Change Language: English

Chemchem Ya Uhuru Imamu Husain Sayyid ash-Shuhada [a] Shukrani

Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Urdu na Mtukufu Sayyadul Ulama Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb, Mujtahid wa huo Kikuu cha Lucknow, Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa Lugha ya Kiingereza na Sayyid Hashim Raza Rizvi, B.A., B.T., Yadgar-e-Husayni H.S. School, Allahabad, Uhindi na kutolewa na Imamia Mission, Lucknow U.P., Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kutoka hiyo tafsiri ya kiingereza na Marehemu Bwana L.W. Hamisi Kitumboy aIiyekuwa Mubalighi Mkaguzi wetu) na kikachekiwa na kusahihishwa na Mwalimu Dhikiri (Zakir Ali) U.M. Kiondo. Edita wa "Sauti ya Bilal".

Utangulizi

Maisha ya mwanadamu ni mnyororo wa mapambano. Ni lazima apambane katika kuyashinda mapenzi yake na misukumo ambayo ni lazima imkabili kwa vile yu mwanadamu, naye ni lazima kuwa macho katika unyonge wake na kuyatii maamrisho yote ya akili zake kuhusu mambo yote anayoamini kuwa ni bora zaidi kuliko aina zote za starehe.

Na kwa upande mwingine ni lazima ajiambatanishe na njia yake ya ukweli katika meno ya nguvu zote zinazompinga ambazo humkingia njia yake. Hana budi kupigana na dhoruba ya fikara, mapokeo, faida za daima na zile nguvu zote za dhuluma na uovu ambazo humfikiria mtu huyu kuwa yu mwovu, na hivyo kumfanyia chanzo cha kuyarudisha nyuma maendeleo yake.

Vitabu vya akhlaki (elimu ya tabia nzuri au mema na mabaya vimejaa mafundisho ya kale, lakini tunahitaji kuona mifano ya siku hizi ya kutushawishi, kuifuata mifano hiyo. Imamu Husayn [a] alikuwa mfano wa aina hiyo.

Nasaba

Sayyidina Abu Abdallah Husayn [a] alikuwa lmamu wa Tatu wa nyumba ya Mtukufu Mtume [s]. Alikuwa mwanawa binti wa Mtukufu Mtume [s], Bibi Fatimah [a], binti ambaye Mtume [s] alikuwa akisimama kuonyesha heshima yake kila alipoingia mahali alipokuwepo Mtume [s]. Baba yake alikuwa Sayyidina Ali [a] binamu yake Mtume [s] na alikuwa mjukuu wa Mtume [s].

Kuzaliwa Kwake

Imamu Husayn [a] alizaliwa mnamo siku ya Alhamisi tarehe tatu ya mwezi wa Shaaban mnamo mwaka wa nne wa Hijiriya. Alipozaliwa Mtume [s] alikuja, akamchukua mikononi mwake na akatia ulimi wake kinywani mwa mtoto huyu mchanga ambaye aliunyonya.

Mnamo siku ya saba ilifanyika sherehe ya Aqiqa (kunyolewa kwa nywele alizozaliwa nazo mtoto). Kuzaliwa kwa mtoto huyu kulikuwa chanzo cha furaha kwa familia yote lakini Mtukufu Mtume [s] alijua yatakayomtokea mtoto huyu baadaye na hivyo alilia sana. Tokea wakati huo jamii nzima ya Mtume [s] ilianza kuyazungumzia masaibu ya maishani mwake yatakayomsibu na ambayo yatahusiana kabisa na maisha yake.

Kulelewa Kwake

Mtukufu Mtume [s] alikuwa akiwalea wajukuu zake Hasan [a] na Husayn [a] na vile vile alikuwa akiulea Uislamu; na Hadhrat Ali [a] na Bibi Fatimah [a] walikuwa nao vile vile wakiwalea watoto hawa ambao Mtukufu Mtume [s] aliwaita wanawe. Alikuwa akiwachukua popote pale aendapo. Mara nyingi Imamu Hasan [a] alikaa katika bega lake Ia kuume na Imamu Husayn [a] alikaa katika bega lake Ia kushoto. Kila mara Mtume [s] aliwataka Waislamu wawapende hao watoto wake Mtume [s], na mapenzi yake kwa Imamu Husayn [a] yalikuwa na kiwango kikubwa.

Mtume [s] alipokuwa akisali, Imamu Husayn [a] alikuwa akija na kukaa mgongoni pake. Mtume [s] alikuwa akiendeleza Sajdah yake mpaka Imamu Husayn atelemke kwa hiari yake. Wakati fulani Imamu Husayn [a] alikuja kwenye Msikiti wa Mtume [s], msikiti wa mjini Madina, wakati Mtume [s] alipokuwa akihutubia. Imamu Husayn [a] alijikwaa na kuanguka chini. Mtume [s] mara moja aliacha kuhutubia, akateremka chini na kumnyanyua mwanawe kwanza. Kisha aliwahutubia watu waliokuwepo hapo akisema, "Huyu ni Husayn; mfahamuni vizuri".

Vile vile Mtume [s] alisema, "HUSAYN ANATOKANA NA MIMI, NA MIMI NINATOKANA NA HUSAYN", akiwa na maana ya kuwa lmamu Husayn [a] alikuwa ndio maisha ya Mtukufu Mtume [s] na jina Ia Mtume [s] litadumu kupitia kwake.

