Change Language: English

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyoangazia macho chimbuko la makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine na kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao hii leo ikiwa ni sehemu ya 20 ya vipindi hivyo.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia kwa ufupi matukio yaliyojiri katika nchi za Kiislamu mwaka 2011 ambayo yalizikumba nchi za kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati ikiwemo Misri na namna ambavyo matukio hayo yalivyowastaajabisha viongozi wa Ikhwanul Muslimin nchini humo. Aidha Tukaashiria mahusiano ya viongozi wa Ikhwanul Muslimin wakiongozwa na rais wa zamani wa Misri Muhammad Mursi, kwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na utawala wa kifalme wa Aal Saudi nchini Saudia. Kadhalika katika kipindi kilichopita tuligusia uungaji mkono wa Ikhwanul Muslimin kwa makundi ya kitakfiri na kigaidi yanayotekeleza jinai huko nchini Syria na Iraq, na kimya cha viongozi wa harakati hiyo kwa jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Sheikh Hassan Muhammad Shehatah, mwanazuoni wa Kishia wa nchini Misri.

Katika kipindi hiki tuntaendelea na mfululizo huo, hivyo endeleeni kuungana nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ndugu wasikilizaji mnapaswa kufahamu kwamba, mauaji dhidi ya Sheikh Hassan Muhammad Shehatah na watu wengine watatu miongoni mwa wafuasi wa Ahlul-Bayti wa Mtume (as), yalijiri katika kipindi ambacho Muhammad Mursi alikuwa bado yumo ikulu ya Misri. Hata hivyo si kiongozi huyo wala wa Ikhwan waliotoa tamko lolote la kulaani mauaji hayo dhidi ya Waislamu hao wa Kishia. Baadaye Ikhwan walipata pigo kali kutokana na kujiaminisha kwao kwa utawala wa Kiwahabi wa Aal Saud na harakati nyingine za Kiwahabi duniani. Baada tu ya kuondolewa madarakani Muhammad Mursi, watawala wa Saudi Arabia walitoa msaada wa mabilioni ya Dola za Marekani kwa askari wa Misri walioongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais huyo wa zamani wa nchi hiyo. Ukweli ni kwamba, baada ya kuondolewa madarakani dikteta Hosni Mubarak, utawala wa Aal Saudi ulifanya kila aina ya ya njama ili kufelisha mapinduzi ya raia wa Misri. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Ikhwanul Muslimin hawakufahamu nani adui na nani rafiki wao baada ya kujiri mapinduzi hayo ya kihistoria nchini Misri. Kosa hilo liliigharimu harakati hiyo na raia wa Misri, gharama ambayo ni muhali kuweza kufidiwa katika katika historia ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

*******************************************

Baada ya kusema hayo, sasa umewadia wakati wa kujadili maudhui mpya ambayo itahusu malengo hasa ya kuleta maudhui hizi ambazo sasa zimefikia sehemu yake ya 20 katika kubainisha msingi wa Usalafi na Uwahabi na tofauti zilipo baina yao.

Kwa hakika misingi ya itikadi ya harakati za utakfiri na ugaidi ni mambo yanayotokana na fikra za Uwahabi. Hii ni kusema kuwa, Uwahabi ndio asili ya utakfiri na ugaidi kote duniani. Katika fremu hiyo tutajaribu kuangazia macho chimbuko la Uwahabi kwa mujibu wa historia. Na hapa tutabainisha pia makundi matatu ya Usalafi kwa mujibu wa historia hiyo.

Kundi la kwanza katika Usalafi ni Usalafi wa upokezi wa riwaya na kundi la pili ni la Usalafi wa itikadi. Ama kundi la tatu ni Usalafi wa Kiwahabi ambao hii leo bendera yake inashikiliwa na Saudia. Moja ya masuala makubwa yaliyoibua tofauti miongoni mwa Waislamu na kuibua mpasuko katika ulimwengu wa Kiislamu, ni suala la upokezi. Kwa hakika suala hilo liliibua maswali na shubuha nyingi katika Uislamu. Miongoni mwa shubuha hizo kamavile: ni upi ukomo wa nafasi ya akili na upokezi katika dini? Na ni kwa kiasi gani inatakiwa kutumiwa akili katika shughuli hiyo?

