saw) na kujifanya kuwa kiongozi wa kidini na kisiasa wa Waislamu pamoja na kiongozi wa ulimwengu wa Kiislamu, Imam (as) alikataa na kukwepa kumpa baia, yaani mkono wa utiifu. Kwa hakika hakuwa na chaguo jingine isipokuwa kupambana na kutangaza kutokuwa wa kisheria utawala wa Yazid.

Imam Hussein (as) ambaye ni mmoja wa Watu wa Nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), mawalii na warithi wa babu yao huyu mtukufu, katika kukabiliana na Farazdaq, ambaye alikuwa mmoja wa washairi maarufu wa Kiarabu katika enzi hizo alimwambia: 'Hawa (Mayazid) wameacha kumwabudu Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, kudhihirisha ufisadi, kubatilisha adhabu ya kisheria (wanayopewa wahalifu), wanakunywa pombe na kujichukulia mali ya masikini. Na mimi ndiye mbora zaidi wa watu wanaopasa kusimama kwa ajili ya kuokoa dini, utukufu, sheria na Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.' Imam Hussein alisimamisha mapambano dhidi ya Yazid kwa lengo hilo. Pamoja na hayo lakini Imam (as) aliendesha mapambano hayo dhidi ya Yazidi kwa njia ya kimantiki na busara kubwa ili kukamilisha hoja mbele ya watu wote. Ili kuyafanya mapambano hayo yawe na athari kubwa zaidi, Imam (as) aliyachanganya mapambano hayo na kuyadhihirisha na uovu wa dhulma, ili madhalimu waendelee kuchukiwa katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu, na kutopata fursa ya kufutwa au kupendelewa na upande wowote ule unaopigania haki. Hii ndio maana mapambano yake yamedumu hadi leo kutokana na kuuawa kwake shahidi pamoja na kuchukuliwa mateka familia yake.

Mapambano ya Imam (as) yanakumbusha moyo mkubwa na adhimu wa wanadamu waliojijenga na kujitakasa kimaanawi, kiroho na wema ambao walijitolea kwa ajili ya kufanikisha mafundisho matukufu ya Mwenyezi Mungu. Hawa ni watu wema na watukufu ambao hufuatilia malengo adhimu na ya kimaanawi na yasiyofungamana na dunia maishani mwao. Hawa ni wanadamu ambao ni mifano bora ya kuigwa katika masuala ya imani, akhlaki, ujasiri, utu na mapambano ambao daima huiremba historia na kuifanya kuwa ya kumvutia kila mtu.

Muslim bin Aqil ni mmoja wa watu hao wema. Kusikia jina la mpiganaji huyo shupavu wa kujitolea katika njia ya haki, kunakumbusha upevu, utu na ushupavu. Hamasa iliyofanywa na Muslim bin Aqil mjini Kufa huko Iraq kwa hakika ulikuwa ni utangulizi wa mapambano makubwa ya Ashura na Muslim mwenyewe alikuwa mtangulizi wa harakati hiyo ya Bwana wa Mashahidi Imam Hussein (as), mjumbe wa mapinduzi ya Karbalaa, shahidi wa kwanza wa hamasa ya kihistoria na ya kudumu milele ya Ashura.