Kufariki kwa Mtume [s]

Alipofariki Mtume [s] Imamu Husayn [a] alikuwa na umri wa miaka sita tu. Kipindi cha miaka ishirini na mitano kilichofuatia ambacho Imamu Ali [a] aliishi maisha ya kujitenga, Imamu Husayn [a] alipata muda wa kutosha kujifunza tabia za babiye. Mafunzo haya yalichukua muda wa ujana wake na alipokuwa na umri wa miaka thelathini na moja baba yake alipewa Ukhalifa. Imamu Hasan [a] alifuatana na babiye katika vita za Jamal, Siffin na Nahrawan. Katika mwaka wa 40 Hijiriya Hadhrat Ali [a] alikufa kishahidi katika msikiti wa Kufa (Iraq) na Imamu Hasan [a] alilazimika kuzishika kazi za Ukhalifa. Imamu [a] Husayn akiwa ndugu mtiifu, alimsaidia Imamu Hasan [a] na Imamu Hasan [a] alipofanya mapatano na Muawiyyah ili kuziokoa haki za Uislamu, Imamu Husayn [a] nae aliishi maisha ya kujitenga kama alivyofanya Imamu Hasan [a].

Imamu Husayn [a] alitumikia Uislamu kimya kimya kwa muda wa miaka ishirinl. Miaka kumi chini ya kaka yake Imamu Hasan [a] na miaka kumi baada ya kifo cha Imamu Hasan [a]. Lakini katu Muawiyyah hakuyatimiza masharti ya mapatano aliyoyafanya na Imamu Hasan [a]. Alimtilia sumu Imamu Hasan [a] na akawasumbua sana wafuasl wa Imamu Ali [a] na akawafunga, akawakata vichwa na hata kuwasulubisha. Mwishoni kabisa alivunja masharti ya mapatano kwa kumchagua mwanawe Yazid kuwa mrithi wake na alitumia kila aina ya nguvu na propaganda ili kuungwa mkono wa Waislamu.

Tabia Yake

Imamu Husayn alikuwa lmamu wa tatu na alikuwa mcha Mungu na mnyofu sana. Hata maadui wake waliukubali ukarimu wake na sifa zake nzuri. Alikuwa akienda Sajdah elfu moja katika muda wa masaa ishirini na manne (siku moja). Alikwenda Hija mara ishirInI na tano kwa miguu. Mtukufu Mtume [s] yeye mwenyewe alisema, "Husayn ana ushupavu na ukarimu wangu".

Mlangoni pake kila wakati palikuwa na maskani na kila mara nyumba yake ilijaa wageni na hakuna mtu yeyote yule aliyerudi kutoka nyumbani kwa Imamu Husayn [a] bila ya kuridhika. Kwa sababu hiyo alikuwa akijulikana kwa jina la "Baba wa maskini". Alikuwa na kawaida ya kuchukua mikungu ya tende na mikate wakati wa usiku kwenda kuwapa watu fukara na maskani. Na kazi hizi za usiku ziliweka alama katika mgongo wake. Kila mara alikuwa akisema, "Kama akikujia maskini yeyote yule kutaka msaada, ina maana kuwa maskini huyo kakuuzia heshima yake na sasa ni wajibu wako kutomrudishia akiwa na wazo baya kuhusu heshima yako."

Jinsi alivyokuwa akiwatendea watumwa na watumishi wake ilikuwa na kama vile atendavyo baba mwenye huruma. Kila mara alikuwa akitafuta nafasi ya kuwapatia uhuru.

Watu wote wa wakati wake waliitambua vizuri elimu yake bora. Katika kila tatizo Ia kidini aliendewa na kutakiwa alitatue tatizo hilo. Mkusanyo wa Sala zake unaoitwa "Sahifah Husayniah" (kitabu cha Husayn) upo hadi sasa.

Ailkuwa na huruma sana kiasi ambacho aliwaonea huruma hata maadui zake. Kila mara aliwashughulikia sana maskini wa watu wengine kabla ya wale maskini wake. Imamu Husayn [a] akiwa na sifa zote hizi nzuri. Alikuwa mpole na mnyenyekevu sana kiasi ambacho siku moja alipokuwa akipita mahali Fulani maskini fulani walimkaribisha kula chakula pamoja nao. Imamu [a] alikwenda kukaa pamoja nao ingawa hakuweza kula nao kwa kuwa sio halali kwa watu wa nyumba ya Mtukufu Mtume [s] kutumia chochote kile kilichotolewa sadaka.

Matokeo yake yalikuwa kila awapo, watu hawakuweza kumtazama. Aliheshimiwa sana kiasi ambacho hakuna mtu ye yote yule aliyezikataa sifa zake nzuri, hata wale wa kabila lililokuwa adui kwa ukoo wake. Siku moja alimwandikia barua kali sana Muawiyyah akimlaumu kwa matendo yake yasiyo sahihi. Muawiyyah alipoisoma barua hiyo alichomwa sana moyoni. Wafuasi wake walimshauri amwandikie Imamu [a] barua kama hiyo. Muawiyyah alijibu, "Kama nikiandika mambo yasiyo ya kweli katika barua hiyo basi barua hiyo haitatimiza lengo lake, na kama nikijaribu kutafuta upungufu wowote ule katika tabia zake (lmamu Husayn [a]), Wallah, nashindwa kupata wowote ule".

Masaibu ya Karbala wanaonyesha sura ya ushujaa wake, ukweli, nia, uvumiIivu, ustahimilivu na amani. Hakuzilegeza juhudi zake katika kufanya mapatano hadi mwisho, lakini hakukubali kugeuka japo inchi moja kutoka kwenye njia yake ya wajibu wake na aliridhika kufa kuliko kufanya hivyo.

Aliishi akiwa mwana chini ya baba yake Imamu Ali [a] na akiwa ndugu mdogo wa Imamu Hasan [a] na aliwatii kwa kuwa ilikuwa haki kwake kufanya hivyo. Huko Karbala aliwaongoza watu wake vizuri sana kama alivyowatii wakubwa wake. Imamu Husayn [a] yu mnara wa taa ya Uongozi kwa wanadamu wote.