Change Language: English

Imam Husein na Tabia Yake Njema:

Imam Husain (as) katika maisha yake na nyendo zake alikuwa anafuata maadili ya Uislamu na tabia njema za Mtume (saww), na wanahistoria wengi wametaja misimamo yake na sehemu ambazo zinaakisi picha, sifa na tabia yake njema, hapa tunataja baadhi yake tu:

    1.Miongoni mwa unyenyekevu wake na ukarimu wake ni kwamba aliingia kwa maskini wakiwa wanakula wakamkaribisha kwenye chakula akaretemka kwenye kipando chake na akala pamoja nao, kisha akawaambia, nimeshawaitikia basi na nyie niitikieni, wakaitika wito wake na wakaondoka pamoja naye hadi nyumbani kwake, akamwambia mke wake Rabab toa ulichokiweka, akatoa aliyokuwa nayo miongoni mwa mali basi akawapa.[1]

    2.Na miongoni mwa ukarimu wake ni kwamba alimtembelea Usama bin Zaid katika maradhi yaliyopelekea kifo chake, alipofika kwake Usama alisema: “Aaah huzuni yangu.” Husain akamuuliza: “Ni nini huzuni yako?” Akasema: “Deni langu ambalo ni elfu sitini (60,000/=)” Husain akasema: “Basi hilo ni juu yangu mimi.” Usama akasema: “Naogopa kufariki kabla halijalipwa.” Basi Husain (as) akampa matumaini kwa kusema: “Hutokufa hadi nililipe badala yako.” Imam akajitolea na akalilipa badala yake kabla ya kufariki.[2]

    3.Na alikuwa ni kigezo katika uchamungu na ni mwenye kudumu katika daraja za ibada, siku moja mmoja wa wafuasi wake alimwambia: “Ni ukubwa ulioje wa hofu yako kwa Mola Wako?” Akasema (as): “Hatosalimika Siku ya Kiyama isipokuwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu duniani.”[3]Na wakati wake mwingi alikuwa anautumia kwa Swala na Saumu. Na alisema juu yake Ibnu Zubair: "Ama Wallahi wamemuuwa mtu ambaye ni mwingi wa Swala usiku, na mwingi wa Saumu mchana.”[4]

Na alihiji Hija ishirini na tano kwa kutembea kwa miguu na sadaka zake zilikuwa zinatangulizwa mbele yake.[5] Na alikuwa ni mwingi wa wema na sadaka, na alirithi ardhi na vitu, akavitoa sadaka kabla ya kuvipokea, na alikuwa anabeba chakula katika giza la usiku kuwapelekea maskini wa Madina.[6]

Maneno Yake ya Kimapinduzi:

Katika mwanzo wa mapambano yake matukufu hadi kupata kwake shahada tukufu, katika matukio mbalimbali, aliuelekeza umma kwa maneno na hotuba zinazozingatiwa kuwa ni hazina kubwa na chemchem inayowapa wanamapinduzi na waungwana misimamo yake, na inayoshibisha matakwa yao katika mapambano na mapigano. Na maneno hayo, hotuba na barua vinabainisha sababu zilizomwajibisha Imam Husain (as) kufanya mapinduzi yake, na malengo ambayo aliyakusudia katika harakati zake.

Miongoni mwa maneno yake ni yale yaliyokuja katika wasia wake kwa ndugu yake Muhammad bin al-Hanafiya wakati wa kutoka Madina:

إني لم أخرج أشراً ولا بطراً، ولا مفسداً، ولا ظالماً وإنما خرجت لطلب الإصلاح في أمة جدي، أريد أن آمر بالمعروف وأنهى عن المنكر، وأسير بسيرة جدي وأبي علي بن أبي طالب، فمن قبلني بقبول الحق، فالله أولى بالحق ومن رد علي أصبر حتى يقضي الله بيني وبين القوم وهو خير الحاكمين

"Hakika mimi sijatoka kwa shari wala kwa kiburi wala kwa kutaka ufisadi wala si kwa udhalimu, hakika nimetoka kwa ajili ya kufanya marekebisho katika umma wa babu yangu,nataka kuamrisha mema na kukataza maovu, na kwenda kwa mwenendo wa babu yangu na baba yangu Ali bin Abi Twalib, hivyo atakayenikubali kwa kuikubali haki basi Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kwa haki, na atakayenikataa basi nitasubiri hadi Mwenyezi Mungu ahukumu baina yangu na baina ya kaumu Naye ni mbora zaidi wa kuhukumu."[7]

