Change Language: English

Imam Husein Alishikamana na Amani Katika Mapambano Yake:

Kwa nini Imam Husein (as) alifanya harakati? Je, katika mapambano yake alikhalifu mfumo wa amani?

Hakika Imam Husein (as) amefanya harakati kwa ajili ya kuhifadhi umma na kulinda maslahi yake, na aliona kwamba utawala wa Ban Ummayya hautoi amani kwa watu bali unafanya mabaya dhidi yao, na tayari Amirul-Muumina Ali bin Abi Twalib alikuwa ameshasema kuwahusu Bani Ummayya: "Wallahi wataendelea hivi mpaka wafikie kiasi cha kuwa hawatoacha alichokiharamisha Mwenyezi Mungu ila watakihalalisha, wala ahadi ila wataitengua, na hata haitobakia nyumba ya matofali wala ya manyoya ila dhulma yao itaingia, na ubaya wa matendo yao utawafanya duni, mpaka watakuja kusimama waliaji wawili:Mliaji analia kwa ajili ya dini yake na mliaji analia kwa ajili ya dunia yake."

Baina ya Ukhalifa na Ufalme:

Umma huu ambao ulikuwa unaishi katika kivuli cha ukhalifa ambao ulimalizika kwa kufa shahidi Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (as), ghafla ulishuhudia Yazid akijitangaza kuwa ni Amirul-Muuminina! Imam Husein (as) alishikamana na mkataba wa suluhu ambayo aliifanya Imam Hasan (as) pamoja na Muawaiya, licha ya kwamba upande wa pili ulivunja mkataba na kufanya ubadhirifu na uharibifu katika Baitul-Mali ya Waislamu, kwani Muawiya alitangaza hayo alipowahutubia Waislamu kwa kusema: "Sikuwapiga vita ili mfunge, mswali, mtoe zaka na mhiji, najua mnafanya yote hayo, bali nimewapiga vita ili niwatawale na Mwenyezi Mungu amenitawalisha juu yenu hali yakuwa nyinyi ni wenye kuchukia.”

Na hapa naashiria kwenye kitabu kizuri cha mwanafikra wa Kiislamu na mlinganiaji maarufu naye ni Sheikh Abu al-A’laa Maudud, naye ni kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika zama hii, aliyepata tuzo ya mfalme Faiswal kwa ajili ya kuutumikia Uislamu mwaka 1997. Mwanachuoni huyu ana kitabu muhimu sana jina lake ni Ukhalifa na Ufalme? humo anazungumzia juu ya ukhalifa ambao ulimalizika kwa kuuliwa Imam Ali (as) na anaulinganisha na ufalme muovu ulioanzishwa na Ban Ummayya. Abu al-A'laa anaashiria katika kitabu chake kwamba dola ya Ban Ummayya hakika iliasisiwa kwa sababu ya mazingira ambayo yaliandaliwa na uzembe ambao ulizunguka ukhalifa wa Uthman.

Kuna baadhi walioudhika kutokana na kitabu hiki kwa sababu ya kumkosoa kwake sahaba, al-Maudud amesema kwa jibu la ufafanuzi ambalo ameliambatanisha katika chapa ya pili, nayo tayari imeshasambazwa, ameashiria humo kwamba kumheshimu sahaba hakuzuii kupata zingatio katika maisha yao, wala haimaanishi tunyamazie makosa, kunyamaza kwetu kutakuwa ni sharia itakayofuatwa na watu.

Na vilevile kuna kitabu cha Muhammad Qutub naye ni mwanachuoni maarufu wa Misrialiyeishi Saudia na ameshiriki katika kuandaa mitaala ya kidini anwani yake ni: Vipi

tutaandika historia ya Kiislamu, humo anasema: "Katika ambalo hakuna shaka ndani yake ni kwamba historia ya kisiasa kwa Waislamu ni mbaya sana, kutokana na yale yaliyomo katika historia yao yote.Hakuna shaka kwamba umetokea upotovu mwingi katika nyanja za kisiasa katika mfumo wa Kiislamu wa asili, na upotovu huu umetokea mapema katika historia ya Kiislamu, na haikuwa inapasa kutokea."