Kwa hakika maswali hayo yaliwaweka katika wakati mgumu sana Waislamu wa karne za mwanzo na hivyo kusababisha kuibuliwa kwa makundi na mirengo kadhaa. Watu wa kundi moja sanjari na kupuuza suna za Mtume Muhammad (saw) na tafsiri ya Qur’an Tukufu wakategemea akili zao kwa kiasi cha kufurutu ada. Ama baadhi sambamba na kupinga kikamilifu akili, wakatumbukia katika lindi la upokezi wa hadithi kwa namna ya kufurutu ada kiasi cha kupiga marufuku utumiaji akili hata kwenye hadithi dhaifu zisizokubalika akilini. Ni kwa ajili hiyo, karne za mwanzo wa kudhihiri dini ya Kiislamu, kukashuhudiwa mirengo miwili ya utumiaji akili na mwingine wa upokezi, ambapo upande fulani ulifurutu ada katika uga wa akili huku mwingine ukifanya tafritwi kwa kupuuza zaidi uwanja huo. Katika hilo, Masalafi wa Kiwahabi wao wakafuata upande wa upokezi wa kufurutu ada. Mawahabi hao sanjari na kuitupilia mbali akili na kufurutu katika upokezi, wakawatwisha nafasi ya umarjaa wa kielimu watu wa zamani, na kuwafanya kuwa watu bora kuliko wale wa baada yao. Ukweli ni kuwa, kitendo cha kufungamana kwao na watu wa zamani kielimu na katika kila jambo ikiwemo maneno na vitendo hususan masahaba na taabiina na waliokuja baada yao, kiliwafanya Mawahabi hao kukimbia na kukwepa majukumu na changamoto za ulimwengu wanaoishi na unaowazunguka na badala yake wakaamua kuwasukumia majukumu hayo watu wa kabla yao (yaani Salaf). Alaakulli haali! upokezi na kukumbatia hadithi kwa kiasi cha kupindukia mipaka, ni mambo ambayo yalikuwa sehemu ya maisha ya watu wa kundi hilo lenye fikra na mitazamo iliyopitwa na wakati.

**********************************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilichohewani ni makala ya utakfiri yanayokujia kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hii leo ikiwa ni sehemu ya 20 ya makala hizo.

