Change Language: English

Husein na Mapambano ya Amani:

Imam Husein (as) alipojua jambo hilo alifanya harakati za kuelimishaumma ili ubebe jukumu lake, alitangaza harakati zake za amani za mabadiliko bila ya kutumia silaha na akasema neno lake mashuhuri ambalo linabainisha sababu ya kutoka kwake: “Hakika mimi sikutoka kwa shari wala kwa kiburi wala kwa kufanya uharibifu, wala kwa dhulma bali nimetoka kwa ajili ya kutaka kuleta marekebisho katika umma wa babu yangu, nataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kwenda kwa mwendo wa babu nyangu na baba yangu."

Na kweli Imam alishikilia msimamo wake, lakini Yazid hakusikiliza hilo, akaamuru kikosi kiende Makka na kumuuwa Imam Husein (as) hata kama atakuwa ameng'ang’ania Kaaba. Na katika sehemu nyingi Imam Husein (as) alitangaza kwamba harakati yake ni ya amani na sio ya vita, na miongoni mwa sehemu hizo ni msimamo wake pamoja na Hurru Riyahiy ambaye alikuja na maelfu ya wapiganaji waliobanwa na kiu, walisimama mbele ya Imam (as) wakati wa adhuhuri katika jua na Imam (as) akawaona na walikuwa wamekaribia kuhiliki kutokana na ukali wa kiu, na ilikuwa ni fursa nzuri kwa Imam (as) kuwapiga vita na kuteka mali zao, lakini aliwahurumia kutokana na hali yao na akawafumbia macho, ilihali anajua kwamba wao wamekuja kwa ajili ya kumpiga vita na kumwaga damu yake, na japo baadhi ya wafuasi wake walimshauri juu ya hilo

lakini mfumo wa Imam haukuwa hivyo na wala hauko hivyo,hiyo ni kwa sababu nembo yake ni: "Hakika mimi nachukia kuwaanza wao kwa vita." Kisha akaamuru wafuasi wake kuwanywesha maji wao na farasi wao.

Hapa Imam Husein (as) anatia mkazo kwa umma kwamba haipasi kutumia ubabe na silahakatika kubadilisha siasa; kwa sababu hiyo sio katika masilahi ya jamii, na Maulamaa na Mafaqihi wetu wameshazungumza kuhusu upande huu na miongoni mwao ni Marjaa MarehemuSayyid Muhammad Shiraziy ambaye ameandika katika nyanja hii vitabu vingi kuhsu “Hakuna kutumia nguvu katika Uislam” na kuhusu “Usalama na Amani”, na humo ametilia mkazo kwamba hakuna nafasi ya kulazimisha rai na kuwatawala watukwa silaha na nguvu, na kwamba vitendo hivi sio katika Uislamu. Na kwa masikitiko makubwa katika zama zetu hizi Uislamu na Waislamu wamepakwa matope kwa sababu ya vitendo vya kigaidi ambavyo haviutakii Uislamu na Waislamu kheri, na kwa sababu yake umma umekosa amani yake na utulivu wake na haikubaki nchi yoyote kati ya nchi za Waislamu isipokuwa imedhurika kwa vitendo hivyo.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu aunusuru umma na shari ya fitina hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

IMAM HUSEIN NA MFUMO WAKE KATIKA KULINGANIA NA KUJADILIANA

"Waite kwenye njia ya Mola Wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola Wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka." (Surat Nahli: 125).

Njia ya kuathiri wengine:

Ni jambo la kawaida mwanadamu kuikuta nafsi yake katika maisha haya mbele ya anayehitalifiana naye katika rai, na ambaye maslahi yake yanapingana na maslahi yake. Watu wanatofautiana katika rai zao na mielekeo yao, na kila mmoja kati ya watu anataka kumiliki kiasi kikubwa zaidi kadiri iwezekanavyo katika chumo katika dunia hii, jambo linalosababisha aina ya mgongano katika maslahi baina ya watu. Na mwanadamu anapokuwa mbele ya anayemkhalifu katika rai hakika anaweza kwenda mbio ili kumkinaisha kwa rai yake, ama kutokana na hali ya kidini, kwa kuzingatia kwamba dini inamsukuma muumini kumhubiria mwenzake mafunzo ya dini yake, na nususi zilizopokelewa zinatilia mkazo hilo, kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) amesema: "Mwenyezi Mungu kumuongoa mtu kupitia mikono yako ni bora zaidi kwako kuliko vilivyochomozewa na jua au vilivyochoewa na jua."[4]

Na katika baadhi ya nyakati inajitokeza hali ya ubinafsi kwa mwanadamu wakati wa kwenda mbio kueneza rai zake, kwa kuzingatia kwamba ni aina ya ushindi wa dhati na kwa hivyo anajikuta ni mwenye kujawa na sururi na furaha. Na swali muhimu hapa ni: Ni ipi njia ya kuathiri wengine? Na ni vipi nitahifadhi maslahi yangu wakati yanapogongana na maslahi ya wengine?