Na cha kushangaza katika jambo la Yazidi ni kwamba yeye alikuwa anafanya uovu wake chini ya anwani ya Uislamu, Ibnu Kathir anasema katika al-Bidayah Wanihayah kuhusu Yazid bin Muawiya: "Ana mambo mazuri miongoni mwa ukarimu, upole, ufasaha, ushairi, ushujaa na rai nzuri katika ufalme, na pia alikuwa anaelemea kwenye matamanio na kuacha baadhi ya swala katika baadhi ya nyakati, na wakati mwingi akiziacha kabisa."

Na vilevile anapokea Ibnu Kathir: “Kwamba Yazid alikuwa ni mashuhuri kwa kucheza ngoma, kunywa pombe, kuimba, kuwinda na kucheza kwake na vijana, watumwa na mbwa, na kupiganisha madume ya kondoo, dubu na nyani, na wala hakuna siku isipokuwa alikuwa ni mlevi, na alikuwa anamfunga nyani kwenye farasi kwa kamba na kumkokota, na anamvalisha nyani kofia za dhahabu na vile vile vijana, na alikuwa anashindanisha baina ya farasi, na ilikuwa anapokufa nyani anamhuzunikia."

Huyu ndio Amirul-Muuminina!.

Na makubwa zaidi kuliko yaliyotangulia, ni Muawaiya alipotaka kumfanya Yazid kuwa makamu wake alimhutubia kwa kusema: "Ewe mwanangu kuna uwezekano mkubwa ulioje wa kufikia haja yako bila ya kufanya uovu unaoondoa utu wako na uwezo wako.” Kisha akasoma mashairi:

"Shughulika mchana kwa kutafuta matukufu, na subiri kumhama kipenzi wa karibu, hadi usiku utakapoleta kiza, na likafumba jicho la mwenye kuangalia, basi fanya usiku unayoyataka, hakika usiku ni mchana wa waovu. Ni mafasiki wangapi unawahesabu kuwa ni wachamungu, ameshafanya mmoja wao maajabu usiku. Usiku umemfunika kwa pazia lake, akawa katika amani na maisha mazuri, na ladha ya mpumbavu iko wazi, anakwenda mbio kwayo kila adui muovu."

Na hata Muawiya alipomtaka ushauri Ziyad bin Abiihi katika jambo la Yazid, yeye alimshauri ampe muda huwenda mwendo wa Yazid utabadilika na ikawa kuna uwezekano wa kuuzika (kwa watu). Riwaya ya kihistoria anayoipokea al- Ya’qubiy katika Taarikh yake inasema: “Hakika Ibn Ziyad alimwambia Muawiya: ‘Watu watasemaje tutakapowaita katika kutoa kiapo cha utii kwa Yazid ilihali yeye anacheza na mbwa na nyani, anavaa dhahabu na ametopea katika kunywa pombe, na anacheza ngoma. Na mbele yake yupo Husein bin Ali, Abdillahi bin Abbas, Abdillahi bin Zuberi, Abdillahi bin Umar. Mwamrishe afuate tabia ya hawa mwaka au miaka miwili, huwenda tutamsitiri kwa watu.”

Huyu ndiye Yazid mwenye kucheza na nyani, mnywa pombe mwenye kutangaza ufuska hadharani, muuwaji wa nafsi isiyo na hatia na mwishowe anakuwa Amirul-Muuminina. Alisema kweli mshairi wa Ahlulbayt Sayid Ja'far al-Hilliy alipoelezea hali yake kwa kauli yake:

"Sijajua mashujaa wa Kiislamu walikwenda wapi, na namna gani Yazid amekuwa mfalme baina yao, mnywa pombe mwenye kulaumiwa kwa aina yake, na kutokana na tabia mbaya inayomuwia vigumu muovu."

Kwa sababu hiyo Imam Husein alitangaza msimamo wake tangu siku ya kwanza katika nyumba ya Walid Gavana wa Madina alipomtaka kutoa kiapo cha utii, pale aliposema: “Ewe kiongozi hakika sisi ni Ahlulbayt wa Mtume na chimbuko la ujumbe na mahala pa kuteremkia malaika, kwetu Mwenyezi Mungu amefungua na kwetu amehitimisha, na Yazid ni mtu fasiki, mnywa pombe, muuwaji wa nafsi isiyo na hatia, mwenye kutangaza ufasiki bayana, na mtu mfano wangu hawezi kumpa kiapo cha utii mtu aliye mfano wake."