Ndugu wasikilizaji ni suala lililo wazi kwamba, baada ya Qur’an Tukufu, suna za Bwana Mtume Muhammad (saw) ikiwemo hadithi, ni njia ya pili katika kumuongoza mwandamu. Hata hivyo haipaswi kusahaulika kuwa, kuna tofauti katika utambulisho wa neno hilo hadithi. Kwa mujibu wa baadhi ya wasomi, neno suna linahusu kufahamu maisha na historia ya Mtukufu Mtume wa Uislamu (swa). Aidha neno suna limetajwa kuwa ni kila kitu ambacho Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alikitenda kuanzia vitendo, kauli, kunyamanzia jambo lililofanywa mbele yake, kuanzia sifa na tabia za kiakhlaqi. Aidha Ahlus-Sunna wanaamini kuwa, baada ya kufariki dunia Mtukufu Mtume Muhammad, kama ambavyo wahyi ulikata, ndivyo ambavyo masuala ya dini yalitimia na kwamba, tangu wakati huo Waislamu walikuwa na wadhifa wa kuyasimamia mambo yao wao peke yao. Hata hivyo kwa upande wao Waislamu wa Kishia wanaamini kuwa, kukatika wahyi kulikotokana na kufariki dunia Nabii wa Allah (saw), haikuwa mwisho wa mahitaji ya Waislamu bali ni kwamba umma wa Kiislamu bado unahitaji mtu maasumu (asiyefanya dhambi) mwenye alimu ya hali ya juu kwa ajili ya kufafanua aya, hadithi na sheria za Mwenyezi Mungu na pia kutatua matatizo na changamoto mbalimbali za Waislamu hao. Itafahamika kuwa, Waislamu wa Kisuni wanaamini uimamu kama ni uongozi mkuu wa kijamii, ingawa hawaamini kama ni marjaa ya kidini au wilaya kwa umma wa Kiislamu. Ama jambo la kushangaza ni hili kwamba, Ahlus-Sunna wenyewe hawaamini mtu yeyote katika masahaba akiwamo Abubakar, Omar, Othman kwamba waliweza kufikia daraja na cheo hicho na ndio maana wanaamini kuwa, khalifa sio lazima awe mtakatifu asiyefanya dhambi. Hata hivyo kwa upande wao, Waislamu wa Kishia wanaamini kuwa, maimamu ni maasumina watakatifu na ambao hawafanyi dhambi wala kosa lolote. Aidha Mashia wanaamini kuwa, baada ya kufariki dunia Mtukufu Mtume Muhammad (saw), maimamu 12 ambao waliteuliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuiongoza jamii ya Kiislamu, walirithi elimu ya Mtukufu Mtume kwa ajili ya kubainisha aya za Qur’an Tukufu na suna za Mtume. Aidha watukufu hao, mbali na kuwa mahatibu, walikuwa wakijibu maswali na matatizo mbalimbali ya Waislamu waliokuwa wakija kwao kuuliza. Ni kwa msingi huo ndio maana Mashia sanjari na kutegemea elimu pana ya maimamu (as) wakaweza baada ya kufariki dunia Mtume Muhammad (saw), wakaweza kutatua matatizo na shubuha mbalimbali za kielimu hata baada ya kupita muda mrefu.

**********************************************

Aban ibn Taghlib, mmoja wa maulama wa Ahlus-Sunnah anawazungumzia Waislamu wa Kishia kwa kusema: “Mashia ni watu ambao baada ya watu kuhitilafiana katika amri za Mtume Muhammad-saw- na watu wa nyumbani kwake, wao walishikamana na Imam Ali-as-. Na baada yake, wakati watu walipohitilafiana tena kuhusiana na misingi ya sheria za Kiislamu wao wakashikamana na mafundisho ya Imam Swadiq-as.” Mwisho wa kunukuu. Katika hali ambayo Waislamu wa Kishia baada ya kufariki dunia, walijibu maswali ya kielimu na shubuha kwa kuwafuata Ahlu-Bayti (as), Waislamu wa Kisuni wao walikabiliana na changamoto kama hizo kwa kutegemea akili yao wenyewe. Hii ni kwa sababu baada ya kufariki dunia, Masuni walishikamana tu na hadithi za Mtume (saw). Hakuna shaka kwamba, riwaya hizo kwa kiasi fulani ziliweza kupunguza mahitaji ya kielimu, hata hivyo hatua ya makhalifa walioshika utawala baada ya Mtume kupiga marufuku uandishi wa hadithi, ilisababisha kupotosha vyanzo vya kuchukulia elimu Waislamu wa Kisuni. Makhalifa wa kwanza na wa pili, kwa madai ya kile walichokisema kuwa ni kuzuia tofauti baina ya Waislamu kuhusiana na riwaya za Mtume, waliamua kupiga marufuku uandishi wa hadithi za mtukufu huyo. Katika upande fulani walifungua upande wa kujibu maswali ya kidini na kwa upande mwingine wakazisusia kabisa suna za Bwana Mtume na kuzifanya kuwa kosa kunakili hadithi hizo.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengewa kipindi hiki umefikia ukingoni. Tutakutana tena katika sehemu ya 21 ya mfululizo wa vipindi hivi wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar hadi wakati huo nakuageni kwa kusema, kwaherini.