Kuna njia mbili:

Kwanza: Kutumia Nguvu na Kulazimisha:

Hapa mwanadamu hurejea kwenye nguvu ili kulazimisha rai yake, hakika kulazimisha fikra na raisio sahihi na haiwezekani, kama ambavyo wewe una akili basi na mwingine pia ana akili, anaweza kutofautiana na wewe katika fikra, na Mwenyezi MunguMtukufu ameumba watu wakiwa huru, hivyo haisihi kwa yeyoye kulazimisha rai yake kwa wenginehata kama atakuwa anaitakidi kwamba rai yake ni ya haki na ni sahihi, ambapo kila mtu anaitakidi kwamba rai yake ni ya haki na ni sahihi, na itikadi hii haitoi kisingizio cha kulazimisharai kwa wengine, Mwenyezi Mungu Mtukfu ambaye ndiye Mlezi wa viumbe halazimishi watu kumwamini kwa nguvu na mabavu, anasema (swt):

"Lau angelitaka Mola Wako, wangeliamini wote waliomo ardhini. Basi je wewe utawalazimisha watu wawe Waumini?" (Surat Yunus: 99).

Na vile vile Manabii na Mitume ambao wanabeba ujumbe wa haki kwa watu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hawakuruhusiwa kulazimisha daawa yao kwa wenginekwa nguvu, bali kazi yao inaishia katika kufikisha:

"Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Kama mkikengeuka basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa. Na mkimtii yeye mtaongoka na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi." (Surat Nuru: 54).

Na pia anasema:

"Basi kumbusha hakika wewe ni mkumbashaji tu. Wewe si mwenye kuwatawalia." (Surat Ghashiya: 22).

Ikiwa Mitume na Manabii hawana haki ya kulazimisha rai ya haki na ujumbe wa haki kwa watu je, inasihi kwa yeyote kufanya kazi hii?

Lakini baadhi ya wenye kiburi wanakwenda mbio ili kulazimisha rai kwa nguvu, na katika historia yetu ya Kiislamu tunakuta namna gani baadhi ya watawala walikuwa wanakwenda mbio juu ya hilo. Na kwa hakika hiyo sio ikhilasi kutoka kwao, kwa rai hizo, lakinini kitendo cha ubabe na kuwakandamiza watu,na hawatosheki kutawala miili ya watu tu baliwanataka pia kutawala fikira zao na kudhibiti rai zao. Na hapa tunataja mfano mmoja:

al-Mahdiy al-Abbasiy ambaye alitawala umma wa Kiislam miaka 11 (kuanzia 169 -185 Hijiria) alitengeneza katika utawala wake nemboya kukabiliana na wazandiki, nao ni wale ambao wana rai yenye kupinga Uislamu, lakini ni namna gani alikabiliana nao? Mapambano hayakuwa kwa mantiki, majadiliano na hoja, lakini ni kwa mapanga. Tuhuma yoyote ikimfikiadhidi ya yeyote kwamba ni zandiki alikuwa anaamuru kuuliwa, na kwa siasa hii ikawa kuna mwanya wa kufitinisha na kukomoana, inatajwa kwamba waziri wake Abu Ubaydullahi Muawiya bin Yasaar alikuwa ni mwanafasihi mjuzi, naye ni mtu wa kwanza aliyeandika kitabu katika mapato, ilitokea hali ya kutoelewana baina ya waziri huyu na Rabi'i aliyekuwa mlinzi, hivyo mlinzi akataka kumkomoa, akamfitinisha kwa al-Mahdiykwamba waziri wako ana mtoto jina lake ni Muhammad, naye anatuhumiwa katika dini yake. al-Mahdiy akasema: “Niletee.” Alipoletwa akasema: “Ewe Muhammad: Soma Qur'an.” Akasoma vibaya kwa kuzingatia kuwa yeye ni kijana, na kwakuwa ni mbele ya khalifa akakanganyikiwa na hakuweza kusoma vizuri. al-Mahdiy akamgeukia baba yake na kumwambia: “Ewe Muawiya je, hukuniambia kwamba mwanao amehifadhi Qur'an?” Akasema: Ndio nilikwambia, ewe kiongozi, lakini yeye ametengana na mimi miaka mingi na katika muda huu amesahau Qur'an.” al-Mahdiy akasema: “Simama jikurubishe kwa Mwenyezi Mungu kwa damu yake.” Akasimama ili afanye hivyo lakini akaanguka. Mmoja kati ya wahudhuriaji akaingilia kati, naye ni Abbasi bin Muhammad, akasema: “Ewe kiongozi ukipenda msamehe mzee.” Akafanya hivyo, lakini bado al-Mahdiy aliamuru mtoto wake akakatwa kichwa."

Njia hii haikubaliwi na akili wala dini, sasa ni ipi njia ya sawa?

Pili: Ni Kuathiri Wengine kwa Njia ya Majadiliano na Kukinaisha:

Nayo ndio njia inayoamrishwa na Qur'an tukufu, anasema (swt):

"Waite kwenye njia ya Mola Wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola Wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka." (Surat Nahli: 125).

Hekima: Inatokana na udhibiti, nayo ni kuweka kitu mahala pake,unapotaka kumkinaisha mtu chagua maneno yanayofaa, hoja inayofaa na njia inayofaa, na hekima inamaanisha kuisemesha akili kwa dalili.

Mawaidha mazuri: Inamaanisha kuathiri utu na hisia nzuri, kiasi kwamba mawaidha hayawi makali.

Na inawezekana upande mwingine una shubuha, hivyo kuwa tayari kupokea rai yake na jadili pamoja naye, huu ndio uongofu wa mbinguni na maelekezo yake, kujadili na kuzungumza pamoja naye kwa njia bora zaidi na mazungumzo mazuri Zaidi: “Na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.”