Mwaka 60 Hijiria watu wa Kufa walimwandikia Imam wao maelfu ya barua wakimtaka aelekee huko ili awasaidie katika kupambana na dhulma ya Yazid. Baada ya kusoma na kutathmini kwa kina barua na hali ya Kufa pamoja na udharura wa kufugamana na watu hao, alimtuma huko Muslim bin Aqil kama mwakilishi wake. Alikuwa na mwamko wa kutosha wa kisiasa, busara na pia takwa na uzingatiaji mkubwa wa masuala ya kidini. Alisema: 'Iwapo watu watanipa beia mimi pia nitakwenda huko.' Muslim bin Aqil alianza safari yake ya kuelekea Kufa kutokea Makka. Alielekea kwenye mji liojaa vituko na matukio na ambao ulikuwa na wakazi waliokuwa na fikra na mitazamo tofauti. Hata kama kidhahiri ulionekana kuwa ni mji uliokuwa na utulivu lakini huo ulikuwa ni utulivu wa kabla ya tufani tu. Muslim alifikia nyumbani kwa Mukhtar ambapo makundi ya watu walikuwa wakifika hapo kumsalimu, kuonana naye na kumbai. Hata hivyo uchangamfu na makaribisho hayo hayakudumu kwa muda mrefu. Yazid ambaye alikuwa na azma ya kulinda utawala wake kwa njia yoyote ile alimteua mtu muovu, Ubeidullah bin Ziyad kuwa liwali wake mjini Kufa licha ya kuhifadhi nafasi yake ya uliwali wa mji wa Basra ili apate kumkamata na kumuua Muslim bin Aqil. Ibn Ziyad alieneza woga na hofu kubwa mjini humo kadiri kwamba kila mtu alijaribu kukwepa na kujitenga na Muslim. Muslim alilazimika kukimbilia kwenye nyumba ya Hani bin Urwa, mzee wa Kufa na mmoja wa viongozi wenye ushawishi wa Kishia kwenye mji huo. Hani pia alipata fahari ya kuonana na Mtume Mtukufu (saw) na alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw).

Tishio kubwa zaidi la Ib Ziyad lilielekezwa kwa watu waliompa hifadhi Muslim bin Aqil na kuahidi kumpa zawadi kila mtu ambaye angetoa habari alikokuwa mjumbe huyo wa Imam Hussein (as). Mjini Kufa Muslim bin Aqil alikuwa amefungiwa milango yote na kila mtu alikuwa akifikiria usalama na utulivu wake mwenyewe tu. Baada ya kuwa mkimbizi kwa siku kadhaa, hatimaye Muslim bin Aqil alipewa hifadhi na mwanamke mmoja aliyekuwa akiitwa Taua, lakini mtoto wake alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Ibn Ziyad. aliporejea nyumbani usiku aligundua kutokana na harakati za mama yake kwamba walikuwa na mgeni nyumbani kwao ambaye hakuwa mtu mwingine isipokuwa Muslim bin Aqil. Kwa kufichua habari hiyo, askari wa Ibn Ziyad waliivamia nyumba ya Taua wakati wausiku kwa ajili ya kumkamata Muslim ambapo alipigana nao wote kwa ushujaa na ujasiri mkubwa. Pamoja na hayo hatimaye alizingirwa na kushambuliwa kwa mkuki kutokea nyuma ya kichwa chake ambapo alianguka chini na kisha kukamatwa na askari hao. Mtu huru ambaye alikusudia kuwaokoa wafungwa hao wa matamanio ya dunia yeye mwenyewe akatumbukia kwenye mtego wao na kuwa mfugwa wao. Alipokuwa akiuawa shahidi kwenye kituo cha watawala wa Bani Ummaiyya, Mulim bin Aqil hakuonyesha woga wowote bali alifurahishwa sana na ukweli kwamba alikuwa akiuawa shahidi kwenye njia ya haki na harakati ya Imam Hussein (as).

Aliposikia habari ya kuuawa shahidi wafauasi wake waaminifu Imam (as) alibubujikwa na machozi na kusema "Ewe Mwenyezi Mungu! Tupe sisi na wafuasi na wetu nafasi ya juu na utujumuishe kwenye rehema zako ambapo Wewe ndiwe Muweza wa kila kitu.

Salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika na wema wote ziwe juu ya moyo mkubwa wa Muslim bin Aqil, na salamu pia ziwe juu ya wale wanaoedeleza njia yao, ambayo ni njia ya haki na uhuru.

Salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika na wema wote ziwe juu ya moyo mkubwa wa Muslim bin Aqil.