Na alisema katika hotuba yake mbele ya jeshi la Bani Ummaya chini ya uongozi wa Hurr bin Yazid ar-Rayaahiy:

أيها الناس إن رسول اللهقال: «من رأى سلطاناً جائراً، مستحلاً لحرم الله، ناكثاً لعهد الله، مخالفا لسنة رسول الله، يعمل في عباد الله بالإثم والعدوان، فلم يغير ما عليه بفعل ولا قول كان حقاً على الله أن يدخله مدخله ألا إن هؤلاء قد لزموا طاعة الشيطان، وتركوا طاعة الرحمن، وأظهروا الفساد، وعطلوا الحدود، واستأثروا بالفيء، وأحلوا حرام الله، وحرموا حلاله، وأنا أحق من غير

"Enyi watu hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) amesema: ‘Yeyote atakayeiona serikali ovu inayohalalisha haramu ya Mwenyezi Mungu, yenye kutengua ahadi ya Mwenyezi Mungu, yenye kukhalifu sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, yenye kuwafanyia waja wa Mwenyezi Mungu madhambi na uadui, na wala asibadilishe yaliyopo kwa vitendo wala kwa kauli, basi ni haki ya Mwenyezi Mungukumwingiza motoni. Eee hakika hawa wameshikamana na kitendo cha kumtii shetani na wameachana na kitendo cha kumtii Mwenyezi Mungu, na wanadhihirisha ufisadi na wanavuka mipaka na wanakula mali, wanahalalilsha haramu ya Mwenyezi Mungu na wanaharamisha halali ya Mwenyezi Mungu, na mimi nina haki zaidi ya kufanya mageuzi kuliko mtu mwingine yeyote."[8]

Na alisema kuwahutubia wafuasi wake wakati wa kushuka Karbalaa:

ألا ترون إلى الحق لايعمل به، وإلى الباطل لا يتناهى عنه، ليرغب المؤمن في

لقاء الله، فاني لا أرى الموت إلا سعادة والحياة مع الظالمين إلا برما

"Hivi hamuoni kuwa haki haifanyiwi kazi na batili haikatazwi, basi muumini na apende kukutana na Mwenyezi Mungu, hakika mimi sioni mauti isipokuwa ni utukufu na kuishi pamoja na madhalimu isipokuwa ni fedheha.”[9]

Na miongoni mwa hotuba zake kwa jeshi la Bani Ummaya kabla ya kuanza vita ni:

ألا وإن الدعي ابن الدعي قد ركز بين اثنتين بين السلة والذلة وهيهات منا الذلة يأبى الله لنا ذلك ورسوله والمؤمنون، وحجور طابت وطهرت وأنوف حمية، ونفوس أبيه، من أن يؤثر طاعة اللئام على مصارع الكرام، ألا وإني زاحف بهذه الأسرة على قلة العدد، وخذلان الناصر....

"Eee, hakika mtoto wa haramu atokanaye na mtoto wa haramu ametia mkazo wa kunitaka nichague moja kati ya mambo mawili, baina ya vita na udhalili, na ni mwiko kwetu kuchagua udhalili, Mwenyezi Mungu, Mtume wake na waumini wanakataa sisi kuchagua udhalili, na vilevile vizazi vitwaharifu, na pua zenye heshima, na nafsi takatifu, vyote vinakataa kuchagua kuwatii waovu badala ya kifo chenye utukufu. Eeee hakika mimi ni mwenye kuondoka pamoja na familia hii licha ya uchache wa idadi na usaliti wa msaidizi."[10]


[1] Al- Qarashiy katika Hayaatu Imamil- Husain juzuu 1 uk: 125akinukuu kutoka katika Tarikh IBnu Asaakir juzuu 13 uk: 54

[2] Rejea iliyotangulia uk: 128

[3] Rejea iliyotangulia uk: 133

[4] Twabariy katika Tarikh al-Umamu wal-Muluk Jz. 6, uk: 273 chapa yakwanzachapisho la al-Hasiniya Misri

[5] Al- Qarashiy katika Hayaatul-Imamil-Husain Jz. 1, uk: 134

[6] Rejea iliyotangulia uk: 135

[7] Al- Qarashiy katika Hayaatul- Imamil Husain juzuu 2 uk: 264

[8] Rejea iliyotangulia uk: 80

[9]""98

[10]""193